
Dar es Salaam. Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla amesema chama hicho hakikubadili gia angani kwa kuwateua wagombea urais mapema kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Badala yake, amesema uamuzi wa kuwateua wagombea hao, umechochewa na shinikizo la wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho, baada ya kuridhishwa na namna makada hao walivyotekeleza ilani.
Kauli hiyo ya Makalla inajibu uamuzi wa mkutano mkuu wa CCM wa Januari 18 na 19, 2025 ambao pamoja na mambo mengine uliwateua Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea urais katika uchaguzi wa baadaye mwaka huu na Dk Hussein Mwinyi kugombea nafasi hiyo kwa upande wa Zanzibar.
Uteuzi wa wagombea hao, ulifanyika ikiwa si miongoni mwa ajenda zilizotangazwa awali kuelekea mkutano huo, jambo lililosababisha kuwepo wale wanaosema kwa kitendo hicho CCM imebadili gia angani.
Lakini, hoja ya kubadili gia angani, ilitokana na chama hicho kufanya uamuzi huo mapema, tofauti na miaka yote ya kuelekea uchaguzi mkuu.
Sambamba na majibu hayo, Makalla pia amerusha kijembe akikosoa msimamo wa Chadema kuhusu ‘No Reform, No Election’ akisema ni maneno matupu kama ilivyo kwenye khanga.
Makalla ameyasema hayo leo Jumapili, Februari 2, 2025 alipozindua sherehe za maadhimisho ya miaka 48 ya CCM kwa Mkoa wa Dar es Salaam.
Katika maelezo yake, amesema baada ya wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho kupokea taarifa za utekelezaji wa ilani kwa pande zote za muungano, wakaagiza Rais Samia na Dk Mwinyi wateuliwe tena kugombea urais.
“Hivi kikao kikubwa kama kile kikishaagiza vikao vingine vinafanyaje. Hapohapo kamati maalumu ilikaa na kumchagua Dk Mwinyi kuwa mgombea urais wa Zanzibar na NEC nayo ilimpigia kura na kumpitisha kwa asilimia 98,” amesema.
Vivyo hivyo, amesema ndivyo ilifanyika kwa Rais Samia na alipitishwa na wajumbe wa mkutano huo kwa asilimia 100.
Hatua hiyo, amesema ilifuatiwa na uthibitishaji wa jina la mgombea mwenza na Dk Emmanuel Nchimbi na alipitishwa.
Katika hatua nyingine, Makalla amesema msimamo wa Chadema wa kutofanyika uchaguzi pasi na mabadiliko ya sheria, ni maneno ambayo hata kwenye khanga huandikwa.
“Tutafanya siasa za kistaarabu kwa sababu yapo mambo mengi mazuri ya kusema. Hao wanaojitoa ufahamu kwamba no reform no election hayo ni maneno ya kwenye Khanga,” amesema.
Hata hivyo, amesema kauli ya hivi karibuni ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu inayofafanua No reform no Election si kususia uchaguzi, inaonyesha chama hicho kimeridhia kuingia kwenye uchaguzi.
Licha ya kauli hiyo ya Makalla, Lissu katika ufafanuzi huo alipokuwa anazungumza na moja ya vyombo vya habari nchini, alisema chama hicho hakitasusia uchaguzi bali hakitaruhusu uchaguzi ufanyike pasi na mabadiliko ya sheria zinazousimamia.
Ili kujua watafanyaje kushinikiza mageuzi hayo ya sheria kabla ya uchaguzi, Lissu aliweka wazi kuwa mwezi huu wataketi kujadili nini wafanye kufanikisha msimamo huo.
Katika mkutano huo, Makalla amesema mageuzi ni suala la kisheria na wananchi wasidanganywe.
Ametumia jukwaa hilo, kuwataka watendaji wa Serikali waendelee kuwa wasikivu wa wahakikishe ofisi zao zinakuwa kimbilio la wananchi.
Amesema hata ofisi za chama hicho zitakuwa tayari kusikiliza kero za wananchi na huo ndio msingi wa CCM kuaminiwa.
Amewahimiza wanachama wa chama hicho kujiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura, kwani ndio mwanzo wa safari ya kuutafuta ushindi.
Katika miaka 48, amesema kuna mafanikio lukuki yakiwemo mageuzi ya kiuchumi katika jamii, kupitia uboreshaji wa huduma kwa jamii na miradi ya maendeleo.
Amani na utulivu ni jambo lingine ambalo CCM inajivunia inapoadhimisha miaka 48 ya kuzaliwa kwake.
Sambamba na hilo, amesema chama hicho kimeendelea kuwa imara na sasa kimefikia hatua ya uimara usiolingana na wakati wowote.
Amesema CCM kwa sasa ina wanachama milioni 12 kuliko chama kingine chochote Afrika.
Kwa duniani, amesema CCM ni chama namba saba kwa wingi wa wanachama duniani.
“Hii maana yake, CCM ndio chama chenye mvuto na kinachokubalika hapa Tanzania, hayo ni mafanikio tunayoyaeleza wakati tunaadhimisha miaka 48 ya kuzaliwa kwa chama chetu,” amesema.