Makundi ya marafiki Simba yako hivi

Berkane. Kila mtu na mtuwe na katika kundi kubwa la watu lazima kuwepo na vikundi vidogo vidogo ambavyo hata hivyo mara nyingi haviwezi kutenganisha kundi zima.

Hivyo ndivyo ilivyo katika kikosi cha Simba ambacho pamoja na uhusiano mzuri uliopo wa kitimu, wapo wachezaji ambao wanaonekana kuwa na urafiki wa kushibana kiasi cha kutembeleana mara kwa mara, kuonekana pamoja pindi wanaposafiri au kuwa katika mizunguko ya kawaida.

Zipo sababu ambazo zinaonekana kuchangia hilo ambazo zinaweza kuwa lugha ambayo wachezaji husika wanatumia kuwasiliana, kutoka nchi moja au jirani lakini nyingine ni ukaribu binafsi.

Katika siku tatu ambazo nimesafiri na Simba kuja hapa Morocco nimebaini baadhi ya wachezaji ambao wana urafiki na ukaribu mno na mara kwa mara ni rahisi kuwaona wakiwa pamoja.

Mshambuliaji Lionel Ateba amekuwa karibu sana na beki Che Fondoh Malone ambaye wanatoka nchi moja ya Cameroon na ni nadra sana kumkosa mmojawapo mahali alipo mwingine pindi wanapokuwa katika mizunguko au safarini.

Nahodha Mohamed Hussein na Shomari Kapombe ni pacha nyingine ya marafiki ambayo imeshibana vilivyo lakini pia Tshabalala ni rafiki wa karibu wa mshambuliaji Kibu Denis kama ilivyo kwa kiungo Mzamiru Yassin.

Ikumbukwe Tshabalala, Kapombe na Mzamiru wote ni manahodha wa Simba na mara kwa mara wamekuwa wakicheza na Kibu katika timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ambayo inaonekana kuimarisha uhusiano wao.

Rafiki mkubwa wa mshambuliaji Steven Mukwala ni nyota wa Zambia, Joshua Mutale na hilo linaonekana kuchagizwa na wawili hao kuzungumza lugha moja ya Kiingereza na kundi lingine la marafiki linaundwa na Valentine Nouma, Charles Ahoua, Karaboue Chamou na Elie Mpanzu.

Ahoua na Karaboue wanatokea nchi moja nayo ni Ivory Coast ambayo raia wake wana muingiliano wa karibu na raia wa Burkina Faso anakotokea beki Valentine Nouma.

Lugha ya Kifaransa inawaunganisha watatu hao na Mpanzu  ambaye yeye anatokea DR Congo.

Kuna wachezaji hao ni kama umoja wa nchi zisizofungamana na upande wowote (NAM), kwani wao wanaonekana kuwa marafiki wa wengi ambao ni Fabrice Ngoma, Hussein Abel, Yusuph Kagoma na Awesu Awesu na Moussa Camara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *