Makipa wamliza kocha TMA Stars

KOCHA msaidizi wa TMA Stars, Augustino Thomas ameweka wazi kuwa makosa ya kibinadamu ya kujirudia rudia ambayo yamekuwa yakifanywa na makipa wao yamechangia timu hiyo kutokuwa na mwenendo mzuri katika Ligi ya Championship.

Timu hiyo inashika nafasi ya tano kwenye msimamo kwa alama 31 baada ya kucheza mechi 17 huku ikiwa na lengo la kupanda daraja wakati huu ambapo imezidiwa alama 13 na Mtibwa Sugar inayoongoza kwa alama 44 lakini pia alama tano na Geita Gold FC inayoshika nafasi ya pili kwa alama 36.

Kwa mujibu wa kanuni za mashindano ya Ligi ya Championship, timu zinazoshika nafasi ya kwanza na pili zinapanda daraja moja kwa moja kucheza Ligi Kuu Bara huku zile zinazomaliza nafasi ya tatu na nne.

Zenyewe zinacheza mtoano (playoff), kutafuta mshindi ambaye anaenda tena kucheza playoff dhidi ya timu ya Ligi Kuu, ikishinda inapanda daraja huku timu ya Ligi Kuu ikishuka, lakini ikifungwa inabaki Championship.

Thomas alitoa kauli hiyo baada ya mechi ya TMA Stars dhidi ya Polisi Tanzania iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Kaluta uliopo jijini Arusha huku timu hizo zikitoka sare ya kufungana bao 1-1.

Uzembe uliofanywa na mlinda lango wake Yusuph Abdul dakika za mwishoni za mchezo kwa kutaka kudaka badala ya kupangua uende mbali mpira wa krosi iliyochongwa na mchezaji wa Polisi Tanzania, uliwagharimu na kuipa nafasi Polisi kusawazisha na mchezo kumalizika kwa sare.

Uzembe kama huo pia kipa huyo aliufanya kwenye mchezo dhidi ya Geita Gold FC ambayo ilimalizika kwa TMA Stars kushinda magoli 2-1.

“Kocha wa magolikipa anatakiwa ajithimini, haiwezekani hii ni mechi ya tano makosa ya makipa ni yale yale yanajirudia jambo ambalo halina afya katika kupambania kupanda daraja,” alisema Thomas.

Aliongeza, sehemu hiyo imekuwa na changamoto kubwa katika timu yake kutokana na makosa ya mara kwa mara hivyo watakaa na kocha wa makipa kumuuliza ni wapi anakwama ili waweze kumuongezea nguvu.

Aliweka wazi kuwa bado nafasi ya kupanda daraja ipo na ndio malengo yao hivyo wanarudi kwenye uwanja wa mazoezi kufanyia kazi sehemu zote zenye upungufu ikiwamo safu ya ushambuliaji.

Katika mechi 17 ambazo TMA Stars imecheza hadi sasa imeshinda tisa, sare nne sawa na ambazo imepoteza huku ikifunga magoli 27 na kufungwa 17.