Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran: Visiwa vitatu vya Bu Musa na Tunb Kubwa na Ndogo ni mali ya Iran

Makamu wa kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuhusu madai ya Imarati ya kumiliki visiwa vitatu vya Bu Musa na Tunb Kubwa na Ndogo kwamba, kila mtu anajua kwamba visiwa hivi ni vya Iran na Jamhuri ya Kiislamu katu haitalegeza kamba kwa vyovyote vile kuhusiana na visiwa hivyo.

Muhammad Reza Aref amesisitiza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haitalegeza kamba kuhusiana na visiwa hivi vitatu ambavyo ni mali yake.

Hivi karibuni, Umoja wa Ulaya na Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi zilikariri madai yasiyo na msingi na yasiyoungwa mkono ya siku za nyuma kuhusu visiwa vitatu vya Iran katika taarifa ya mwisho ya pamoja.

Visiwa vya Ghuba ya Uajemi vya Bu Musa, Tunb Kubwa na Ndogo kihistoria vimekuwa sehemu ya Iran, na uthibitisho wake unaweza kupatikana na kuthibitishwa na hati nyingi za kihistoria, kisheria, na kijiografia nchini Iran na sehemu zingine za ulimwengu. Hata hivyo, Muungano wa Falme za Kiarabu, Imarati umekuwa ukirudia kila mara madai ya kumiliki visiwa hivyo.

Visiwa hivyo vilikuwa chini ya udhibiti wa Uingereza mwaka 1921 lakini mnamo Novemba 30, 1971, siku moja baada ya majeshi ya Uingereza kuondoka katika eneo hilo na siku mbili tu kabla ya UAE kuwa shirikisho rasmi, mamlaka ya visiwa hivyo yalirejeshwa kwa Iran.