Lindi. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetaja mambo manne kuelekea uchaguzi Mkuu Oktoba, 2025 huku kikisisitiza kuwa hakitafanya makosa katika kuteua wagombea kwenye ngazi ya ubunge na udiwani.
Aidha, kimesema uchaguzi utakuwa huru na haki kwa sababu tayari kuna Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Hayo yamebainishwa leo Alhamisi, Aprili 10, 2025 na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla wakati wa mkutano wake wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Mkapa Garden wilayani Kilwa mkoani Lindi.

“Kama ambavyo tumepata mafanikio katika utekelezaji wa ilani, CCM itawaletea ilani nzuri itakayokonga nyoyo za Tanzania, pili tunawaahidi kama ambavyo tuliwaletea wagombea katika serikali za mitaa, CCM itawaletea wagombea wazuri wanao kubalika katika nafasi za udiwani na ubunge.
“CCM haitafanya makosa, ahadi ya tatu tutafanya kampeni za kistaarabu haitafanya kampeni za matusi wala kejeli, tutafanya kampeni za kistaarabu,” amesema Makalla na kuongeza kuwa:
“Ahadi ya nne kwa maboresho yaliyofanywa na Tume huru ya uchaguzi (INEC) uchaguzi utakuwa huru na haki na ahadi ya mwisho tutahakikisha amani inakuwepo hata baada ya uchaguzi kumaliziaka, hatuna nchi nyingine.”
Makalla amesema tayari Serikali imeshafanya marekebisho ya sheria mbili ambayo ni ya Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi na Ile ya kupita bila kupingwa.
CCM kiko imara, Chadema hawana pumzi
Katika hatua nyingine, mwenezi huyo amesema CCM kiko imara na tayari kushiriki na kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa kishindo, huku akiwabeza wale wanaofanya kampeni ya No Reforms, No Election wameishiwa pumzi na hawako tayari kwa uchaguzi.
“Watanzania hawapendi fujo, wanapenda amani. Wapo watu wanakuja na kusema ‘tutakinukisha’, mtu ana uraia wa nchi mbili, watoto wake wako Marekani, halafu anakuja kusema Watanzania wajitoe kufa ni sawa na mfanyakazi hewa,” amesema Makalla.
Amesema CCM inatambua dhamana waliyonayo hivyo itahakikisha nchi inaendelea kuwa na amani, utulivu na maendeleo.
“Hatutaki watu wanaotuingiza kwenye machafuko. Hatuna Kilwa nyingine, hatuna Lindi nyingine. CCM oyeee!,” amesema Makalla.
Akiizungumzia CHADEMA, Makalla amesema lengo la chama cha siasa ni kushika dola, na ili kishike dola lazima kishinde uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.
“Lakini wenzetu wameomba wapumzike mwaka huu, wana mgogoro ndani ya chama chao, wameishiwa pumzi. Wanaigiza tu, hawako tayari,” amesema Makalla.
Kauli ya Makalla inakuja katika kipindi ambacho Chadema inaendeleza vuguvugu la kufanyika kwa mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi kupitia kampeni yao ya No reforms, No election.
Kilwa wamtwisha zigo la fidia, barabara
Awali, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilwa, Said Timami akizungumzia utekelezaji wa ilani ya chama hicho wilayani humo, amesema imetekelezwa kwa asilimia 100 isipokuwa kuna changamoto mbili kama zitafanyiwa kazi, huenda zikafuta upinzani wilayani humo.
“Moja ya kero kubwa hapa ni mbili tu ambazo zitawezesha kufuta upinzani, kwanza ni malipo ya fidia kwa wananchi 446 waliopisha upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kilwa.
“Pili ni changamoto ya barabara ya Kibiti- Lindi yenye urefu wa kilometa 30 ambayo imekuwa kero kubwa kwa wananchi na zikifanyiwa kazi tutakuwa tumemaliza kabisa upinzani,” amesema Timami.
Akijibu hoja hizo, Makalla alimpigia simu Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba ambaye alikiri kutambua hoja ya madai ya fidia.
“Hii ni changamoto ya maendeleo tunayataka maendeleo lakini wapo watu waliotoa maeneo hayo kwa ajili ya maendeleo, nimeambiwa ni Sh6 bilioni ngoja hapa nimtafute Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba ili aniambie hii fedha wanalipa lini,” amesema.
Akijibu kuhusu madai hayo, Dk Mwigulu amesema; “Asante sana…asante sana Katibu Mwenezi ni kweli hili jambo nalitambua, nitakachokifanya baada ya maelekezo yako haya ni wananchi hawa wema na wapenda maendeleo wapewe stahiki zao, nitawasiliana na wenzangu wa wizara ili tuweze kulikamilisha hili,” amesema Dk Mwigulu.
Baada ya maelezo hayo Makalla amesema: “Ndugu zangu huyu ndiye waziri wa fedha amenihakikishia fedha zimetengwa katika bajeti inayoishia Juni 30, 2025 atahakikisja baada ya mkutano huu fedha zinapatikana na atawasiliana na wanaohusika ili fedha ziweze kulipwa kwa wananchi kwa wakati ili waweze kunufaika na kile ambacho waliahidiwa.”
Makalla yuko mkoani Lindi kwa ziara ya siku nane ambayo inalenga kukiimarisha Chama hicho na kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025.