Makocha wafichua kinachombeba Fei Toto kutua Simba

UNAKUMBUKA namna ambavyo Clatous Chama wakati anaichezea Simba alivyokuwa akihusishwa na Yanga kila kinapofika kipindi cha usajili kabla ya msimu huu dili hilo kuwa kweli? Basi ishu hiyo imehamia kwa Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye ni msimu mmoja sasa unakatika tangu ameanza kuhusishwa na Wanamsimbazi.

Kiungo huyo ametajwa kuwa na mambo manne yanayombeba zaidi huku akiwa na uwezo wa kucheza kikosi cha kwanza cha timu yoyote ndani ya Ligi Kuu Bara kwa sasa.

Ipo hivi; Simba inatajwa kuiwinda saini ya kiungo huyo mwenye umri wa miaka 27 anayecheza Azam FC, huu ukiwa ni msimu wa pili akifunga jumla ya mabao 24 kwenye ligi. Msimu huu ukimalizika, mkataba wa Fei Toto ndani ya Azam utabaki mwaka mmoja.

Licha ya Simba kuwepo wa Jean Charles Ahoua (23), ambaye ndiye kinara wa upachikaji mabao katika kikosi hicho sambamba na ligi kwa jumla, akifunga 12, akifuatiwa na nyota wawili wa Yanga, Clement Mzize na Prince Dube, lakini Fei Toto bado anabebwa na namba sambamba na ubora wa kucheza eneo hilo.

Hivi karibuni, Mwanaspoti limeripoti Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, katika ripoti yake ya awali kabla ya kumalizika kwa msimu huu, amewataka mabosi wa klabu hiyo kumsajili Fei Toto kwa ajili ya kuongeza nguvu kikosini kwake aende kushirikiana na kiungo kutoka Ivory Coast, Ahoua.

Kutokana na hali hiyo, makocha mbalimbali wamewazungumzia wachezaji hao huku wakiweka wazi hakuna ambaye atamkataa Fei Toto kwenye kikosi chake kutokana na aina ya uchezaji wake sambamba na umri alionao huku wakiweka wazi uzoefu na ubora alionao anaingia moja kwa moja kikosi cha kwanza.

Makocha hao wamefichua, Fei Toto ukiwa naye kwenye timu ana uwezo wa kukaba, kushambulia, nguvu na maarifa makubwa ya kumiliki mpira mguuni.

Kocha wa zamani wa Dodoma Jiji, Biashara United na Kagera Sugar ambaye kwa sasa anaifundisha Polisi Kenya, Francis Baraza alisema Fei Toto ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa anayeweza kucheza kikosi cha kwanza, siyo Simba pekee bali timu yoyote ya Ligi Kuu Bara kwa sasa.

“Fei Toto ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa, ana umri ambao kocha anaweza kumtumia kwa namna yoyote anayotaka kwani ana nguvu na maarifa makubwa anapomiliki mpira mguuni kwake, hakuna kocha anayeweza kumkataa kikosini kwake, naamini kila mmoja anatamani kuwa na mchezaji wa aina yake.

“Kuhusu Ahoua pia ni mchezaji mzuri lakini anahitaji muda zaidi kuzoea soka la Tanzania ili aweze kushindana na Fei Toto ambaye tayari ameingia kwenye mfumo wa soka la Tanzania ukiondoa ubora alionao,” alisema kocha huyo raia wa Kenya.

Kocha wa zamani wa Mashujaa, Abdallah Mohammed ‘Bares’ alisema wachezaji wote wawili ni wazuri lakini Fei Toto kwake ndio chaguo la kwanza kwani anaweza kumpa vitu vingi uwanjani ikiwemo kukaba na kushambulia, pia anafunga na kutengeneza nafasi.

“Kama ataingia Simba ana nafasi kubwa ya kucheza kikosi cha kwanza, kuhusu nani anaanza nani anasubiri, itategemea kocha atatumia mfumo gani, wanaweza kucheza wote au mmoja akaanza na mwingine akasubiri ila kwangu chaguo la kwanza ni Fei Toto,” alisema Bares.

Kocha wa Wydad Casablanca, Rhulani Mokwena, alikiri waziwazi yeye ni shabiki mkubwa wa Fei Toto na anatamani sana siku moja kufanya naye kazi.

Kocha huyo wa zamani wa Mamelodi Sundowns, aliyasema hayo alipokutana na mchezaji huyo nchini Morocco wakati Azam FC ilipokuwa kwenye maandalizi ya msimu huu 2024-2025.

Fei Toto mbali na kutajwa kutakiwa na Simba, pia Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini inayofundishwa na kocha Nasreddine Nabi inamhitaji huku mchezaji mwenyewe akionyesha nia ya wazi kutaka kucheza soka nje ya Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *