Makalla awatupia kijembe Chadema

Mafinga. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amewataka watiania ubunge na udiwani kwa tiketi ya Chadema, kujiunga na vyama vingine ili kutimiza ndoto zao badala ya kunga’nga’nia chama hicho, ambacho kina ajenda ya No Reforms, No Election inayowaweka njia panda makada wao.

Katika maelezo yake, Makalla amesema kila anapozungumzia suala la Chadema kushiriki Uchaguzi Mkuu, amekuwa akipata marafiki wengi wakiwemo wanaotaka ubunge na udiwani kutoka chama hicho, waliomtaka akomalie hoja hiyo hadi kieleweke.

Aprili 3, 2025 Chadema kimewaita watia nia wote wa udiwani na ubunge kujadili mwenendo wa hali ya kisiasa kikao kitakachofanyika makao makuu ya Chadema Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Wakati kikao hicho kikikaribia baadhi ya watiania  wamekuwa njia panda kuhusu mustakabali wao wa kisiasa, kutokana na msimamo wa No Reforms No Election, lakini wengine wanafikiria kuhamia vyama vingine ili kuwania udiwani na ubunge.

Makalla ameeleza hayo leo Ijumaa Machi 28, 2025 akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja Mashujaa wilayani Mufindi mkoani Iringa katika akianza ziara ya siku mbili mkoani Iringa.

“Naomba watia nia nia vyama vipo vingi kuna CCM na vyama vingine 17 nendeni mkagombee wamefungwa wakati wana ndoto zao. Maana wameingia wanafikiria udiwani na ubunge, lakini wanakatishwa tamaa,” amesema Makalla.

Amesisitiza kuwa vijana, kina mama wa Chadema na wengine wenye ndoto za udiwani na ubunge vyama vipo vingi waende wakajiunge navyo ili kutimiza ndoto zao za kuwania nafasi za uongozi kupitia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Mbali na hilo, Makalla ambaye amewahi kuwa mkuu wa mikoa ya Mwanza, Katavi na Mbeya amewataka Watanzania kuwapuuza baadhi ya watu wanaosema chama hicho, hakijatimiza majukumu yake ya kuisimamia Serikali.

Makalla amesema Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya mambo makubwa ikiwemo kuboresha huduma za jamii na kuwakwamua kiuchumi wananchi katika kipindi cha miaka minne.

Afanya harambee ya matibabu ya kada Chadema

Akiwa mbioni kumaliza hotuba yake Makalla aliendesha harambee ya papo kwa papo kwa wanachama na wananchi ili kumchangia Siglada Mligo (Mwenezi wa Baraza la Wanawake la Chadema Taifa) kwa matibabu zaidi.

Katika harambee hiyo, Makalla amesema zaidi ya Sh1.5 milioni zilipatikana ikiwa ni pamoja na fedha taslimu na ahadi zilizotolewa na viongozi wa CCM wakiwemo wajumbe wa halmashauri kuu ya chama hicho.

“Kina mama huyu ni mwenzenu,  kama una 500 lete hapa kila anayeguswa aje hapa, Msigwa njoo hapa. Tutamchangia kama ambavyo tulifanya kwa Lissu ili kufanya matengenezo ya gari lake.

“Hii ndiyo 4R CCM tuna uungwana, wastahimilivu, tutamtumia mchango huu ili akapate matibabu zaidi hospitali ya Peramiho mkoani Ruvuma. Nimeongea naye (Siglada) asubuhi, maana sisi ni wenezi wa vyama,” amesema Makalla.

“Hii ni kuonyesha Watanzania tupo pamoja, tunatofautiana kiitikadi lakini sisi ni Watanzania,” amesema Makalla.

Mligo anadaiwa kushambuliwa na kujeruhiwa na mlinzi wa chama hicho, Machi 25 katika kikao cha ndani cha viongozi wa Chadema, kilichongozwa na  Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara).

Inadaiwa kuwa sababu za Mligo kushambuliwa ni baada ya kunyimwa nafasi ya kujitetea kwa tuhuma alizopewa katika kikao cha ndani kilichofanyika mkoani Mbeya.

Kada wa CCM, Mchungaji Peter Msigwa amedai mkakati wa No Reforms, No Election hauendani na mila na desturi za Kitanzania, akiwataka Watanzania wapuuze ajenda ya bila ya mabadiliko, hakuna uchaguzi.

Mchungaji Msigwa aliyewahi kuwa mbunge wa Iringa Mjini kwa miaka 10, amesema Serikali imefanya mambo mengi ya kimaendeleo lakini kazi ya Chadema ni kupinga kwa kila kitu jambo ambalo siyo sahihi.

“Tumpe ushirikiano Rais Samia katika uchaguzi mkuu, puuzeni vyama vya upinzani havina hoja kwa sasa, kura zote kwa Samia, msipoteze kura zenu CCM ndio chama kinachoshughulika na changamoto za Watanzania,” amesema Mchungaji Msigwa.

Naye Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Cosato Chumi amesema Serikali imetekeleza miradi mbalimbali ikiwemo afya, elimu ili kurahisisha huduma kwa wananchi wa wilaya Mafinga mkoani hapa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *