Mbeya. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amesema chama hicho hakitawabembeleza Chadema ili kishiriki Uchaguzi Mkuu, kisiposhiriki itakuwa mwisho wao kuwa chama kikuu cha upinzani nchini.
Amesema CCM kinaheshimu sheria na hakiwezi kwenda kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo kitashiriki uchaguzi ambao maboresho mbalimbali ya sheria ya uchaguzi yamefanyika kupitia kikosi kazi kilichoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Hata hivyo, Chadema, ambacho kinashikilia kunadi ajenda ya “No Reforms, No Election” Nyanda za Juu Kusini, kwa nyakati tofauti kimesema hakitasusia uchaguzi bali kitashinikiza umma kuuzuia mchakato huo.
Makalla ameeleza hayo leo, Alhamisi Machi 27, 2025, wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Ruanda Nzovwe, jijini Mbeya. Mwenezi huyo yupo katika ziara ya siku moja mkoani Mbeya, kisha kesho, Ijumaa Machi 28, ataelekea mkoani Iringa.
“Hawa watu wanasema, oooh, tutazuia uchaguzi kwa nguvu ya umma.’ Hapa Mbeya wana nguvu ya umma? CCM itashiriki uchaguzi kwa sababu maandalizi yanaendelea na tumejipanga kushinda kwa kishindo.
“Narudia, Chadema hatuna haja ya kuwambeleza. Tunakwenda kwenye uchaguzi kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania. Kama hawashiriki, shauri yao, na baada ya uchaguzi, itakuwa mwisho wao wa kuwa chama kikuu cha upinzani Tanzania,” amesema Makalla.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia, ameiambia Mwananchi kuwa msimamo wa chama hicho kwa sasa ni “No Reforms, No Election” na hawatarudi nyuma katika ajenda hiyo.

“Waache wafanye wanavyofanya. Msimamo wetu ni kuwaelimisha wananchi kuhusu ‘No Reforms, No Election.’ Haturudi nyuma katika hili. Mpango wetu ni ‘No Reforms, No Election,’ hatuna mpango mwingine,” amesema.
Kwa mujibu wa Makalla, Chadema kinaogopa uchaguzi, ndiyo maana kinaogopa kuingiza timu uwanjani, hivyo wananchi wanapaswa kupuuza ajenda yao.
“Ushindi wa asilimia 99 katika uchaguzi wa Serikali za mitaa ulikuwa tunajaribu mitambo, sasa imetiki. Sasa hiyo mitambo tutashinda uchaguzi mkuu,” amesema Makalla.
Makalla amesema CCM inakwenda kwenye uchaguzi mkuu ikijivunia rekodi nzuri ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, huku akitumia fursa hiyo kuwapongeza wana-CCM wa Mbeya kwa kukipa ushindi chama hicho katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika mwaka 2024.
Kada wa CCM, Mchungaji Peter Msigwa, amesema 2025 ni mwaka wa uchaguzi, hivyo vyama lazima vijiandae. Hata hivyo, amesema kuna wengine wameshaanza kuweka mpira kwapani, licha ya Serikali kuja na 4R (Ustahimilivu, Kujenga, Mageuzi na Maridhiano) ili kuwepo na ushindani wa kweli.
“Wamekuja na mkakati wa ‘No Reforms, No Election’ ambao hauwezi kufanikiwa wala kutekelezeka. Ili wawe na uhalali wa kutaka mabadiliko, lazima waanzie ndani ya chama hicho kwanza,” amesema Msigwa.
Mchungaji Msigwa, aliyewahi kuwa mbunge wa wa Iringa Mjini na Mwenyekiti wa zamani wa Chadema Kanda ya Nyasa, amesema alifikia uamuzi wa kuondoka katika chama hicho kwa kile alichodai kuwa hakuna haki wala demokrasia.