Malaysia yasisitiza Israel ifukuzwe Umoja wa Mataifa kwa mauaji ya kimbari unayofanya Ghaza

Waziri Mkuu wa Malaysia Anwar Ibrahim amesisitiza kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel inapasa utimuliwe katika Umoja wa Mataifa kutokana na ukiukaji haki za binadamu na mauaji ya kimbari unayofanya katika Ukanda wa Ghaza.

Anwar Ibrahim amesema, “hatua kali, ikiwa ni pamoja na kuondolewa Israel katika Umoja wa Mataifa kwa kukiuka haki za binadamu na kufanya mauaji ya kimbari huko Ghaza, lazima zitekelezwe haraka iwezekanavyo.”

Rais wa Malaysia ametoa wito huo alipowahutubia wabunge wa nchi hiyo na kuongeza kuwa, rasimu ya azimio hilo iko katika hatua ya majadiliano na inatarajiwa kuwasilishwa “hivi karibuni” kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ili kuidhinishwa.

Waziri Mkuu wa Malaysia ametoa matamshi hayo wakati hivi karibuni Francesca Albanese, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu katika ardhi za Palestina naye pia alitoa wito wa kusitishwa uanachama wa utawala wa Kizayuni katika Umoja wa Mataifa akiashiria ukiukaji wa mara kwa mara wa sheria za kimataifa na uvamizi na ukaliaji wa mabavu ardhi za Palestina unaofanywa na utawala huo ghasibu…/