Makongoro Nyerere ashinda tuzo ya kiongozi mchekeshaji, ampiga chini Chalamila

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere ameshinda tuzo ya kiongozi mchekeshaji Tanzania ‘Best Funny Leader Of The Year’ katika tuzo za Tanzania Comedy Awards.

Makongoro ambaye ni mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ametwa tuzo hiyo usiku wa leo Jumamosi, Februari 22, 2025 katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki, jijini Dar es Salaam..

Katika tuzo hizo ambazo mgeni rasmi ni Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan. Makongoro  alikuwa akishindana na  Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Richard Hananja na Naibu Waziri na Mkuu wa Mkoa Mstaafu, Aggrey Mwanri.

Mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Makongoro amesema, “Hatimaye, hatimayeee, hatimayeeeee leo nimepata tuzo yangu mwenyewe,” amesema

Amesema amekuwa akipokea tuzo ndani na nje nchi za Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere lakini leo amepokea ya kwake mwenyewe.

Hata hivyo amewashukuru waandaaji kwa kutambua uwezo wake wa kuchekesha watu.