Makedonia Kaskazini: Makumi ya watu wafariki katika mkasa moto uliozuka katika klabu ya usiku

Watu kadhaa wamefariki katika mkasa wa moto uliozuka katika klabu ya usiku huko Makedonia Kaskazini usiku wa Jumamosi Machi 15 kuamkia Jumapili Machi 16, shirika la habari la serikali la MIA limeripoti, likinukuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo ya Balkan.

Imechapishwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

“Takriban watu 50 wamefariki kufuatia mkasa wa moto uliozuka katika klabu ya usiku huko Kocani,” mashariki mwa nchi, karibu kilomita 100 mashariki mwa mji mkuu wa Skopje, ambapo “karibu watu 1,500 wamekuwa wakihudhuria tamasha,” shirika la habari la serikali la MIA limeripoti, likinukuu Wizara ya Mambo ya Ndani. Shirika la habari la AFP halikuweza kuthibitisha habari hii mara moja na mamlaka.

Kulingana na shirika hilo, moto huo uliteketeza klabu ya usiku ya “Pulse” katika mji huu wenye wakazi takriban 30,000, wakati wa tamasha la DNK, kundi maarufu sana la hip-hop nchini humo. Watazamaji katika tamasha hilo lililoanza usiku wa manane, wengi walikuwa vijana, kulingana na chanzo hicho.

Kulingana na tovuti ya habari ya SDK, moto huo ulizuka mwendo wa saa 9:00 usiku (11:00 Alfajiri saa za Afrika Mashariki). Moto huo huenda ulisababishwa na matumizi ya vifaa vya pyrotechnic, kulingana na baadhi ya ripoti za vyombo vya habari. Video zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii na kurekodiwa kabla ya moto huo zinaonyesha watu wakirusha vitu  aina ya fataki za ndani zinazotumiwa wakati wa tamasha.

Video nyingine zilizochapishwa na vyombo vya habari vya ndani zinaonyesha giza liki limetanda kwenye mlango wa jengo hilo kutokana na miali ya moto. SDK pia inadai kwamba “zaidi ya vijana mia moja walijeruhiwa,” likikinukuu Kurugenzi ya Ulinzi na Uokoaji na Kituo cha Kudhibiti Mgogoro. Waliojeruhiwa wamesafirishwa hadi hospitali za Kocani na Stip, takriban kilomita thelathini kusini mwa Kocani, na hadi Skopje, kulingana na tovuti.

Watu 27 waliojeruhiwa wamelazwa katika kliniki ya upasuaji ya Naum Ohridski huko Skopje, daktari katika kituo hicho, Nebojsa Nastov, ameiambia tovuti ya habari ya SDK. Waziri Mkuu Hristijan Mickoski, Waziri wa Mambo ya Ndani Pance Toskovski, pamoja na mkurugenzi wa Kituo cha Usimamizi wa Migogoro na mkurugenzi wa Ofisi ya Usalama wa Umma wako kwenye eneo la tukio na wanaweza kuzungumza asubuhi, kulingana na vyombo vya habari vya ndani. Mnamo Septemba 2021, katika mkasa wa moto mkubwa ulioathiri nchi hiyo, watu 14 walifariki katika kitengo cha wagonjwa wa Covid-19 huko Tetovo (kaskazini-magharibi).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *