
Nchini Mali, kwa mujibu wa agizo la rais lililopitishwa siku ya Jumanne, Mei 13, wakati wa mkutano usio wa kawaida wa Baraza la Mawaziri, vyama vya siasa na mashirika ya kisiasa yamefutwa kote nchini. Uamuzi wa kufutwa kwa vyama vya siasa na mashirika hayo umekuwa ukiandaliwa kwa wiki kadhaa na umezua wimbi kubwa la maandamano nchini humo.
Imechapishwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
Tangazo hilo limetolewa kwenye televisheni ya serikali ORTM na Mamani Nassiré, Waziri Mjumbe kwa Waziri Mkuu mwenye dhamana ya Mageuzi ya Kisiasa na Kusaidia Mchakato wa Uchaguzi. Mikutano na shughuli zingine za vyama vya siasa na mashirika, ambayo sasa yamefutwa, ni marufuku, chini ya adhabu ya vikwazo. Watu wanaohudumu katika taasisi za kisiasa na kiutawala za Serikali kwa sababu ya kuteuliwa kisiasa wanaweza kuendelea na majukumu yao, lakini bila kudai kuwa ni sehemu ya chama chao.
Serikali ya mpito inabainisha kuwa hatua hii inafuatia kufutwa kwa mkataba wa vyama vya siasa. “Tuko katika mchakato wa mageuzi,” ameeleza Mamani Nassiré, akibainisha kuwa mchakato huo utaendelea. Itabidi sheria mpya itungwe hasa kwa ajili ya usimamizi wa maisha ya kisiasa ya Mali. Miongoni mwa malengo yaliyowasilishwa tayari: kupunguza idadi ya vyama vilivyoidhinishwa, kuimarisha sheria za kuunda vyama vipya, kuzuia au hata kupiga marufuku ufadhili wao wa umma.
Katika wiki za hivi karibuni, vyama vya siasa vya Mali viliendelea kushutumu kufutwa kwao kuliopangwa, ambao wanachukulia kuwa ni ukiukaji wa Katiba na shambulio dhidi ya wingi na mafanikio ya kidemokrasia. Vuguvugu la maandamano ambalo halijawahi kushuhudiwa nchini humo lilizuka mapema mwezi huu, lakini baadhi ya viongozi wake kadhaa wametekwa nyara na Usalama wa Taifa katika siku za hivi karibuni, na kuwanyamazisha wanaharakati wanaounga mkono demokrasia.
“Tumerudi kwenye udikteta”
“Sio mshangao,” mmoja wao amesema. Tutaendelea kupambana, hata kizani. Kufutwa huku kunaongeza matatizo mengi ambayo Mali inakabiliana nayo. “Ni mwendelezo wa kimantiki,” amesema waziri wa zamani, “lakini ni wa uzito na ambao haujawahi kutokea. “Uamuzi huu “unafungua njia kwa mamlaka ya kiimla,” anajibu kwa hasira mwanasiasa aliye mstari wa mbele katika maandamano. “Lakini mawazo yetu yataonyeshwa kwa njia moja au nyingine. Wasiwasi wao pekee ni kushikilia madaraka. Pambano litafayika na tutashinda.”
“Kwa agizo hili, tumerudi rasmi katika zama za udikteta,” mpinzani mwingine amelalamika, akimaanisha utawala wa kijeshi wa Jenerali Moussa Traoré, ambaye alitawala Mali hadi mwaka 1991. “Mapambano yanaonekana kuwa magumu, lakini watu wa Mali wamefunzwa kihistoria na kushikamana na demokrasia,” chanzo hiki kimeongeza, kikitoa mfano wa katiba ya Mandé ya 1236, ambayo mara nyingi huzingatiwa kama tamko la kwanza la haki za binadamu.
Baadhi ya viongozi wa kisiasa, ambao daima wana nia ya kubaki ndani ya sheria, tayari wanazingatia hatua za kisheria kupinga hatua hii. Lakini kwa vile vyama vya kisiasa sasa vimevunjwa, hatua hizi zinazowezekana haziwezi hata kufanywa kwa jina lao. Kuhusu uhamasishaji wa “raia”, uko wazi zaidi kuliko hapo awali kwenye hatari ya ukandamizaji.