Iringa. Kinachoendelea kwa sasa baina ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ni mnyukano wa piga nikupig. Ndivyo unavyoweza kueleza kutokana na Makalla kufurumusha tuhuma kuhuu Chadema kila anaposimama jukwaani kuzungumza n wanachama na makada wa CCM.
Kwa sasa Makalla amekuwa akikishambulia Chadema kuwa hakina ajenda, hakina fedha na hakijajindaa kupambana kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba, 2025.
Hata hivyo, Chadema nacho kimeendelea kujibu mashambulizi ya Makalla huku kikiweka bayana kuwa, kila kitu kipo sawa.
Akizungumza na wanachama na makada wa CCM leo Jumamosi Machi 29, 2025 wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja Mwembetogwa mkoani Iringa, Makalla amesema hata kampeni ya No reforms, no election haijaeleweka miongoni mwa wanachama wa Chadema.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia amesema chama hicho hakina mgogoro wowote wa ndani na kazi zinaendelea ikiwamo kufanya mikutano kama ambavyo CCM kinafanya.

Katibu wa Itikadi,Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla akihutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Mwembetogwa, Manispaa ya Iringa
“Kazi zinaendelea na kesho tutakuwa Iringa, kuhusu No reforms, no election, sio msimamo wa Lissu, ulitangazwa tangu Desemba mwenyekiti akiwa Mbowe (Freeman). Sio kwamba Chadema haijajiandaa na uchaguzi, tumeona yaliyotokea mwaka 2024 kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, ndio tukasema hatuendi bila mabadiliko, wafanye mabadiliko tutakwenda kwenye uchaguzi,” amesema Rupia.
Katika mkutano huo, Makalla aliyeambatana baadhi ya wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM na kamati ya siasa ya mkoa wa Iringa, amedai Chadema haina fedha hata mkutano wao kesho wa hadhara wanaungaunga.
“Hata mkutano wa kesho wanahangaika kufanya fedha hawana, wataweza uchaguzi mkuu? amehoji.
Katika maelezo yake, Makalla amedai kuna mgogoro unaondelea kufukuta ndani ya Chadema kati ya kambi ya Mbowe na Lissu zinazoendelea kunyukana tangu kumalizika kwa uchaguzi wa chama hicho, uliofanyika Januari 2025.
“Si mmesikia kilichompata Katibu Mwenezi wa Bawacha (Siglada Mligo) aliyetandikwa kwenye kikao cha ndani, kuna vita kubwa ndani ya chama chao,” amedai Makalla.
Kuhusu kampeni ya ‘bila mabadiliko, hakuna uchaguzi’, Makalla amesema kuna watu ndani ya Chadema wanataka udiwani na ubunge, lakini wamegawanyika kuhusu msimamo huo.
Katika hatua nyingine, mwenezi huyo amesema yupo tayari kubeba kila aina ya mashambulizi ikiwemo kejeli kutoka kwa vyama vya upinzani, kikiwemo Chadema, akisema ndiyo kazi ya uenezi.
Mbunge wa Iringa Mjini, Jesca Msavatavangu amesema CCM ni chama cha kushika dola, hivyo kimejipanga ipasavyo kushinda uchaguzi mkuu kutokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Msambatavangu ametolea mfano upatikanaji wa umeme katika jimbo hilo kuwa imefika asilimia 90 bado mitaa michache kufikiwa na huduma hiyo, akisema kwa hali waliofikia CCM inakila sababu ya kutembea kifua mbele.
“Sh5 bilioni zimetolewa na Serikali katika kipindi cha miaka minne kuanzia shule za shikizi, awali na msingi. Wakati Sh10 bilioni zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari,” amesema Msavatavangu
Msambatavangu amesema mbali na miundombinu ya elimu, lakini imewezesha upatikanaji wa walimu katika shule mbalimbali. Pia Serikali imeboresha huduma ya afya ikiwamo uboreshaji wa hospitali ya mkoa wa Iringa.

Mbunge wa zamani wa Iringa Mjini na kada wa CCM, Mchungaji Peter Msigwa amesema kama Chadema wanataka demokrasia ya kweli wasikimbie bali waingie uwanjani.
“Nashauri Chadema wakae na kutafakari kuhusu kampeni yao kwani, itakwenda kukiua chama chao, jambo ambalo CCM haina nia hiyo,”
“Siasa ni mchezo ambao hautaji hasira nendeni mkashawishi wananchi ili mpendwa na kushiriki uchaguzi, lakini sio kuzuia uchaguzi jambo lisilowezekana,” amesema Msigwa ambaye ni kada wa zamani wa Chadema.
Kwa mujibu wa Mchungaji Msigwa, Rais Samia Suluhu Hassan ana kila sababu ya kuendelea kuchaguliwa ili kutetea nafasi hiyo, kwa mara nyingine kutokana na kazi kubwa aliyoifanya ndani ya miaka minne ya utawala wake.