Makosa haya ya ulalaji  yanagharimu afya yako

Dar es Salaam. Usingizi ni raha, ni starehe na haja ya kimsingi kwa binadamu yeyote. Usipolala inavyopaswa unaiweka afya yako hatarini.

Hata hivyo, unapokosa usingizi, jua una tatizo la kiafya na linaweza kuwa hatari kwa maisha yako. Lakini, hivi wengi tunajua taratibu bora za kulala?

Kwanza tujue tunapolala, ubongo hupata wakati wa kutunza kumbukumbu na kufanyia kazi taarifa tulizonazo ambazo ni matukio ya kutwa nzima au kipindi ambacho binadamu alikuwa ameamka.

Kuamka katikati ya usingizi kwa sababu zozote na kisha kulala tena, huingilia mchakato wa kemikali maalum inayofanya matengenezo ya ubongo wa binadamu na kuleta athari; hivi ndivyo wataalamu wa afya wanavyoonya.

Makosa hayo wataalamu wanasema  huchangia kwa kiasi kikubwa kuharibu afya ya ubongo na mfumo mzima wa mwili, ikiwa mtu hataruhusu mwili kupumzika ipasavyo.

Wanasema kwa mfano, ndani ya saa 24 mtu hutakiwa kulala mfululizo kwa saa sita mpaka nane, bila kuamka ili kuruhusu shughuli ya uchakataji wa ubongo.

Mitindo ya ulalaji

Miongoni kwa makosa tunayofanya katika kulala na hivyo kuweka afya zetu shakani ni pamoja na mitindo ya kulala, huku mtindo wa kulala chali ukitajwa kama mtindo unaotakiwa kuepukwa.

Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa upumuaji na magonjwa ya ndani, Elisha Osati anasema mtindo bora wa kulala ni ule ambao mtu unakua huru, huku akisisitiza watu kulala kwa kuegemea ubavu.

“Ukilala chali ni rahisi kupaliwa, sababu ulimi unalegea unaweza kuziba njia ya hewa lakini pia ni rahisi kupaliwa na mate yakaingia katika njia ya hewa.

Anasema kulalia tumbo ni kwa watoto wadogo… “Akilalia tumbo akikunja miguu inasaidia mtiririko mzuri wa damu kwenye moyo na mapafu, ndiyo maana watoto wengi wanakuwa huru na wanapenda kulalia tumbo pia inasaidia kuwazuia kupaliwa, ” anaeleza.

Kuhusu kulalia mto, anasema ni vizuri zaidi mtu akiepuka kulalia mto.

“Wapo waliozoea kulalia mto, ukiweza kutolalia mto ni sawa, shingo inakuwa imenyooka. Tunashauri zaidi walalie watu wenye shida ya moyo  au magonjwa mengine, kama ni mnene kiafya unaweza kulalia mto ili kusaidia misuli ya shingo isikaze sana,” anasema Dk Osati.

Anasema kwa mgonjwa mwenye shida ya moyo au ini, mto unasaidia mzunguko wa maji kubaki  kwenye mwili, hivyo anatakiwa atumie mto ili apumue vizuri.

Makosa mengine

Daktari bingwa wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Patience Njenje anasema kuna makosa kadhaa ambayo wengi huyafanya wakati wa kulala.

Anasema makosa hayo huchangia kwa kiasi kikubwa kuharibu afya ya mhusika bila yeye mwenyewe kujua.

Dk Njenje anasema kulala ni muhimu kwa binadamu, kitendo cha kulala ubongo huanza kujifanyia matengenezo, wakati huo binadamu huwa amelala usingizi hajitambui.

“Baada ya ubongo kufanya kazi kwa siku nzima huchoka na unaposikia usingizi ni kwamba unahitaji muda kujifanyia matengenezo na unapouruhusu kupumzika unaanza uchakataji.

“Kule ndani kuna kama kemikali zinatumika kuuendesha ubongo, baada ya kazi hiyo ile kemikali inatakiwa isafishwe baadaye inakuja mpya, inatumika kulala usingizi usipolala ile kemikali inakutafuna mwenyewe, inakuwa chafu,” anasema.

Dk Njenje anasema mtu anapolala kwa usahihi bila kuamka katikati ubongo wake huwa makini na safi kuendeleza michakato mingine katika mwili.

“Lazima ulale saa za kutosha, kama hulali utapata shida baadaye wengine wanakonda, wanapata msongo wa mawazo, wengine wanachanganyikiwa kwa sababu kemikali ambayo ni sumu inakuwa hujasafishika kwenye ubongo,” anasema Dk Njenje na kusisitiza kuwa kwa mtu mzima, wastani wa kulala kwa siku ni saa nane.

Dk Njenje anataja makosa mengine yanayofanywa kuwa ni pamoja na kutazama runinga kwa muda mrefu kabla ya kulala au kulala huku runinga ikiwa wazi.

“Ukiwasha TV au redio ina maana hutalala vizuri, lazima uzime taa ili ulale vizuri. Mwili unapokuwa katika hali au mazingira tulivu inakufanya ulale vizuri na ubongo ufanye matengenezo vizuri,” anasema.

Pia anasema matumizi ya simu kabla ya kulala hasa ukiwa umezima taa, pia ni makosa yanayochangia kutopata usingizi mzuri.

Akitaja sababu za kuamka katikati ya usiku au muda wa kupumzika, anasema wengine huamka sababu wanakwenda kupata haja ndogo.

“Hutaacha mpaka uchafue kitanda, ukipata haja ndogo mapema kabla hujalala ni jambo zuri ili kupata usingizi ulio mzuri na katikati ya usingizi hutaamka. Ule muda wa kwenda haja wengine wanaharibu usingizi, lakini wengine wakirudi wanalala kama kawaida,” anaeleza.

Akitaja vitu vingine vinavyoweza kuharibu usingizi ni makosa ya kutojiandaa kabla ya kulala, ikiwemo kuhakiki kila kitu kimefanyika, ikiwemo kufungwa kwa milango.

Pia anataja unywaji wa vinywaji vya kafeini na kahawa muda mfupi kabla ya kwenda kulala, kuwa ni tabia inayopaswa kuepukwa.

“Epuka kunywa kahawa au vinywaji baridi vyenye kafein, wengine mazingira yasiyofaa kulala yanamfanya akose usingizi mfano godoro lililochakaa au kitanda kinachokuumiza,” anasema.

Suala hilo linaungwa mkono na Daktari wa magonjwa ya ndani hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Innocent Tesha anayesema kahawa, pombe na vitu vingine hupunguza hamu ya kulala na vinazuia homoni iliyopo mwilini inayosaidia kuamsha usingizi.

“Sasa unapokunywa kawaha kwa mfano inapunguza usingizi kwa asilimia kubwa sana na inaanza kuupunguza ndani ya dakika 30 mpaka 60 na ikishakamilika inafanya kazi kwa saa nne mpaka sita hiyo ni kahawa tu bado pombe,” anasema.

Anasema ni muhimu kuachana na vitu hivyo, kwani ili kupandisha kinga za mwili mtu anatakiwa apate usingizi wa kutosha, akilala vizuri mwili huimarika kwa asilimia kadhaa kutokana na kujijenga upya.

“Usingizi unasaidia kwenye kuimarisha moyo kwani unapopumzika moyo unajijenga upya katika kufanya kazi, kwakuwa unafanya kazi saa 24 kwa maisha yako yote.  Usipolala mwili utaachia homoni ambayo inakwenda kufanya moyo ufanye kazi ya ziada wakati ulitakiwa kulala ili kuupumzisha.

“Pia usingizi unasaidia kujenga kumbukumbu na kuleta ari nzuri ambayo husaidia mtu awe na furaha tofauti, iwapo jana alilala na msongo wa mawazo. Akiamka msongo unakuwa umepungua mwili unakua vizuri,” anasema.

Dk Tesha anasema mtu asipolala ni rahisi kupata magonjwa ya moyo, uzito mkubwa, kuwa na hasira muda wote, uzalishaji hupungua na kumbukumbu pia hupungua.

Usingizi ni nini?

Kwa mujibu wa Dk Tesha, usingizi ni kitendo cha mwili kupumzika na kuanza kujijenga upya baada ya saa kadhaa za kufanya kazi.

Kuna hatua nne za usingizi, kwanza usingizi huanza mtu anapokuwa macho, kuwa na usingizi mwepesi mpaka mzito na hatua ya pili mapigo ya moyo yanapungua na upumuaji huanza kupungua.

Hatua ya tatu ni pale mapigo ya moyo, upumuaji na ufanyaji kazi wa ubongo unapopungua  ili mwili uweze kupumzika na hatua ya nne na  ya mwisho ni pale mwili unaingia katika hatua ya usingizi mzito ‘usingizi wa pono’ ambapo sasa katika hatua hii mwili huwa unaingia katika usingizi wa ndoto.

Mtu wa kawaida kuanzia miaka 25 mpaka 60, anatakiwa apate usingizi usiopungua wa saa saba mpaka name.

Watoto kuanzia mwaka sifuri mpaka miwili, wanatakiwa walale saa 11 mpaka 14 watoto kuanzia miaka mitatu mpaka minne wanatakiwa wapate usingizi kuanzia saa 10 mpaka 13.

Miaka sita  hadi 13 wanatakiwa kulala saa kwa saa tisa hadi 11 na miaka 14 hadi 17 saa nane hadi 10 na watu wenye miaka 68 na kuendelea wanatakiwa walale kwa muda wa saa saba mpaka nane kwa siku.