Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amehimiza kutolewa kwa elimu ya biashara ya hewa ukaa (kaboni) ili wadau muhimu kwenye biashara hiyo wawe na uelewa utakaochochea ukuaji wa uchumi.
Kutokana na umuhimu huo, Dk Mpango ameelekeza Ofisi ya Rais (Tamisemi), Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), serikali za mikoa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Tanzania na Zanzibar, zikutane.
Dk Mpango amebainisha hayo leo Machi 6, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wake na wakuu wa mashirika na taasisi za umma uliohusu mabadiliko ya tabianchi na biashara ya kaboni.
Biashara hiyo mpya nchini imeonyesha fursa kubwa ya kuongeza pato la Taifa, hata hivyo inakabiliwa na changamoto lukuki ikiwemo kutofahamika vema miongoni mwa wadau kama vile halmashauri.
Makamu wa Rais, Dk Mpango amesema kwa kuwa biashara hiyo inahusisha wadau wengi, ni muhimu kuwa na uratibu mzuri utakaowezesha manufaa yake kuonekana nchini.
“Ofisi ya Rais Tamisemi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, kwa pande zote mbili za muungano na serikali za mikoa, zikutane kupitia uzoefu zilizoupata hadi sasa na katika hili, kupata uelekeo wa pamoja katika biashara hii na kurekebisha kasoro zilizopo hivi sasa,” amesema.
Amesema kuna uelewa mdogo wa biashara ya kaboni kuhusu faida na hasara zake, taratibu za namna inavyofanyika hazijawekwa wazi kwa wadau wakuu kama wanakijiji na halmashauri.

“Kwa mfano, mchakato wa kuwapata wawekezaji, namna ya kujua kiwango cha kaboni ni mambo ambayo hayafahamiki. Ni muhimu kutoa elimu kwa wadau kwa maana ya vijiji na halmashauri ili waelewe biashara hii,” amesema.
Kiongozi huyo amekitaka Kituo cha Uratibu wa Kaboni (NCMC) kuratibu elimu ya kaboni ili iwafikie wadau wote muhimu katika biashara hiyo.
Dk Mpango ameangazia uwazi wa mikataba kama jambo linalopaswa kuangaziwa kwenye biashara ya kaboni kwa kuwa imetawaliwa na madalali na hakuna uwazi. Amesisitiza kwamba ni muhimu kuzingatia vigezo vinavyotumika badala ya kuziachia halmashauri pekee.
“Uzoefu kutoka nchi nyingine ni muhimu, wadau waelimishwe namna nchi nyingine zinavyoendesha biashara hii na kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo,” amesema.
Makamu wa Rais ameeleza kwamba mikakati ya Serikali ni kuhakikisha kila Mtanzania anatumia nishati safi na malengo yao ni kwamba asilimia 80 ya Watanzania watumie nishati safi ifikapo mwaka 2034.
Katika kufanikisha hilo, amesema taasisi 672 zinazolisha watu zaidi ya 100 kwa siku, zimehamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia. Ametoa wito kwa taasisi nyingine ambazo bado hazijaanza kutumia nishati safi, zifanye hivyo haraka iwezekanavyo.
Awali akizungumza kwenye mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni amesema katika kuimarisha mfumo wa kitaasisi na kisheria wa usimamizi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi, wamefanya marekebisho madogo ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191.
Ambapo pamoja na masuala mengine imeanzisha kisheria NCMC na kuainisha majukumu yake.
Amesema marekebisho hayo yamefanyika kutokana na changamoto zilizobainika katika utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira.
“Ni wakati mwafaka kwa taasisi zetu kufanya kazi kwa karibu na kituo chetu cha uratibu wa kaboni,” amesema.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Zanzibar, Harusi Said Suleiman amesema Zanzibar, kama kisiwa, imeendelea kuathirika na mabadiliko ya tabianchi kama maeneo mengine. Amesema kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wanaendelea kujifunza kuhusu biashara ya kaboni.
“Hivi karibuni, Zanzibar tumepitisha kanuni za biashara ya kaboni. Mkutano huu ni fursa muhimu kwetu kujifunza kwani biashara hii imeanza kutekelezwa,” amesema.
Mwakilishi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mohamed Nyasama amesema mashirika ya umma yanapaswa kushiriki katika biashara ya kaboni ili kuongeza pato la Taifa.
“Ofisi ya Msajili wa Hazina tuko tayari kufanya kazi na ofisi yako (Ofisi ya Makamu wa Rais) kupitia mashirika ya umma ambayo ni injini ya kukuza uchumi,” amesema.