
Katika dunia ya sasa inayosonga mbele kwa kasi kutokana na maendeleo ya teknolojia, familia zinakabiliwa na changamoto nyingi katika malezi ya watoto. Kuwepo kwa baba na mama katika maisha ya mtoto, kunaleta msingi imara wa maendeleo yake ya kihisia, kiakili na kijamii.
Wataalamu wa malezi wanasema ili kukabiliana na hilo, wazazi wanapaswa kuwa pamoja katika kuwalea watoto wao kwa uangalifu, kuhakikisha wanakuwa katika maadili na mwongozo mzuri wa maisha. Leo natazama umuhimu wa malezi ya pamoja ya baba na mama, changamoto zinazoletwa na maendeleo ya teknolojia katika familia na hatua zinazoweza kuchukuliwa ili kuhakikisha ustawi wa familia.
Wazazi wanapaswa kuzingatia kuwa malezi kutoka kwa baba na mama hujenga msingi wa utu na maadili katika maisha ya mtoto. Kila mzazi ana mchango wake muhimu.
Mama ni mlezi wa karibu anayehakikisha kuwa mtoto anapata upendo na malezi ya msingi tangu utotoni. Kwa mujibu wa wanasaikolojia, hutoa msaada wa kihisia na humfundisha mtoto misingi ya huruma, uelewa na mshikamano wa kifamilia. Mara nyingi mama ndiye anayekuwa na ukaribu wa moja kwa moja na mtoto, hivyo ni wazi kuwa anayo nafasi nzuri ya kumfundisha nidhamu na tabia njema.
Lakini baba naye anao mchango wake mkubwa sana katika hili. Tangu enzi na enzi, baba ndiye kielelezo cha nidhamu, ujasiri na uongozi katika familia.
Kwa sababu ndiye anayeaminika kwamba humfundisha mtoto umuhimu wa uwajibikaji, bidii katika kazi sambamba na kujitegemea.
Hivyo katika utafiti mdogo nilioufanya unaonesha kuwa baba anahusika moja kwa moja katika kuimarisha hali ya kiuchumi ya familia, mchango wake unahakikisha ustawi wa familia japo kuwa kwa nyakati tulizo nazo kina mama nao wanafanya mambo makubwa ya maendeleo kwenye familia zao.
Hali hii inatuonyesha kuwa wazazi wanaposhirikiana katika malezi ya watoto wao, wanawapa msingi imara wa kujiamini, kufanya uamuzi sahihi kwa mustakabali wa maendeleo ya familia.
Hii yote ilikuwa inawezekana kirahisi nyakati hizo ikilinganishwa na sasa. Hivi sasa teknolojia imeleta maendeleo makubwa, lakini pia imeathiri malezi ya watoto kwa njia tofauti.
Baadhi ya changamoto zinazoathiri familia nyingi. Tunaambiwa hivi wazazi wengi wanakuwa na shughuli nyingi kazini au wanatumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii, hivyo kupunguza muda wa kukaa na watoto wao.
Kumbuka kuwa malezi ya baba na mama ni nguzo muhimu katika maisha ya watoto, hasa katika dunia ya sasa inayotawaliwa na maendeleo ya teknolojia.
Kwa maana hiyo, ushirikiano wa wazazi katika malezi kunasaidia kujenga kizazi chenye maadili, heshima na uwajibikaji. Pamoja na changamoto zinazoletwa na teknolojia, wazazi wanapaswa kujitahidi kuweka mipaka ya matumizi yake, ili kuimarisha mawasiliano na watoto wenu.
Na wanapaswa kuwa mfano bora wa kuigwa na wanenu na kwaa kufanya hivyo, familia itaendelea kustawi na jamii itanufaika na kizazi bora kinachokuja. Kinyume na hapo, watoto watajiona kama wameachwa peke yao, jambo linaloweza kuathiri maendeleo yao ya kihisia.
Hapo sasa ndipo wengi wao huamua kutumia muda mwingi kwenye simu na kompyuta, jambo linaloweza kuwaathiri kimaendeleo hasa ya kiakili.
Wakati mwingine mtoto anaweza kujiingiza kwenye kutazama maudhui yasiyofaa yanayopatikana kwa urahisi mitandaoni hali inayoweza kuchangia kuwaharibu kimaadili.
Nasema hivyo kwa sababu tayari tumeshashudia namna mawasilianoya ana kwa ana baina ya wazazi na watoto yanavyodhoofishwa na vifaa kama simu na kompyuta mpakato.
Sasa ukikuta nyumba ina mzazi mmoja, hali ndiyo huwa mbaya zaidi. Sasa Ili kuhakikisha kuwa familia inastawi vema katika dunia hii ya teknolojia, wazazi wanapaswa kuhakikisha wanatumia muda wa kutosha kuzungumza na watoto wao.
Wazazi wanapaswa kuonyesha mfano mzuri kwa watoto kwa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya simu na mitandao ya kijamii. Na wanapaswa kuwa tayari kuwasikiliza watoto wao na kuwapa nafasi ya kueleza hisia na changamoto wanazopitia.
Mazungumzo ya mara kwa mara, husaidia kujenga uaminifu na mshikamano wa kifamilia na watoto hujikuta huru zaidi kufanya kitu chochote nyumbani, hali inayosaidia kuwaepusha na changamoto za kiteknolojia na hatimaye watajikuta wakikua kwa kujitambua zaidi na kuwa wema mbele ya uso wa jamii.