Makalla aonya makundi kutishia ushindi wa CCM uchaguzi ujao

Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla ameonya kuhusu makundi yaliyoanza kuota mizizi kuelekea uchaguzi mkuu ujao huku akisema yanaweza kuwa turufu kwa upinzani kushinda nafasi za ubunge na udiwani.

Baadhi ya makada wa chama hicho wameanza kujipitisha majimboni kwa mitindo tofauti wakitengeneza mtandao na kutangaza nia za kuwania nafasi za uongozi kwenye kata na majimbo, jambo linalopigwa vita na uongozi wa CCM.

Januari 2025, chama hicho kilifanya mabadiliko madogo ya katiba yao kwa kuongeza idadi ya wajumbe wa kupiga kura za maoni kuchagua wagombea kwenye kura za maoni kutoka wajumbe 10 hadi 20 ili kupanua demokrasia na kuziba mianya ya rushwa.

Kutokana na mabadiliko ya katiba hiyo, sasa iwapo katika jimbo moja wakijitokeza watia nia 70, mchujo utafanyika na kupitisha majina matatu pekee ambayo yapelekwa ngazi ya juu kupigiwa kura na kupatikana jina moja la kupeperusha bendera katika eneo husika.

Leo Alhamisi, Machi 6, 2025, Makalla akiwa kwenye mwendelezo wa ziara yake ya mikutano ya ndani, Segerea, Dar es Salaam, amesema siri ya kuvuna ushindi wa kimbunga katika uchaguzi mkuu ni kuwa wamoja.

“Makundi na mgawanyiko unaoendelea kuelekea kwenye kura za maoni ndani ya chama chetu, hasa kwa Mkoa wa Dar es Salaam, hauwezi kuwa na tija na niseme wanaofanya tabia ya kuongoza makundi hayo wanaturahisisha kuwaengua kwenye mchujo,” amesema Makalla.

Makalla ambaye ni mlezi wa chama Mkoa wa Dar es Salaam, amesema hawezi kukubali makundi hayo yaendelee, atatumia nafasi yake ya kuingia kwenye vikao vya halmashauri kuu, sekretarieti na kamati kuu kudhibiti watu wa aina hiyo.

“Mkoa wa Dar es Salaam unawapiga kura wengi kuliko mkoa mwingine wowote Tanzania, sasa migawanyiko kuelekea kwenye kura za maoni inaweza kutukosesha ushindi kwenye uchaguzi mkuu kwenye nafasi ya udiwani na ubunge na kuwapa nafasi upinzani,” amesema.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na viongozi wa chama hicho, jumuiya ngazi ya shina, tawi, mitaa, kata na Wilaya ya Ilala, Makalla amesema viongozi wanapaswa kufuatilia ili kuhakikisha kila mmoja anaondoa makundi.

Hoja ya makundi kuelekea kura za maoni ilianza kuibuliwa na mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM, Ibrahim Msengi, aliyesema mgawanyiko na makundi yanayojitokeza yasipodhibitiwa yanaweza kuwagharimu kwenye uchaguzi mkuu.

“Tunaweza kuchukua viti vyote vya udiwani katika kata zote 102 za Mkoa wa Dar es Salaam, lakini wasiwasi wangu ni huu mgawanyiko unapojitokeza, tunasababisha kuwapa nafasi upinzani, kura za maoni zisituchanganye, tubaki kuwa wamoja tukilinde chama chetu na kukitetea,” amesema.

Awali, mbunge wa Ilala, Mussa Zungu amesema wanafanya kazi kwa kushirikiana na Serikali kuwatumikia wananchi kuwaletea maendeleo na huduma za msingi.

“Serikali ilituletea fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya barabara, kuna baadhi ya barabara zimeanza kujengwa kwa kiwango cha lami na zege,” amesema.

Zungu ambaye ni Naibu Spika wa Bunge, amesema kutokana na maendeleo hayo, wanajiona wana deni la kulipa katika uchaguzi mkuu mwaka huu kwa kuwapigia kura za kutosha madiwani, wabunge na urais.

“Nawaomba wanachama wenzangu tusihangaike na madalali wa kusaka vyeo, udiwani na ubunge, hawana hoja,” amesema.

Makalla alianza ziara hiyo Machi 4 na anatarajia kuhitimisha Machi 8 katika Wilaya ya Kigamboni. Lengo la ziara hiyo ni kuwahamasisha wanachama wa chama hicho kujitokeza kwa wingi kwenye shughuli ya uboreshaji wa taarifa zao kwenye daftari la kudumu la mpigakura.

Kazi ya uboreshaji wa taarifa za wapigakura kwa mkoa huo inatarajiwa kuanza Machi 17 hadi 23, 2025 ambapo Mkoa wa Dar es Salaam itahitimisha baada ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kupita katika mikoa yote Tanzania.