Makocha kimataifa waipa ujanja Simba

Makocha kimataifa waipa ujanja Simba

Inaonekana. Ndivyo walivyosema kwa nyakati tofauti makocha wa zamani wa Yanga, Luc Eymael na Hans van der Pluijm, wakiamini Simba inaweza kupindua matokeo ya mabao 2-0 dhidi ya RS Berkane katika fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayopigwa nchini wikiendi hii.

Vijana wa Fadlu Davids wanahitaji ushindi wa mabao wa 3-0 ili kuandika historia mpya ya kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza, baada ya kupoteza 2-0 mechi ya kwanza yaliyowekwa wavuni ndani ya dakika 14 za kwanza za pambano hilo lililopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Manispaa ya Berkane.

Wakizungumza na Mwananchi jana kwa muda tofauti, makocha hao walisema kwa namna walivyotazama mechi ya kwanza, wanaamini Simba bado ina nafasi ya kubadili hatima yake kama itaonyesha nidhamu ya kiuchezaji, utulivu na ubunifu mkubwa katika eneo la mwisho la ushambuliaji.

Eymael, ambaye kwa sasa anaifundisha FC Saint Eloi Lupopo ya DR Congo, alisema ubora muda mwingine sio kigezo cha kuamua matokeo.

“Berkane walikuwa bora zaidi katika dakika za awali, lakini baada ya dakika 20 Simba ilirejea mchezoni. Kama wangeanza na utulivu ule tangu mwanzo, stori ingekuwa tofauti. Hili bado linawezekana,” alisema Eymael.

Kocha huyo alikumbusha mafanikio ya Simba kwenye robo fainali dhidi ya Al Masry ambapo iliibuka na ushindi wa mikwaju ya penalti ilikuwa ni baada ya kukomboa mabao 2-0 ambayo iliruhusu katika mechi ya kwanza jijini Cairo, Misri.

“Hiyo mechi iwe kumbukumbu kuwa Simba wakicheza kwa nidhamu na kasi, wanaweza kupindua matokeo. Kwa namna nilivyowaona, wana kikosi chenye wachezaji wa aina tofauti hivyo kila kitu kipo mikononi mwao japo haitakuwa rahisi, wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii,” alisema Eymael.

Kwa upande wa Hans Pluijm, kocha aliyeinoa Yanga kwa vipindi tofauti kisha kupita Azam an Singida Big Stars ambaye kwa sasa anaishi Ghana, alisema:

“Simba wana faida ya kucheza nyumbani, mbele ya mashabiki wao. Kama watamudu kupata bao la mapema moja tu basi sura ya mchezo itabadilika kabisa na presha yote itahamia kwa Berkane.”

Pluijm alisisitiza kuwa mechi hii si kwa wachezaji tu, bali pia ni wa benchi la ufundi kuja na mbinu tofauti na zile ilizotumia pambano la kwanza kwa mechi nyingine za msimu huu:

 “Davids anatakiwa kufanya maamuzi magumu kama kuanza na viungo wa kushambulia zaidi. Muda wa kusubiri umekwisha,” alisema Pluijm.

Pablo atoa lake

Kocha wa zamani wa Simba, Pablo Franco, ambaye kwa sasa anaifundisha Al-Qadsiah ya Saudi Arabia, alisema Simba inatakiwa kucheza kwa akili na si nguvu pekee.

“Berkane ni timu yenye uzoefu mkubwa kwenye michuano ya CAF. Watachelewesha muda, watatumia mbinu nyingi kuvuruga kasi. Simba inapaswa kuwa na subira, lakini bado iwe na kasi kwenye maamuzi ya mwisho,” alisema Pablo aliyesisitiza kocha Fadlu akija na mpango mkakati mpya wa kuibana Berkane na kutengeneza nafasi ya mabao ni wazi, Siomba itaishangaza Berkane na Afrika kwa ujumla.

Nyota wa zamani na kocha wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, alisema: “Huu ni wakati wa Simba kupambana kwa roho moja. Wachezaji wanapaswa kutambua kuwa historia haijengwi kwa maneno bali vitendo.”

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Kuhusu Fadlu

Kocha mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema kikosi chake kimejifunza kutokana na makosa ya mechi ya kwanza na kwamba wapo tayari kwa marudiano.

“Tumefanya tathmini ya yale tuliyokosea, hasa namna tulivyoanza mchezo taratibu. Safari hii tunaanza kwa kasi, tunamaliza kwa kasi. Tunahitaji bao la mapema kuhamasisha mashabiki wetu na kuwavuruga wapinzani.”

Davids alisema atawapa uhuru baadhi ya wachezaji wake kubadilika ndani ya uwanja kutegemea hali ya mchezo, jambo ambalo linaweza kuwa silaha ya kushangaza Berkane.

Mastaa wanena

Nahodha wa Simba, Mohammed Hussein, alisema: “Tuna deni kwa mashabiki wetu. Tunaamini tunaweza kupindua matokeo haya. Hii ni fursa ya kuweka majina yetu kwenye vitabu vya historia ya klabu.”

Beki mkongwe Shomary Kapombe aliongeza: “Tumewahi kucheza mechi ngumu zaidi ya hii. Tutaingia kwa utulivu na mpango mmoja kushinda na kutwaa kombe.”

Naye kiungo mchezeshaji Charles Jean Ahoua alisema: “Nimecheza mechi nyingi za ushindani Afrika Magharibi, lakini hakuna presha kama hii. Tuna dhamira ya kushinda, na tutapigana hadi mwisho.”

Kauli ya bosi

Mtendaji Mkuu wa Simba, Zubeda Sakuru, alisema maandalizi yanaendelea vizuri kama ilivyokuwa katika fainali ya kwanza ambapo wao kama viongozi walifanya kila ambalo lilitakiwa kufanyika ndivyo wanawajibika pia katika nusu ya pili ya fainali ambayo ipo mbele yao.

“Mashabiki waje kwa wingi kuisukuma timu. Tunahitaji uwanja uwe jiko.”

Namba zinawabeba

Rekodi zinaonyesha, Simba ikiwa nyumbani katika michezo sita iliyopita ya Kombe la Shirikisho kwa msimu huu ikiwamo ile ya raundi ya pili dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya, imeshinda mechi zote huku ikiruhusu mabao mawili tu ni katika 3-1 na Walibya, na ile ya 2-1 dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia.

Mechi nyingine ilizifunga Bravos do Maquis (1-0), CS Constantine (2-0), Al Masry (2-0) na Stellenbosch (1-0).

Katika mechi sita zilizopita kwa Berkane ikiwa ugenini katika Kombe la Shirikisho Afrika, imeshinda nne ikiwamo ile ya raundi ya pili dhidi ya Dadje ya Benin iliyoifumua 2-0, kisha kuinyoa Stellenbosch 3-1, Stade Malien Bamako na ASEC Mimosas kila moja kwa bao 1-0, imetoa suluhu moja dhidi ya Desportivo Lunda-Sul na kuchapwa dhidi ya CS Constantine kwa bao 1-0 katika nusu fainali.

Hii ikiwa na maana timu hiyo katika meci hizo za ugenini imeshinda nne, kutoka sare moja na kupoteza moja, lakini ikifunga jumla ya mabao saba ya kufungwa mawili tu, huku kipa wa timu hiyo Munir Mohammed akiongoza kwa kuwa na clean sheet nane katika mechi 13, akimzidi Moussa Camara wa Simba mwenye sita katika idadi ya mechi kama hizo za michuano hiyo ya CAF hadi sasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *