
Dar es Salaam. Kumbusho Kagine na Martin Masese wamefungua kesi jinai dhidi ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Itikadi Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla kuhusu kukishutumu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuwa kimepanga kununua na kusambaza nchini virusi vya Ebola na Mpox.
Machi 22, mwaka huu, katika moja ya mikutano yake mkoani Simiyu, Makalla alidai kuwa Chadema inachangisha pesa kununua virusi vya ugonjwa wa Ebola na Mpox na kuvisambaza nchini.
Kagine na Masese wamefungua shauri hilo la maombi ya ruhusu ya kumfungulia Makalla kesi ya jinai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu jijini hapa.
Shauri hilo la maombi ya jinai mchanganyiko la mwaka 2025, lililopangwa kusikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Romuli Mbuya limetajwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza jana, Jumatano, Aprili 16, 2025.
Hakimu Mbuya ameelekeza mjibu maombi, Makalla apelekewe nyaraka za kesi ndani ya siku tano kuanzia jana na ametakiwa kuwasilisha mahakamani kiapo kinzani (majibu yake) ndani ya siku 14 baada ya kupokea nyaraka hizo.
Pia Makalla ametakiwa kuwapatia waombaji nakala ya kiapo kinzani ndani ya siku tatu, baada ya kuwasilisha mahakamani na waombaji watatakiwa kuwasilisha mahakamani majibu ya kiapo kinzani cha Makalla ( kama wataona kuna haja), ndani ya siku saba baada ya kupokea kiapo kinzani.
Ikiwa waombaji hao watakuwa na majibu dhidi ya kiapo kinzani cha Makalla, basi nao wameelekezwa kumpatia Makalla ndani ya siku tatu baada ya kuyawasilisha mahakamani.
Hakimu Mbuya amepanga kuwa shauri hilo litatajwa tena mahakamani hapo Mei 15, 2025, saa 3:30 asubuhi kuangalia kama taratibu hizo za ubadilishanaji nyaraka zitakuwa zimekamilika, kwa ajili ya kuendelea na hatua inayofuata.
Hata hivyo ameelekeza kuwa shauri hilo litatajwa kwa njia ya mawasiliano ya video (video conference) na amezitaka pande zote kuzingatia muda wa kujiunga na mfumo huo kupitia kiunganishi (link) watakayopewa. Hivyo ameahirisha shauri hilo mpaka tarehe hiyo.
Kagine na Masese wanawakilishwa na Wakili Hekima Mwasipu, wamefungua maombi hayo wakiomba waruhusiwe wao wenyewe kumfungulia Makalla kesi ya jinai, badala ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP)
Wamefungua maombi chini ya vifungu vya 99(1), (3); 128(2) na 392A (1) na (2) vya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), Sura ya 20, Kama ilivyorekebishwa mwaka 2022, inavyoruhusu mwendesha mashitaka huria.
Sambamba na hati hiyo ya maombi ya ridhaa ya kufungua mashitaka hayo ya jinai, pia wameambatanisha hati ya mashitaka hayo ya jinai wanayokusudia kumfungulia Makalla.
Makalla an adaiwa kutoa tuhuma hizo dhidi ya Chadema, Machi 22, 2025, wakati akihutubia katika moja ya mikutano yake mkoani Simiyu.
Katika mkutano huo, anadaiwa kuwa alisema Chadema inachangisha pesa kununua virusi vya ugonjwa wa Ebola na Mpox.
Waombaji hao wamenukuu maneno hayo ya tuhuma anayodaiwa kuyatoa Makalla, katika hati ya maombi, kiapo kinachounga mkono maombi pamoja na kwenye hati ya mashitaka.
Kwa mujibu wa nyaraka hizo, siku hiyo Makalla alikaririwa akisema kuwa:
“Chadema wanakusanya fedha Kwa kisingizio cha kwenda kuhadaa umma ili wakatae uchaguzi, ili wasimamishe uchaguzi. Lakini kuna ajenda ya siri…,
Wamedai alinukuliwa akisema kuwa, “Hawa watu, na hasa viongozi waandamizi ambao familia zao hazipo Tanzania wanataka kutumia michango inayochangishwa ya Tone Tone, eti ilifika wakati wakanunue virusi vya Ebola na Mpox, ili wavilete visambae Tanzania na uchaguzi usifanyike.”
Waombaji wanadai kuwa mkutano huo ulihudhuriwa na watu wengi na uliripotiwa na vyombo vya habari vya kawaida na vya mitandaoni ambavyo viliufikia umma na kwamba maneno hayo pia, yalipandishwa katika majukwaa ya mitandao ya kijamii ukiwemo Youtube.
Wanadai kuwa viongozi wa Chadema walianzisha na kuzindua kampeni ya Tone Tone kwa lengo la kukusanya pesa kutoka kwa umma kusaidia kuendesha shughuli za chama na si kwa ajili ya kununua na kuingiza virusi vya Mpox nchini Tanzania kutoka nchi nyingine.
Wanafafanua kuwa Ebola na Mpox si maradhi yanayouzwa kwa kuwa hayawezi kumilikiwa na mtu binafsi na kuuzwa kama bidhaa sokoni, bali ni maradhi ya mlipko ambayo yanaweza kuambukiza na kusababisha vifo vya watu wengi yanapoibuka.
Waombaji hao wanafafanua zaidi kuwa Ebola na Mpox ni virusi vya maradhi ambavyo haviwezi kuonekana wala kubebeka katika vyombo vyovyote kwa ajili ya biashara.
Wanadai kuwa taarifa na maneno yaliyotamkwa na Makalla siku hiyo ni ya uwongo, ya hatari na ya udanganyifu, hivyo wanaomba maombi yao yakubaliwe ili kuwezesha kumshtaki Makalla.
Katika hati ya mashitaka wanayokusudia kumfungulia Makalla kuna mashtaka sita, matatu kati yake yakiwa ni ya kuchapisha taarifa za uongo kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015.
Mashitaka mawili ni kutoa taarifa za uongo zenye lengo la kudhuru hadhi, haki na uhuru wa watu wengine na za udanganyifu za kutunga, kinyume na kifungu cha 50(1) a(ii) na 50(1) B vya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016.
Shitaka lingine ni la kitisho kinyume na kifungu cha 89B (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.