Malalamiko mikopo ya asilimia 10 yamuibua Zungu bungeni

Dodoma. Naibu Spika wa Bunge, Musa Zungu ameitaka Serikali kufuatilia malalamiko ya vikundi vinavyoomba mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu kuwa hawatendewi haki na baadhi ya watendaji na maofisa maendeleo.

Zungu ameyasema hayo leo Jumatano Februari 12, 2025 wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni baada ya Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Zainab Katimba kujibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Sylvia Sagula.

“Mheshimiwa waziri nikuombe kuna malalamiko mengi sana kwa wananchi kwa watendaji wa kata baadhi ya maofisa maendeleo hawatendi haki kwa baadhi ya vikundi,” amesema.

“Aidha kwa makusudi kwa upendeleo ama kwa kutokujua, hebu jaribuni kulifuatilia hili suala na mtoe tahadhari kwa yeyote atakayehusika kuonea kikundi bila sababu maana hizi fedha ni za mama kwa watoto wake,” amesema.

Awali, Sagula katika swali lake la msingi, amehoji ni lini Serikali itarejesha mikopo ya asilimia 10 iliyokuwa ikitolewa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Akijibu swali hilo, Katiba amesema kutokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri ilisitishwa na Serikali Aprili 13, 2023 ili kupisha maandalizi ya utaratibu mpya wa utoaji wa mikopo hiyo.

“Kufuatia kukamilika kwa mfumo mpya wa utoaji wa mikopo, Serikali ilitangaza Julai 01 2024 mikopo hiyo kuanza kutolewa tena kwa mujibu wa sheria na kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo hiyo,” amesema.

Amesema Ofisi ya Rais – Tamisemi inaendelea kuzisimamia mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha zinatoa mikopo kwa mujibu wa sheria ambapo tangu mikopo kurejeshwa hadi Desemba, 2024 halmashauri 64 zimetoa mikopo ya Sh22.07 bilioni kati ya Sh27.76 bilioni zilizoombwa na vikundi 2,726 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Naibu Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mussa Azzan Zungu, akizungumza leo Februari 12, 2025 Bungeni Jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha

Amesema kati ya fedha hizo Sh21.88 bilioni zimetolewa kutokana na michango ya halmashauri (asilimia 10 ya mapato ya ndani) na Sh194.3 milioni ni mikopo iliyotokana na fedha za marejesho.

Februari 7, 2025, Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa aliwaonya viongozi kutocheza na fedha za mikopo hiyo na atakayebainika eneo lake lina kikundi hewa atawajibishwa.

Mchengerwa alitoa onyo hilo wakati wa hafla ya utiaji saini mikataba ya utoaji mikopo hiyo kati ya halmashauri 10 na benki tatu jijini Dodoma.

“Kabla ya waziri hajawajibika, atawajibika mkuu wa mkoa, wilaya na wakurugenzi, nawaambia wazi kabisa, tumefika hapa kwa sababu kuna watumishi wasio waaminifu ambao walitafuna fedha hizi kwa kukopeshana wenyewe na hawakuwa na sifa ya kupokea mikopo hii,” alisema Mchengerwa.

Alisema kanuni zimeboreshwa zinawapa nguvu maofisa maendeleo ya jamii na benki zinazotoa fedha hizo kufuatilia, kusimamia na kuvikagua vikundi kabla ya kutoa fedha hizo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Tamisemi, Profesa Adolf Ndunguru amesema kusainiwa mikataba hiyo ni mwanzo wa mapinduzi ya kuhakikisha mikopo hiyo ya asilimia 10 inakuwa na tija tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Mikopo hiyo imeanza kwa katika halmashauri tano za Jiji la Dar es Salaam na Dodoma, Manispaa ya Kigoma, Halmashauri ya Mji wa Mbulu, na Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kwa majaribio ambayo kwa sasa inatolewa kupitia benki.