Malale Hamsin atua Mbeya City

UONGOZI wa Mbeya City umemalizana na aliyekuwa kocha wa JKT Tanzania Malale Hamsin baada ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo kutimkia Mashujaa.

Malale ameungana na Mbeya City akiwa kocha huru baada ya kuachana na JKT Tanzania mwanzoni mwa msimu huu amekabidhiwa mikoba ya Salum Mayanga aliyetimkia Mashujaa akiiacha City nafasi ya pili kwenye msimamo wa Championship.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Mbeya City kimeliambia Mwanaspoti kuwa uongozi wa timu hiyo upo kwenye hatua za mwisho kumalizana na Hamsin na muda wowote kuanzia sasa watamtambulisha kama kocha mkuu.

“Timu ilikuwa chini ya Patrick Mwangata tangu alipoondoka Mayanga sasa Hamsin anakuja kuongeza nguvu lengo ni kuona timu inarejea tena ligi kuu na tuna imani kubwa na wachezaji sambamba na benchi la ufundi malengo yatatimia,” alidokeza mmoja wa viongozi wa Mbeya City na kuongeza;

Chanzo hicho kilisema Malale ataungana na City muda wowote kuanzia sasa ili kusukuma gurudumu kwa kuhakikisha timu hiyo inarudi tena Ligi Kuu baada ya kushuka 2022-23.

Hadi sasa timu hiyo imecheza mechi 26 za Championship ikishinda 16, sare saba na kupoteza michezo miwili, ipo nafasi ya pili kwenye msimamo baada ya kukusanya pointi 55, huku safu yake ya ushambuliaji ikifunga mabao 50 na kuruhusu 21.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *