Makumi ya wanajeshi wa Israel wauawa, kujeruhiwa; Hizbullah yapiga kambi ya jeshi huko Haifa

Mujahidina wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon wamefanya mashambulizi makali dhidi ya vituo vya kijeshi na maeneo ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika mji wa Haifa, na kuua wanajeshi kadhaa wa utawala huo.

Vyombo vya habari vya Kiebrania vimekiri kuwa wanajeshi 15 wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika operesheni ya Hizbullah iliyolenga Kikosi cha Golani (Golani Brigade) huko Binyamina, kusini mwa Haifa, baada ya kuripotiwa kuwa wanajeshi 110 wamejeruhiwa, wakiwemo waliokuwa mahututi.

Vyanzo vya Kiebrania vinaeleza kuwa, ndege isiyo na rubani ya Hizbullah imepiga shabaha kusini mwa Haifa bila ving’ora kulia, na idadi kubwa ya majeruhi imeripotiwa katika eneo la tukio. Vimesisitiza kuwa magari 50 ya kubeba wagonjwa yamepelekwa katika eneo la tukio.

Kwa upande wake, Muqawama wa Kiislamu umetangaza katika taarifa yake kwamba: Hizbullah imetekkeleza oparesheni ya ndege zisizo na rubani katika kambi ya mafunzo ya Brigedi ya Golani huko Binyamina, kusini mwa Haifa inayokaliwa kwa mabavu, ili kujibu mashambulizi ya Wazayuni hususan katika vitongoji vya Al-Nuwairi na Basta mjini Beirut.

Harakati ya Ahrar imepongeza operesheni ya kishujaa iliyotekelezwa na Hizbullah kwa kulenga chumba cha kulia chakula katika kambi ya kijeshi ya Brigedi ya Golani huko Haifa.