
Katika kujitafuta kila mtu ana njia yake na anakutana na misukosuko yake lakini akishajipata yote huyasahau na kubakia sehemu ya hadithi za historia akisimulia wengine na ndivyo ilivyo kwa bondia chipukizi kutoka mitaa ya Mabagala, Mussa Makuka.
Huenda siyo maarufu kabisa katika mchezo huo kwa kuwa anajitafuta kupitia mapambano mbalimbali lakini kama unataja mabondia wenye uwezo wa kuburudisha ulingoni basi jina lake utaliweka hata kama hupendi kutokana na uwezo na kipaji kikubwa alichokuwa nacho huku akisimamiwa na Gym ya B Combination chini ya Babu Ally.
Makuka ambaye leseni yake katika mchezo huo ukiwa inasoma ID#1024660 akiwa tayari na jumla ya mapambano saba mpaka sasa ambayo amefanikiwa kucheza katika mchezo wa ngumi za kulipwa.
Bondia huyo amefanikiwa kushinda mapambano manne pekee, amepigwa mara moja na ametoka sare mara mbili lakini hajawahi kupigwa wala kushinda pambano lolote kwa ‘Knockout’ tangu aanze kupigana katika ngumi za kulipwa mwaka 2021 kwa mujibu wa mtandao wa Boxrec, ambao umekuwa ukihifadhi taarifa za mabondia duniani kote.
Makuka anayepigana kwenye uzani wa bantam anakamata nafasi ya 12 katika mabondia 59 nchini wakati duniani akiwa bondia wa 289 katika mabondia 1144 huku akiwa na hadhi ya nyota moja.
Kwa upande mwingine bondia huyo amepewa asilimia 34 za ushindi wa Knockout pamoja na nafasi yake ya mtindo wa kupigana yaani orthodox unaotokana kutanguliza mguu wa kushoto na mkono wa kushoto wakati wa kupigana.
Mwananchi limefanya mahojiano maalumu na bondia huyo, mwenyeji wa mkoa wa Morogoro ambaye kwa sasa amejikita katika mchezo huo huku makazi yake yakiwa Mbagala jijini Dar es Salaam.
Makuka anasimulia sababu ya yeye kuwa bondia hakutokea kama bahati mbaya kutokana na kuanza mazoezi ya mchezo huo tangu akiwa anasoma elimu ya sekondari mkoani Morogoro katika shule ya Mladani.
“Nimeanza kuupenda na kufuatilia huu mchezo siku nyingi tangu wakati nasoma kwetu huko Morogoro, nilikuwa nafanya mazoezi na kusoma.
“Nilichokuwa nafanya ni kutenganisha muda wa masomo na mazoezi hadi pale nilipomaliza shule ndiyo nikaingia rasmi katika mchezo huu ambao kwangu ni burudani lakini pia ni ajira ambayo naamini inaweza kunisogeza katika maisha.
“Kuhusu ngumi nimeanza kucheza kwenye ngumi za ridhaa kwa sababu huko ndiyo kuna misingi sahihi ya mchezo wa ngumi, nimecheza ridhaa kwa miaka miwili kabla ya kuingia rasmi kwenye ngumi za kulipwa mwaka 2020, ingawa mapambano yangu yameanza kuingizwa mwaka 2021.
“Nashukuru ngumi za ridhaa nimejenga na nimeweza kupata hata medali katika mashindano ya majeshi ambayo nimekuwa nacheza hivyo kwangu naona siyo jambo dogo ingawa nimecheza kwa kipindi kifupi sana kabla ya kugeukia ngumi za kulipwa.
Kwa muda ambao umecheza ngumi za kulipwa jambo gani ambalo huwezi kulisahu?
“Naweza kukwambia kwamba ni mizengwe nadhani, mwaka huu Februari 28, nilipigana na bondia mkongwe na mwenye uzoefu wa kutosha, Haidari Mchanjo lakini nilichokutana nacho ndiyo siwezi kusahau katika maisha yangu.
Ulikutana na kitu gani?
“Unajua pambano langu lilikuwa la raundi sita na uzuri hata wewe (mwandishi) ulikuwepo, nimeongoza kwa pointi kuanzia raundi ya kwanza hadi ya mwisho.
“Kiukweli watu waliokuwepo siku ile hata ukipata nafasi ya kuangalia tena video kwenye mitandao, utaelewa ambacho nakisema kwa sababu mpinzani nilimzidi karibu kila raundi.
“Lakini ilivyofika raundi ya sita, nilianguka lakini kuanguka kwangu haikuwa ngumi ambayo imenipata maana nilikwepa ila wakati huo nilikuwa narudi nyuma, mwamuzi akanitegeshea mguu, nikaanguka chini.
“Baada ya kuanguka, mwamuzi alinihesabia kama ‘knockdown’ kitu ambacho hakikuwa sawa ndiyo maana nasema mizengwe kwa sababu baada pale katika matokeo ikaonekana nimepigwa, mipigwa mimi.
“Kiukweli kama bondia mchanga ambaye najitafuta kwangu nilichukulia lile jambo kama mizengwe ya kurudishana nyuma kwa makusudi maana najua nilicheza na bondia mkubwa lakini hakutakiwa kulindwa kwa staili ile na mwamuzi na badala yake alitakiwa ajilinde mwenyewe.
“Nadhani pengine waamuzi hawaoni namna tunavyoumia kwenye mazoezi lakini wanatakiwa kutambua sisi wote ni mabondia ambao tunataka kufikia malengo na siyo kuturudisha nyuma kwa kutukatisha tamaa makusudi.”
Ushirikina imekuwa ni sehemu ya watu wa michezo ukiwemo ngumi, vipi wewe umewahi kukutana na tukio gani?
“Unajua ushirikina kweli upo lakini kwanza unatakiwa uamini kwenye imani yako na Mungu kama yupo halafu na jinsi ambavyo ulivyojiandaa kuweza kupambana ili upate matokeo.
“Lakini hayo mambo ni kweli yanatokea kwa kiasi chake na wengi washakutana nayo maana hata mimi mwenyewe nilishakutana na jambo la hivyo wakati fulani katika pambano langu.
“Nilipigana na mtu lakini ajabu nilikuwa naishiwa nguvu kadiri muda ulivyokuwa ukizidi kwenda ila namshukuru Mungu nilifanikiwa kumaliza salama na pambano likaisha kwa sare japo kuwa kabla ya pambano nilikuwa sawa ila nilivyopanda ulingoni mambo yakabadilika.”
Una mipango gani kwenye ngumi?
“Mungu akinipa uzima na afya ya kuendelea kupigana basi malengo yangu makubwa ni kutaka kuwa bondia mkubwa, naamini kipaji kikubwa ninacho lakini bado nahitaji kuongeza juhudi na nidhamu ili niweze kushinda mikanda mikubwa zaidi,” anasema Makuka.