Arusha. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amewataka wakuu wa wilaya zote ndani ya mkoa huo kuandaa majukwaa ya kiuchumi katika maeneo yao, kama ilivyofanyika kwa jukwaa la uchumi la ngazi ya mkoa, kwa lengo la kuibua na kuendeleza fursa za kiuchumi zilizopo.
Wakati Makonda akisema hayo, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Maridhiano Tanzania, Askofu Dk Israel Maasa amewasihi viongozi nchini kuwa na hofu ya Mungu katika utendaji wao wa kazi na kutambua kuwa nafasi walizonazo ni kwa mapenzi ya Mungu.
Makonda na Dk Maasa walitoa kauli hizo jana Mei 21, 2025, wakati wa hafla ya kumuapisha Mkuu mpya wa Wilaya ya Karatu, Lameck Nganga, anayechukua nafasi ya Dadi Kolimba ambaye amehamishiwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tanga.
“Kama tulivyofanya jukwaa la uchumi la mkoa, lengo lilikuwa ni kuweka chachu katika ngazi hiyo. Sasa na ninyi fanyeni hivyo katika ngazi ya wilaya kwa kuangalia fursa zilizopo na namna wananchi wanaweza kunufaika nazo,” amesema Makonda.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa viongozi wa wilaya kuwa na mtazamo chanya kuhusu uchumi na kushirikiana na wadau wa maendeleo.
“Ukiwa mkuu wa wilaya na huwazii masuala ya fedha, ukikutana na mfanyabiashara utaanza kumhisi kama mwizi. Hatutaki viongozi wenye mawazo ya kimaskini.
“Kiongozi unapaswa kuandaa mazingira bora ya kiuchumi yatakayowafanya Katibu Tawala, Mkurugenzi wa Halmashauri, Mwenyekiti wa Halmashauri na wafanyabiashara kufurahia uongozi wako,” ameongeza.
Pia, Makonda amewakumbusha wakuu wa wilaya kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo waliyopewa.
“Sitarajii kusikia DC analalamika kila wakati. Umekula kiapo cha kulinda Katiba, fanya kazi. Unaruhusiwa kuniambia kama kuna mtu anakukwamisha katika kazi zako, nitakulinda.
“Lakini si kila changamoto ndogo tu ni simu kwa Mkuu wa Mkoa. Tatueni matatizo ya wananchi wenu, kaa kwenye kiti chako na fanya kazi,” amesisitiza.
Kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, Makonda amewataka viongozi wa Serikali katika mkoa huo kusimamia kwa uadilifu Katiba, sheria, kanuni na miongozo waliyopewa.
“Mwaka huu ni wa uchaguzi. Watu watachuana kwa sera. Sisi kama serikali, tuhakikishe tunasimamia Katiba, sheria na miongozo. Tusikubali amani ya mkoa wetu ipotee.
“Amani ni mtaji mkubwa unaosukuma uchumi wetu kusonga mbele. Tusikubali miezi mitatu au mitano ya kisiasa kutupotezea amani hiyo,” amesema Makonda.
Askofu Dk Israel Maasa amewasihi viongozi nchini kuwa na hofu ya Mungu katika utendaji wao wa kazi na kutambua kuwa nafasi walizonazo ni kwa mapenzi na mamlaka ya Mungu.
Dk Maasa amesema kuwa licha ya kuwepo kwa njia mbalimbali zinazotumika katika kuwateua viongozi, mwisho wa siku ni Mungu ndiye anayewachagua na kuwaweka katika nafasi hizo.
“Kama tunavyoona hapa, Mkuu wa Mkoa ameketi katika nafasi yake ni Mungu ndiye aliyemuita. Hata kama leo Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) yupo katika nafasi yake, ni Mungu ndiye aliyemuita,” amesema Dk Maasa.

Mkuu mpya wa Wilaya ya Karatu,Lameck Nganga,akiapa katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha,leo Jumatano Mei 21,2025.
Aliendelea kusisitiza kuwa kila mtu anapaswa kutambua kuwa nafasi aliyonayo ni wito kutoka kwa Mungu, na kwa kulitambua hilo, hofu yao ya kwanza inapaswa kuwa kwa Mungu katika kila jambo wanalolifanya.
“Mwisho wa siku, kila mmoja wetu ajitambue kuwa Mungu ndiye aliyemuita kufanya kile anachokifanya. Tukilielewa hilo, basi hofu yetu ya kwanza itakuwa kwa Mungu katika yale tunayoyatenda,” amesisitiza Dk Maasa.
Mkuu mpya wa Wilaya ya Karatu, Lameck Nganga aliyekuwa ameapishwa katika hafla hiyo, amesema atatekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na viongozi wenzake na kuhakikisha wilaya hiyo inanufaika kiuchumi kupitia sekta ya utalii.
“Nitasimama daima kutekeleza haki na wajibu wangu kwa kuzingatia sheria na kanuni. Nitakuwa mtiifu na nitashirikiana na viongozi wenzangu kuhakikisha sekta ya utalii, ambayo inaongoza kwa kuchangia uchumi wa Karatu, inaendelezwa ili kuongeza mapato zaidi,” amesema Nganga.