Makatibu wa Kanda wailima barua Chadema, Mnyika atoa ufafanuzi

Dar es Salaam. Waliokuwa makatibu  wa kanda tano za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamekiandikia chama hicho barua kuomba malipo yao yanayotokana na utumishi wao kwa miaka 10.

Makatibu hao ni Gwamaka Mbugi, Emmanuel Masonga, Kangeta Ismail, General Kaduma na Jerry Kerenge, waliokuwa watumishi wa chama hicho katika Kanda za Nyasa, Kati, Magharibi, Kusini na Pwani.

Viongozi hao ni sehemu ya wale walioachwa katika uteuzi uliofanywa na Kamati Kuu ya Chadema iliyoketi Machi 11-12, 2025 chini ya Uenyekiti wa Tundu Lissu.

Hata hivyo, Ofisi ya Katibu Mkuu wa Chadema iliyoandikiwa barua hiyo, haikuweka wazi iwapo imepokea au laa, licha ya viongozi hao wastaafu kudai walishaiwasilisha tangu Machi 21, 2025.

Hata hivyo, viongozi wa chama hicho wapo Kanda ya Nyasa kwa ziara ya kuzindua ajenda ya ‘No Reforms, No Election’ (hakuna mabadiliko hakuna uchaguzi) leo Jumapili, Machi 23, 2025 wakianzia jijini Mbeya.

Kwa mujibu wa barua ya pamoja ya viongozi hao (nakala tunayo), maombi yao ni stahiki za utumishi wa chama hicho kama ulivyo utaratibu wa chama hicho.

Wamesema wamekitumikia chama hicho katika kipindi cha mwaka 2015/20 na 2020/25 na baadaye uongozi wa Chadema umeonyesha nia ya kutoendelea nao.

Stahiki walizoziainisha katika barua hiyo ni gharama za usafiri wa kurudi nyumbani kutoka maeneo ya kazi na kuiinua mgongo.

“Tunatumai barua yetu itafanyiwa kazi kwa haraka ili kutupa na sisi wakati mzuri wa kuendelea na majukumu mengine ya ujenzi wa chama na Taifa kwa ujumla,”imeeleza sehemu ya barua hiyo .

Kutokana na barua hiyo, Mwananchi ilimtafuta Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika aliyesema ni vema kwanza aulizwe aliyeandika barua hiyo kama ameiwasilisha au laa.

Alipoulizwa zaidi iwapo ameipokea au laa, amesema viongozi wa chama hicho wapo Kanda ya Nyasa kwa sasa kuzindua ajenda ya ‘No Reforms, No Election’.

“Vyombo vya habari msiyumbishwe na haya mambo, sisi viongozi tupo Nyasa huku kuzindua ajenda yetu, hakuna kingine tunachojua kwa sasa,” amesema.

Amesisitiza, “ni muhimu kwa gazeti kama la Mwananchi mkahakikisha mnajikita kwenye hiki tunachokifanya kama chama kikuu cha upinzani, hakikisha hamyumbishwi.”

Mwananchi limezungumza na baadhi ya watendaji hao wa zamani wa Chadema ambao wamesema barua hiyo imekwishafika ofisi ya katibu mkuu na wanasubiri majibu yao.

“Hatujajua kwanza hiyo barua imevujaje huko mitandaoni, tuliandika na kuiwasilisha kwa katibu mkuu. Tunaomba stahiki zetu ambazo ni utaratibu wa kawaida kabisa,” amesema na kuomba hifadhi ya jina lake.

Mwingine alipoulizwa madai hayo yanaweza kuwa kiasi gani? Amejibu, “kama unakuwa umefanya kazi zaidi ya miaka kumi si chini ya Sh100 milioni. Kwa hiyo kwa sasa tunasubiri majibu.”

“Na hii isitafsiriwe kwamba sijui tunahujumu kampeni yetu ya ‘No Reforms, No election’ la hasha, tunadai stahiki zetu kama watumishi na kama mtu yoyote anayeweza kudai. Ndio maana tumemwandikia barua katibu mkuu ili tupewe,” amesema naye pia akiomba hifadhi ya jina lake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *