Makipa Taifa Stars…Kuna tatizo kubwa

Hivi karibuni Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Wallace Karia alisema wanaandaa kanuni ambayo msimu ujao hakuna klabu ambayo itaruhusiwa kuwa na makipa wawili wa kigeni.

Hili ni jambo zuri ambalo linaonekana kuja kwenye wakati mzuri kutokana na baadhi ya timu kuwa na makipa wawili wa kigeni ambao wamekuwa kama wanazuia nafasi za wazawa.

Kila nchi huwa na kanuni zake, kabla ya kuwa na wachezaji wa kigeni Tanzania ilikuwa haina wachezaji hao, na hata walipoanza kuzichezea timu zetu walikuwa wachache kuliko idadi ambayo ipo kwenye ligi kwa wakati huu.

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Hivyo suala la kupunguza makipa wa kigeni linaweza kuwa na faida kubwa kwenye soka letu kama nchi kwa kuwa tayari tumeshakuwa na tatizo kubwa kwenye eneo hilo.

Hadi tunapozungumza leo timu ya Taifa, Taifa Stars haina kipa namba moja, wamekuwa wakipishana karibu kila baada ya mechi mbili kwa kuwa wote wamekuwa siyo makipa namba moja kwenye klabu zao.

Aishi Manula ambaye mara ya mwisho ndiye alikaa langoni kwenye kikosi cha Stars hana nafasi kwenye kikosi cha Simba na hajacheza mchezo hata mmoja, lakini inaonekana kuwa anapata nafasi kwenye timu hiyo kwa kuwa ana uzoefu tu wa kutosha wa kucheza soka nchini.

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Uhalisia ni kwamba hajacheza dakika hata moja kwenye mechi ya ushindani ndani ya kikosi cha Simba ambacho kipa wake namba moja ni Moussa Camara ambaye amekuwa kwenye ubora wa hali ya juu na sasa ndiye anatajwa kuwa bora zaidi kwenye ligi.

Lakini pia kabla yake alikuwepo Ayoub Lakred ambaye naye ubora wake ulikuwa haupigwi, pamoja na hayo makocha wa Stars wanalazimika kuwaita makipa kutoka Simba, akiwemo Manula na Ally Salim, wakiachana hawa wamekuwa wakiwaita makipa wa Yanga Abuutwalib Mshery na mara chache Khomein Abubakary.

Haina maana kuwa ndiyo makipa hao tu wapo kwenye ligi, wapo wengine tunawaona kila siku wakicheza kwenye klabu zao kama ambavyo amekuwa akifanya Yona Amosi kwenye kikosi cha Pamba na amekuwa akiitwa mara chache na kukaa kwenye benchi akiwaacha hawa ambao hawachezi wapate nafasi kwenye kikosi cha Stars.

Inawezekana wanapokwenda mbele ya makocha wa Stars, pamoja na kwamba kina Aishi Manula hawachezi kwenye timu zao, bado wanaonyesha uwezo wa juu kuliko kina Amosi ambao wanacheza kila siku.

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Lakini ninachofikiri suala siyo timu kusajili makipa wawili wa kigeni, bali ni kuweka kanuni bora ambazo wakati mwingine zitakuwa na faida kwa soka la nchi hii.

Tumeshaona tatizo kwenye eneo la makipa kuwa hatuna kipa wa timu ya Taifa aliyebora kwa kuwa hawapati nafasi ya kucheza mara kwa mara, nchi kama nchi lazima ije na mkakati thabiti wa kutazama jambo hilo kwa jicho lingine.

Ni ukweli uliowazi kuwa tunakwenda kwenye mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani bila kuwa na kipa anayepata nafasi kwenye klabu, hili siyo jambo jema.

Ni lazima TFF na Bodi ya Ligi, waje na kanuni ambayo inaweza kuwalinda wachezaji wanaocheza timu ya Taifa.

Je? kama Manula ndiye kipa wa timu ya Taifa na Simba kuna makipa wengine wanaomzidi kutoka nje ya nchi akienda Azam atacheza? akienda Tabora atacheza, akienda Singida atacheza? kama ni ndiyo TFF walishindwa kukaa na Simba na kuangalia jinsi ya kulinda kipaji cha kipa huyu, lakini pia kumuandaa kwa ajili ya kuisaidia Taifa Stars kwenye CHAN? sidhani kama walishindwa.

Lakini pia tunapofikiri kuhusu klabu kusajili makipa wawili wa kigeni, Mshery, Khomeny pamoja na Manula wala hawakosi nafasi kwa kuwa kwenye timu zao kuna makipa wawili wa kigeni, wanakosa nafasi kwa kuwa kuna kipa namba moja bora, kwa msaada wa nchi ikionekana kuna ulazima tujaribu kuweka kanuni ya kuhakikisha wale wazawa waliopo pale wanapata nafasi ya kucheza anagalau asilimia 40 ya mechi zote, kama hawatuwezi kuweka kanuni ya kutosajili makipa kutoka nje moja kwa moja.

Tukiweka kanuni hatutakuwa wa kwanza nchi nyingi zimeweka kanuni kwa masilahi ya taifa kwanza na mambo mengine baadaye. Lakini wakati tunafanya hivyo lazima tuhakikishe tunatengeneza mtaala bora wa kuzalisha makipa wengi bora kutoka kwenye mashindano shuleni, akademi na kuweka mkazo kwenye kusomesha makocha wengi wa makipa ili wachezaji hao wapate mafunzo bora.