Goma. Takriban vikundi vitatu vya wapiganaji wa kundi la wazalendo wanaoliunga mkono Jeshi la Serikali ya Jamhuri Kidemokrasia ya Congo (FARDC) Kivu Kaskazini wameasi na kujiunga na muungano wa makundi ya waasi wa Alliance Fleuve Congo (AFC/M23).
Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini DRC, taarifa iliyosainiwa na kiongozi wa wazalendo, Shukuru Bulenda, vikundi hivyo vilivyoasi ni pamoja na Mai-Mai Kabidon (FPP-AP), sehemu ya Mai-Mai Kifuafua na kikundi cha Nduma Defense of Congo-Renovated (NDC-R/M).
Vikundi hivyo, vinadaiwa kujiunga na AFC/M23, juzi Machi 9, 2025.
Kituo cha habari cha Kivu Morning Post kiliripoti jana kuwa wapiganaji wa muungano huo mpya walikuwa wakielekea kaskazini kutoka ngome zao za Kivu Kaskazini na Kusini kuelekea kijiji cha Kasugho, takriban maili 28 magharibi mwa Wilaya ya Lubero kwa lengo la kupambana na FARDC.

M23 imekuwa ikijaribu kuzunguka ngome za FARDC katika mji wa Lubero tangu mwishoni mwa Februari bila mafanikio.
M23 iliuteka Mji wa Kasugho Machi 2, 2025, kabla ya kuondoka Machi 7 na kuelekea Bunyatenge, eneo lenye machimbo ya dhahabu lililo umbali wa saa sita kutoka Kasugho nchini humo.
Vyombo vya habari vya DRC vimesema uasi wa wapiganaji wa FPP-AP kujiunga na M23 ni pigo kubwa kwa jeshi la FARDC katika mapambano ya kuidhibiti M23.
Pia, vimeielezea FPP-AP kama moja ya vikundi vyenye muundo mzuri na ushawishi mkubwa katika Jimbo la Kivu Kaskazini ambavyo vilikuwa vimepeleka mamia ya wapiganaji kwenye vijiji kadhaa katika Wilaya ya Lubero ili kuwazuia M23 kusonga mbele kuelekea Lubero, Butembo na Mji wa Beni.
Kituo cha habari cha DRC, Actualite.cd, kilisema kwamba FPP-AP ina ushawishi mkubwa katika wilaya ya Kaskazini magharibi ya Lubero, hasa katika mji wa machimbo ya dhahabu wa Maguredjipa, ulio maili 73 kaskazini magharibi mwa mji wa Lubero na unapakana na jimbo jirani la Tshopo.
Kituo hicho, kilimnukuu mtafiti wa ndani aliyesema kuwa kuingizwa kwa FPP-AP katika muundo wa muungano wa M23 kutairuhusu M23 kusonga mbele bila kuzuiliwa kutoka Kasugho hadi Manguredjipa kupitia Bunyatenge.
Wakati huo, Jeshi la FARDC na wanamgambo wa Wazalendo walipambana na waasi wa Twirwaneho na RED Tabara wanaotajwa kuwa tawi la M23 katika vijiji kadhaa karibu na mji wa Minembwe jana Machi 10, 2025.
FARDC ilifanya mashambulizi ya anga dhidi ya ngome za Twirwaneho huko Minembwe Machi 10, 2025.
Vyombo vya habari vya Congo viliripoti kwamba ndege zisizo na rubani za FARDC na ndege ya kivita ya FARDC zilishambulia maeneo ya Twirwaneho katika uwanja wa ndege wa Minembwe na kwenye mtaa wa jirani wa Kiziba.
Vikosi vinavyounga mkono serikali ya Congo vimekuwa vikiwashambulia waasi wa M23 katika eneo la Minembwe na maeneo ya jirani tangu mapema Machi baada ya Twirwaneho kuteka vijiji kadhaa.
Mbali na hilo, M23 iliteka mji muhimu wa makutano ambao utairuhusu kundi hilo kuimarisha udhibiti wa Wilaya ya Masisi na kusonga mbele kuelekea Wilaya ya Walikale huko magharibi mwa Jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC.
M23 ilianzisha mashambulizi ya kushtukiza yaliyovunja ngome za vikosi vya serikali karibu na mji mkuu wa wilaya ya Masisi na kuishia kuteka eneo la Nyabiondo na vijiji kadhaa jirani, kuanzia juzi Machi 9, 2025.
Pia, FARDC na wanamgambo wanaounga mkono serikali walikuwa wakishambulia vijiji karibu na mji wa Masisi tangu Machi 6, 2025 kwa lengo la kurejesha mji mkuu wa wilaya hiyo na kuwazuia M23 kusonga mbele upande wa magharibi mwa nchi hiyo.
Kutekwa kwa Nyabiondo na M23 kunazuia vikosi vya FARDC kutumia barabara kuelekea Masisi, hivyo kuwatenga kabisa wanajeshi wa FARDC ama wanamgambo washirika walioko barabarani kusini mwa mji wa Masisi.
Vyombo vya habari vya ndani viliripoti kuwa udhibiti wa M23 katika eneo la Nyabiondo utatoa mwanya kwa kundi hilo kusonga mbele kuelekea Kashebere, mji muhimu unaoelekea wilaya tajiri kwa madini ya Walikale, takriban maili 50 kutoka mji mkuu wa wilaya ya Walikale.
Wakati mapigano yakiendelea, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema iko tayari kujadiliana na serikali ya Rais Felix Tshisekedi wa DRC juu ya namna ya kukabiliana na makundi ya waasi nchini humo, kwa sharti la kunufaika na madini ya nchi hiyo.
Alipofanya mahojiano na The New York Times, Februari 22,2025, Rais Tshisekedi aliahidi hadharani kutoa fursa kwa Marekani na Umoja wa Ulaya kushiriki katika utajiri mkubwa wa madini wa nchi yake, akisema utawala wa Trump unaweza kufaidika na mkondo wa madini muhimu kutoka DRC.
Msemaji wa serikali ya DRC, Patrick Muyaya alisema kwamba maofisa wa DRC na Marekani wamekuwa na mazungumzo ya kila siku katika siku za hivi karibuni, kuhusu uwezekano wa makubaliano ya madini.
Kauli ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilikuja sambamba na ripoti ya vyombo vya habari kwamba Rais wa Marekani, Donald Trump atamteua Mshauri Mkuu wa Masuala ya Nje katika mataifa ya Mashariki ya Kati, Massad Boulos, kuwa Mjumbe Maalumu wa Marekani eneo la Maziwa Makuu.
Pia, Serikali ya DRC imeweka zawadi kwa maofisa waandamizi wa M23 huku Wizara ya Sheria ya DRC nayo ikitangaza zawadi ya Sh13 bilioni (Dola milioni 5) kwa atakayefanikisha kukamatwa kwa kiongozi wa Alliance Fleuve Congo (AFC), Corneille Nangaa, Kamanda wa M23 Sultani Makenga na rais wa M23, Bertrand Bisimwa.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.