Makalla awataka mabalozi CCM kuhamasisha uandikishaji daftari la wapigakura

Muleba. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amewapa rungu mabalozi wa chama hicho nchini la kuhamasisha Watanzania wakiwemo vijana kujitokeza katika mchakato uandikishaji na uboreshaji wa daftari la kuduma la wapigakura awamu ya pili.

Makalla amesema jambo muhimu katika  mchakato wa uchaguzi ni kuhakikisha wananchi wamejiandikisha na kuboresha taarifa zao katika daftari la mpigakura, ndio maana CCM kimekuwa mstari wa mbele kuhamasisha uandikishaji.

Katibu huyo mwenezi ametoa kauli hiyo, leo Jumatatu Mei 19,2025 wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Fatuma wilayani Muleba mkoani Kagera katika mwendelezo wa ziara yake katika kanda ya ziwa iliyoanza jana Mei 18, 2025.

Makalla amesema ratiba ya INEC, uandikishaji na uboreshaji wa taarifa za mpigakura unafanyika katika mikoa 11 ya Tanzania Bara na mikoa mingine ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa INEC, mzunguko wa pili wa mchakato wa uboreshaji wa Daftari la Kuduma la Wapigakura umeshaanza ukihusisha mikoa 16 Tanzania Bara na Zanzibar.

Mei 17, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan aliboresha taarifa zake, jijini Dodoma akitoa wito kwa Watanzania kujitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa zao na kwa ambao hawajafikiwa na mzunguko wa pili wakiukosa hawatakuwa na nafasi tena.

” Awamu hii inawapa fursa pia hata vijana ambao kwa sasa wanatimiza wana miaka 17 na miezi, lakini ikifika Oktoba watatimiza miaka 18 ni muda wa kujiandikisha daftari litakapopita awamu hii. Ni fursa nzuri kwa vijana wetu, mkajiandikishe ili tupate wapiga kura.

“Katika uchaguzi mtu anatangazwa ameshinda kwa wingi wa kura, kwa hiyo WanaCCM tuna mtaji wa wanachama milioni 11, nimeanza kwa kuwasalimia mabalozi kwa sababu ndio msingi wa chama chetu, mpo karibu na wapigakura, wananchi na wanachama,”  amesema.

Kwa mujibu wa Makalla, mabalozi wakitekeleza majukumu yao vema, matawi, kata, wilaya, mkoa hadi ngazi ya Taifa ya CCM itafanya kazi nzuri. Amesema msingi wa CCM ni mabalozi, hivyo amewaomba kutekeleza jukumu hilo.

“Niwaombe mabalozi awamu itakayokuja hamasisheni watu wakiwemo vijana waende kuboresha daftari la wapigakura. Hakikisheni mnapita nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa kwa sababu ndio mnaoishi karibu na watu.

” Tukifanya kazi hiyo vizuri ikifika Oktoba tutahakikisha tunazima zote… tunawasha kijani maandalizi ya uchaguzi ni pamoja na watu kujiandikisha,” amesema Makalla.

Amesema WanaCCM milioni 11 kila mmoja akihamasisha watu kupiga kura basi chama hicho tawala kitapata kura za kutosha katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba ambao kwa mara ya kwanza utasimamiwa na INEC.

Katika hatua nyingine, Makalla amesema CCM inatambua wananchi wa Kagera katika kufanikisha mchango wa maendeleo mkoani humo, akiwataka kupuuza lugha na maneno ya kejeli zinazotolewa na wanasiasa mbalimbali.

Awali mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage amesema wabunge wa Mkoa wa Kagera, wamepeana majukumu ya kuhakikisha wanatafuta kura zaidi ya milioni 1.5 za mgombea wa urais wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan.

“Kulikuwa na changamoto ya maji hapa, lakini Serikali imeleta mradi wa maji Muleba Magharibi, pia Serikali imeagiza visiwa vyote 38 vya Muleba kuwekewa umeme, ndio maana tunasema kura zake milioni 1.5 tunamtafutia,” amesema Mwijage.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *