Makosa haya yanavyobomoa ndoa

Hakuna anayeingia katika ndoa akiwa na nia ya kuiharibu. Hata hivyo, ni rahisi kuharibu ndoa kuliko kuijenga.

Wengi hawajui kuwa ndoa inaweza kufungwa kwa gharama kubwa au mbwembwe za kila aina, lakini ikashindwa kudumu kutokana na makosa madogo yanayoweza kuepukika hasa yanapopuuzwa na wenza.

“Ikiwa unataka kuharibu ndoa yako, mpuuze  Mungu nyumbani kwako na mpe shetani. Muweke  Mungu kando na uthamini anasa, dhambi na udhalimu,” anasema mshauri wa ndoa Doreen Kerubo ambaye pia ni mwanasaikolojia.

Anasema watu wanaingia katika ndoa wakiwa na matumaini ya maisha yenye furaha,  lakini kwa sababu ya kupuuza maisha yao ya kiroho wanaisambaratisha.

“Raha inapaswa kuwa kwa  kiasi na katika kuwania hiyo raha, usimtenge Mungu wako,” anaeleza.

Miongoni mwa makosa yanayofanywa na wenza kwenye ndoa, ni kutumia muda wanaopaswa kuwa pamoja  kwa mambo mengine ya binafsi.

“Ukitaka kuharibu ndoa yako, kamwe usitumie muda na mume au mkeo. Wewe endelea kushinda ukiwa na marafiki zako katika chama, wafanyakazi wenzako na safari za kazi. Ukifanya hivi  hautakuwa na ndoa na utajilaumu mwenyewe,” anasema.

Mume au mke ni mtu maalumu katika maisha yako na haufai kumchukulia kama mtu kwa kawaida. Haifai kumchukulia kama watu wengine.

“Watu huwa wanaharibu ndoa zao kwa kuwachukulia waume na wake zao kama watu wa kawaida, wanakosa kuwajali na kuwaheshimu. Unakuta mtu anamwita mume au mke wake  kwa majina ya kumdhalilisha. Usipomthamini mume au mkeo kama mtu ‘special’ kwa maisha yako,  unaharibu ndoa yako,” anafafanua.

Mwanasaikolojia mwingine, James Kariuki anasema wenza huwa wanaharibu ndoa zao kwa kupeana presha.

‘’ Unakuta  mtu anapenda kulalamika bila kikomo kwa chochote ambacho mume au mke amefanya,’’ anaeleza.

Raha ya ndoa

“Ukitaka ndoa yako ikose raha na kuvunjika haraka, usimpe mtu wako nafasi ya kupumua. Mpe presha. Lalamika hata kwa mambo madogo,” anasema.

Japo kazi ni nzuri, wataalamu wanasema inaweza kuharibu ndoa hasa pale mwanandoa anapoitumia kujitenga na mwenzake.

“Mke, ukitaka kuharibu ndoa, fikiria zaidi biashara na kazi yako na umpuuze mume na watoto wako. Ukifanya hivi, ndoa haitadumu na hata mumeo akikuvumilia, atachepuka. Sawazisha muda wa kazi, familia na usikose kutenga muda wa kuwa na mumeo,” anasema Kariuki.

Kwa upande wake, Kerubo anaongeza kuwa hali hiyo ni kwa wanaume pia.

“Wanafaa kuhakikisha wanapata muda wa kuwa na wake zao hata pale wanapokuwa katika harakati za  kuhakikisha vyanzo vyao vya riziki haviyumbi,” anaeleza.

Kosa jingine linaloelezwa ni watu kuzungumzia wapenzi wao wa zamani mara kwa mara,  wakiashiria kwamba walikuwa bora kuliko waume au wake zao wa sasa.

Zisemavyo tafiti

Mtafiti maarufu wa masuala ya uhusiano nchini Marekani, John Gottman   katika utafiti wake mwa mwaka 2016, anaeleza  ili kuondoa tofauti wanandoa wanapaswa kujenga mhimili wa urafiki na kuimarisha uhusiano wao kwa kufanya mazungumzo ya kila siku, kuhusu mambo madogo na ya kawaida.

Anasema, hali hiyo itasaidia kupunguza msongo wa mawazo na kujenga upendo wa kudumu. Hakuishia hapo anasema wanandoa wawe na tabia ya kusameheana na kutoa msamaha kwa urahisi.

 Aidha, utafiti wa Chama cha Wanasaikolojia Marekani  wa mwaka  2018 ulionyesha kuwa wanandoa wanapokuwa na migogoro, ni muhimu kufahamu tofauti za kila mmoja na kukubaliana na kisha kutatua tatizo ili kuijenga ndoa.

Mawasiliano kati ya wanandoa,  ni njia bora inayoelezwa na watafiti inayoweza kurejesha amani kati yao na huwapa uwezo wa kuzungumza waziwazi,  kuhusu hisia zao na matatizo wanayokutana nayo.

Njia hiyo mwarobaini wa kutatua matatizo badala ya kushambuliana kwa maneno makali na kisha kuachana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *