
Uzoefu unaonyesha watu wengi hawana utaratibu wa kufanya mazoezi au kuushughulisha mwili kwa kazi maalumu. Na wanaofanya hivyo pengine ni pale wanapotaka kupunguza uzito au baada ya kushauriwa na wataalamu wa afya.
Hii ni tofauti na maelekezo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) linalopendekeza kwa mfano watu wazima kufanya mazoezi ya wastani wa dakika 150 kwa wiki, au dakika 75 ya mazoezi ya nguvu kubwa au shughuli yoyote inayofanya mwili kushughulika.
Kwa mujibu wa WHO inakadiriwa kutoushughulisha mwili, kunachangia asilimia sita ya vifo vyote duniani, asilimia 17 ya magonjwa ya moyo na kisukari, asilimia 12 ya kuanguka kwa wazee na asilimia 10 ya saratani za matiti na utumbo mkubwa.
Shirika hilo linataja miongoni mwa faida za mazoezi ni kupunguza hatari ya kupata magonjwa ya moyo, kiharusi, kisukari, matatizo ya afya ya akili pamoja na saratani.
Pamoja na faida hizi chekwa, unajua kama aina za mazoezi unayofanya au utaratibu unaotumia kufanya mazoezi hayo, vinaweza kuwa janga kwako?
Makosa ya wafanya mazoezi
Baadhi ya makosa yanayofanywa na wafanya mazoezi wengi ni pamoja na kutopima afya kabla ya kuanza mazoezi, kufanya mazoezi bila kujua kiwango cha ufanyaji, kutojua mazoezi ya kufanya na wakati wa kuyafanya pamoja na kuvaa mavazi yasiyo ya mazoezi.
Mtaalamu wa Mazoezi na Afya kutoka Taasisi ya Ushughulishaji mwili Tanzania (PAAT), Dk Waziri Ndondi, anasema ni muhimu mfanyaji wa mazoezi atambue hali yake kiafya, kabla hajaanza kufanya mazoezi kwa kuwa kufanya bila kujua hali ya afya, kunaweza kuwa na athari ya ulemavu au kifo cha ghafla.
“Pengine labda una shida ya moyo, mapigo yako ya moyo yakalazimika kupiga haraka haraka, unaishiwa nguvu au kupata shambulio la moyo na matatizo mengine, ‘’ anasema na kuongeza:
‘’Kama una shida ya upumuaji maana mazoezi yanahitaji pumzi ya kiwango cha juu, kwahiyo kama mwili wako una shida ya upumuaji maana yake unapofanya mazoezi bila kujua hali yako, unalazimisha mapafu kwenye upumuaji na kama misuli yako haipo imara, baadaye unaweza kujikuta inauma sana kupita kiasi.’’
Anasema makosa mengine ni kufanya mazoezi bila mhusika kujua anafanya kwa kiwango gani, akieleza mtu anaweza kujikuta anafanya mazoezi chini ya kiwango na mwili kutotoa matokeo, au kufanya mazoezi kupita kiasi cha muongozo wa mazoezi.
“Muongozo wa ufanyaji mazoezi kuna kiwango cha kati na cha juu, sasa unajuaje kiwango cha juu? Ni pale unapofanya mazoezi unakuwa unaweza kuongea kwa shida..lakini kama unafanya mazoezi huwezi kuongea na mwenzako aliye karibu maana yake mazoezi yanafanywa kiwango cha juu kupita kiasi, sasa kufanya mazoezi kupita kiasi kinaweza kusababisha kifo cha ghafla au kupata ulemavu,”anaeleza.
Anaongeza kuwa, kosa lingine linalofanywa na wafanya mazoezi ni kutojua mazoezi gani wanatakiwa kufanya, akieleza kikawaida kuna mazoezi ambayo yanatakiwa kufanywa kwa wakati mmoja kama vile ya kiaerobia (Aerobic exercise), mazoezi ya misuli na ya kulegeza mwili.
“Muongozo wetu unasema ufanye mazoezi ya kiaerobia si chini ya dakika 150 kwa wiki, ufanye mazoezi ya kuimarisha misuli angalau mara tatu kwa wiki, ufanye mazoezi ya kulegeza mwili angalau mara tatu kwa wiki,”anasema Dk Ndondi.
Anasema baadhi ya wafanya mazoezi, hawaangalii mavazi ya mazoezi akitolea mfano mtu anaishi mji wenye joto, lakini anavaa jaketi hivyo kufanya atoke jasho sana kitu ambacho ni hatari kwa afya yake.
Anasema mtu huyu akitokwa na jasho jingi, hupoteza kiwango kikubwa cha maji, hivyo kusababisha kupata shida ya mwili kwa kupoteza maji, kuishiwa nguvu na kudondoka akiwa anafanya mazoezi.
“Sehemu ya joto watu wanashauriwa wavae fulana ya kawaida. Pia watu wanaofanya mazoezi barabarani jioni wanapaswa kuvaa nguo zinazoonekana na mtu mwingine…’’ anaeleza.
Anaongeza: ‘’Lazima mtu mwingine anayetumia hiyo barabara aone kuna mtu mwingine barabarani anakimbia lakini pia viatu vya kufanyia mazoezi lazima viwe laini, vyepesi mtu asifanye mazoezi na kiatu cha ngozi.’’
Faida za mazoezi, kuushughulisha mwili
Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza, Dk Jesca Lebba anawasisitiza watumishi wa umma na wananchi kuzingatia ufanyaji mazoezi, ili kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambikiza, kwakuwa yanaongezeka kwa kasi.
Anaeleza kuwa, magonjwa hayo yasiyo ya kuambukiza kama vile kisukari, saratani, changamoto mbalimbali za figo, magonjwa ya moyo; yote hayo yana gharama kubwa kwenye matibabu lakini yanazuilika kwa mazoezi na kubadilisha mtindo wa maisha.
Kwa mujibu wa mtaalamu wa mazoezi kutoka shirika la kimataifa linalojihusisha na mazoezi na afya la ‘International Association of Resistance Training’, Brian Johnston, mazoezi yanafanya moyo kuwa na nguvu na mapafu kuwa bora pamoja na kuwezesha mfumo wa mzunguko wa damu kutoa oksijeni zaidi mwilini.
Faida nyingine ni kubaki kijana kwa muda mrefu zaidi, kudhibiti unene, sukari na mafuta yaliyozidi mwilini na kuepusha shinikizo kubwa la damu, kisukari, magonjwa ya moyo na saratani.
Pia mazoezi hujenga misuli ambayo husaidia kutumia nishati ya ziada na hivyo kuepuka unene, kujenga mifupa imara na ukunjufu wa viungo, kupunguza msongo wa mawazo na uchovu, kuwezesha usingizi mnono, kuongeza kinga ya mwili na kuimarisha hisia na kuongeza ufanisi wa akili.
Faida nyingine ni kupunguza maumivi ya viungo na mgongo yanayowakumba wazee wengi, pamoja na kuondoa matatizo ya mifupa na viungo uzeeni.
“Faida za mazoezi huanza kupungua baada ya wiki chache mtu anapoacha kufanya mazoezi. Nguvu ya moyo, nguvu ya misuli, na kiwango cha lehemu hupungua, wakati shinikizo la damu na mafuta ya mwili huongezeka,”anasema mtaalamu huyo.
Muda wa kufanya mazoezi
Muda wa kufanya mazoezi au kushughulisha mwili unatofautiana kati ya watu wazima na watoto, ambapo watoto wenye mwaka mmoja hadi miwili wanatakiwa kushugulisha mwili sio zaidi ya dakika 60 kwa siku.
Watoto wenye miaka mitatu hadi minne wanatakiwa kufanya mazoezi angalau dakika 180 za mazoezi ya uzito wa kati au dakika 60 za mazoezi ya uzito wa juu.
Miaka mitano hadi 17 wanatakiwa kufanya mazoezi angalau dakika 60 kwa siku za mazoezi ya uzito wa juu, huku watu wazima wenye miaka 18 hadi 64 wakitakiwa kufanya mazoezi dakika 150 hadi 300 kwa wiki na hayo ni mazoezi ya uzito wa kati. Kwa mazoezi ya uzito wa juu, wanatakiwa kutumia dakika 75 hadi 150 kwa wiki.
Pia, watu wenye miaka zaidi ya 64 wanashauriwa kufanya mazoezi ya uzito wa kati kwa dakika 150 hadi 300, dakika 75 hadi 150 mazoezi ya uzito wa juu kwa wiki ili kuimarisha mapafu na misuli ya moyo.
Lakini pia wanashauriwa kufanya mazoezi siku mbili kwa wiki kuimarisha misuli na siku tatu kwa wiki ili kujenga mizania.