Makalla: CCM haijiweki yenyewe madarakani

Newala. Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amesema dhana ya baadhi ya watu vikiwamo vyama vya siasa kudhani kuwa chama chake kinajiweka chenyewe madarakani ni potofu.

Amesisitiza kwamba ushindi wa CCM mara zote hutokana na kazizinazofanywa na viongozi wake wa chama na Serikali.

Akizungumza leo Jumatano Aprili 16, 2025 mbele ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Butiama wilayani Newala mkoani Mtwara, Makalla amesema CCM hailazimishi  kukaa madarakani bali hutokana na sanduku la kura.

“Wapo wanaosema wamekichoka Chama cha Mapinduzi. Wanasahau kuwa sisi hatujiweki wenyewe madarakani. Hatujilazimishi. Tunawekwa na Watanzania kupitia sanduku la kura kutokana na kazi tunayofanya na imani waliyonayo kwa viongozi wetu,” amesema Makalla.

Amesema CCM hakikumweka madarakani Rais Samia Suluhu Hassan na wengine waliomtangulia kwa nguvu, bali kwa ridhaa halali ya wananchi kupitia kura zao.

“Chama hakijamuweka Samia kwa mabavu. Wananchi wamempa ridhaa kutokana na uchaguzi uliofanyika huko nyuma na kazi anayoifanya. Ameonyesha kuwa na dhamira ya kweli ya kuleta maendeleo. Kama kuna mtu ana sera bora au ilani bora kuliko ya CCM, aje tulinganishe Kisha wananchi wataamua,” amesema.

Akijibu hoja za baadhi ya watu wanaodai kuwa uchaguzi hautakuwa huru, Makalla amesema demokrasia haiwezi kusimama kwa sababu ya uamuzi wa mtu binafsi au kikundi fulani.

“Uchaguzi utaendelea hata kama vyama vingine vikisusia. CCM itashiriki uchaguzi na hivi karibuni itazindua Ilani yake,” amesema.

Kauli hiyo ya Makalla inakuja wakati Tanzania inajiandaa kuelekea katika uchaguzi wake mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utakaonyika Oktoba mwaka huu.

Neno kwa Mkuchika

Katika mkutano huo, Makalla alitoa heshima kwa mwanasiasa mkongwe, George Mkuchika ambaye ametangaza rasmi kustaafu siasa, akisema ametoa mchango mkubwa kwa Taifa na sasa anahitaji kupumzika.

“Mzee wetu ametangaza kustaafu. Naamini atakayekuja kumrithi ni lazima awe mwenye nguvu. Mzee Mkuchika amechoka na amestaafu kwa heshima. Si kila mtu anaweza kustaafu kwa kusema ‘nimechoka’. Tutazidi kuchota busara zako, naamini pale utakapohitaji ushirikiano, utakuwapo,” amesema Makalla.

Akizungumza katika mkutano huo, Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye amemsifu Mkuchika kwa uamuzi wake wa kung’atuka rasmi kutoka kwenye siasa za uchaguzi, akisema huo ni mfano bora wa uongozi wa busara na wa kuigwa na viongozi wengine wa kisiasa.

Amesema Mkuchika amefanya uamuzi wa kishujaa kwa kuamua kung’atuka huku bado akiwa na mvuto na mapenzi makubwa kutoka kwa wananchi wa Newala na Mkoa wa Mtwara kwa ujumla.

“Mzee Mkuchika ni Mmakonde halisi, ametoka hapa kwetu Kusini. Amelitumikia taifa kwa uadilifu mkubwa, na sasa anastaafu bila kuwa na hata doa moja la kashfa,  jambo la nadra sana katika siasa,” amesema Nape.

Akiweka wazi uhusiano wake wa karibu na Mkuchika, Nape amesema hata baada ya kifo cha baba yake mzazi, Mkuchika ndiye aliyekuwa mlezi wake katika siasa na maisha yake kwa ujumla.

“Mimi ni mtoto wa Kimakonde. Marehemu baba yangu alipofariki dunia, aliniacha mikononi mwa Mzee Mkuchika. Hivyo, kwa kweli amekuwa mlezi na mwalimu kwangu. Sasa amestaafu, tuache apumzike. Tujifunze kusema mazuri ya mtu akiwa hai, si kungojea afe ndipo tumsifie,” amesisitiza Nape.

Mbunge huyo wa Mtama amehitimisha kwa kutoa somo la uongozi, akisema: “Ukijua mlango wa kuingilia, tafuta na mlango wa kutokea kabla watu hawajakutoa. Niamini, huu ni uamuzi wa hiari, japo amefunga mlango wake kwenye makaratasi, lakini moyo wake wa utumishi utaendelea kuwapo kwa jamii.”

Mkuchika asisitiza kupumzika

Katika kuonesha msimamo wake wa kisiasa wa eneo hilo, Mkuchika ametoa tamko lenye taswira ya umakini katika uchaguzi.

“Kuna uyoga unaliwa na kuna uyoga mwingine ukichanganya unaweza kupata matatizo. Sisi hapa tumeamua, hakuna kuchanganya. Tunasimama na CCM, hatutaki mchanganyiko, iwe hivyo kuanzia kwa Rais Samia na kwa mbunge na madiwani watakaoteuliwa,” amesema Mkuchika.

Makalla anaendelea na ziara yake ya kukagua  utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025 katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *