Makamu wa Rais Sudan Kusini akamatwa

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini, Riek Machar amekamatwa na watu wenye silaha katika makazi yake yaliyopo Juba nchini humo.

Taarifa za kukamatwa kwa Machar zimeanza kusambaa leo Machi 27, 2025 ambapo tovuti ya France 24 imeeleza kukamatwa kwake kunahusishwa na mgogoro wa muda baina yake na Rais Salva Kiir.

Tovuti ya France 24 imeripoti kuwa: “Msafara wa magari 20 yaliyokuwa na silaha uliingia katika makazi ya Machar katika mji mkuu  wa Juba na kumtia mbaroni.

Mgogoro wa hivi karibuni ulioripotiwa kwa wiki kadhaa katika nchi hiyo, umesababisha kuzorota hali ya usalama katika taifa hilo.

Tovuti hiyo imesema kuwa Machar ambaye kwa muda mrefu amekuwa mpinzani wa Rais Salva Kiir, alikamatwa Jumatano.

“Mkataba wa kugawana madaraka kati ya Kiir na Machar umekuwa ukivurugika mara kwa mara na kutishia kurejea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe. Machafuko nchini humo yaliwahi kutokea na kudumu kwa miaka mitano huku takriban watu 400,000 wakihofiwa kupoteza maisha kati ya mwaka 2013 na 2018,” imeripoti tovuti hiyo.

Miongoni mwa mambo yanayowagombanisha Kiir na Machari ni tofauti za kisiasa.

Awali, Salva Kiir alikuwa mmoja wa viongozi wa SPLM (Sudan People’s Liberation Movement) iliyoiletea Sudan Kusini uhuru, Riek Machar na alikuwa na nafasi ndani ya SPLM, hivyo alijikuta akiingia kwenye mgogoro na Kiir. Hatimaye alianzisha kundi la upinzani linalojulikana kama SPLM-IO (Sudan People’s Liberation Movement-in-Opposition).

Muda mfupi baada ya Machar kukamatwa, chama chake kilitoa taarifa ya kulaani tukio hilo.

“Tunalaani vikali vitendo vya ukiukwaji wa katiba vilivyofanywa leo na Waziri wa Ulinzi na Mkuu wa Usalama wa Taifa, ambaye, pamoja na magari zaidi ya 20 yenye silaha, yaliingia kwa nguvu kwenye makazi ya Makamu wa Kwanza wa Rais,” imeeleza taarifa hiyo iliyotolewa na Reath Muoch Tang, Mwenyekiti wa Kamati ya Mahusiano ya Nje ya chama chake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *