Makundi haya ya wajawazito hatarini kujifungua watoto wenye matatizo ya moyo

Arusha. Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Naiz Majani ametaja makundi manne ya wanawake wajawazito walio katika hatari ya kujifungua watoto wenye matatizo ya moyo.

Dk Majani amesema kuwa wajawazito wenye matatizo ya moyo au waliowahi kuzaa mtoto mwenye tatizo la moyo, au mwanafamilia yeyote aliyewahi kupata mtoto wa aina hiyo, wako katika hatari zaidi ya kujifungua mtoto mwenye shida hiyo kutokana na vinasaba.

Makundi mengine ni wajawazito wenye watoto pacha, lakini pia wanaougua au wanaotumia dawa kwa muda mrefu kama vile za kisukari, presha au kifafa.

Dk Majani amebainisha hayo leo Machi 7, 2025 wakati akizungumzia huduma wanayotoa katika banda la JKCI katika viwanja vya TBA ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Dunia,  inayotarajia kuhitimishwa kitaifa kesho jijini hapa.

Kutokana na hatari hiyo, Dk Majani amewashauri wajawazito kuhudhuria kliniki mapema na kuhakikisha wanafanya kipimo cha ‘Fetal Echocardiography’ ili kubaini tatizo na kujipanga namna ya kukabiliana nalo.

“Magonjwa mengi ya moyo ya kuzaliwa yanatibika lakini yana sharti kubwa la kujulikana mapema na yanahitaji tiba kwa wakati mwafaka.

Daktari Bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Naiz Majani akimfanyia kipimo mmoja wa wajawazito katika banda lao lililopo viwanja vya TBA Arusha ikiwa sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Wanawake Duniani inayoadhinishwa kitaifa mkoani Arusha Machi 8, 2025. Picha na Bertha Ismail

“Inaumiza sana unapogundua mtoto ana tatizo la moyo halafu unamwambia hatuwezi kufanya upasuaji kwa sababu tu amechelewa,” amesema.

Mbali na makundi hayo, Dk Majani amewataka wanawake kuchukua tahadhari ya kujifungua watoto wenye matatizo ya moyo ikiwemo kuzingatia lishe yenye virutubisho vyote muhimu kipindi chote cha ujauzito na kutumia vidonge aina ya ya ‘Folic Asidi’.

“Wajawazito wasitumie dawa zozote hovyo, pombe wala kuvuta sigara na hata kukaa karibu na mtu anayevuta sigara, kwani inaweza kuathiri ukuaji mzuri wa moyo wa mtoto aliye tumboni na viungo vingine kwa ujumla,” amesema.

Pia, amewapa mbinu kina mama kuzitambua dalili za awali zinazoashiria mtoto kuwa na matatizo ya moyo ikiwemo mtoto kushindwa kunyonya, kutoka jasho kwa wingi, kubadilika rangi na kuwa bluu kwenye midomo, mikono na miguu.

Akizungumzia kliniki hiyo, amesema wamewaona zaidi ya watu wazima 551 na kuwafanyia uchunguzi wa magonjwa ya moyo wakiwemo wajawazito 91 na watoto 70.

“Tangu tumefungua kampeni hii ya kuchunguza watoto wakiwa tumboni, tumeona wajawazito zaidi ya 91 na watano kati yao wamegundulika watoto wao wana matatizo ya moyo na wameshapangiwa hospitali ya kujifungua.

“Pia, tumechukua taarifa zao muhimu ikiwemo matarajio ya siku ya kujifungua kwa ajili ya uchunguzi na tumewapa mawasiliano ambayo watawasiliana na sisi ili kuanza matibabu haraka ya mtoto atakapozaliwa,” amesema Dk Majani.

Kwa upande wake, daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watu wazima kutoka JKCI, Dk Engerasia Kifai amesema katika kliniki hiyo waliyoanza Machi Mosi, 2025, wamefanikiwa kutoa elimu ya magonjwa ya moyo kwa watu wazima na namna ya kukabiliana nayo ikiwemo kuwa na mtindo mwema wa maisha.

Mmoja wa wajawazito waliopimwa katika kliniki hiyo, Jasmini Mwanga, mkazi wa Majengo jijini hapa, amesema huduma hiyo imekuwa nzuri na faraja kwao na ameomba Serikali kuweka kitengo cha huduma ya magonjwa ya moyo jijini Arusha.