Makada CCM watoa angalizo kujirudia ya 2015 Moshi Vijijini

Moshi. Joto la kusaka ubunge katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2025 kwenye Jimbo la Moshi Vijijini, mkoani Kilimanjaro limezidi kupanda baadhi ya makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakitajwa kuingia katika mbio kuliwania.

Jimbo hilo linaloongozwa na Profesa Patrick Ndakidemi (CCM) ni miongoni mwa majimbo tisa ya uchaguzi yaliyopo mkoani Kilimanjaro.

Licha ya muda bado haujatamatika, tayari baadhi ya makada wanadaiwa kujipitisha wakionyesha nia ya kurithi mikoba ya Profesa Ndakidemi.

Miongoni mwa wanaotajwa, ni waliojitokeza katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 waliobwagwa na Profesa Ndakidemi katika kura ya maoni ndani ya CCM.

Katika uchaguzi mkuu wa 2020, ndani ya CCM walijitokeza zaidi ya makada 40 kuomba kuteuliwa na chama hicho kupeperusha bendera ndani ya jimbo hilo.

Kwenye kura ya maoni, Profesa Ndakidemi alishinda kwa kura 262, huku aliyemfuatia akipata kura 46 na aliyeshika namba tatu akipata kura 35.

Makada hao licha ya kudaiwa kutengeneza kambi kupitia baadhi ya madiwani jimboni humo, wanatajwa kuongeza ukarimu kwa jamii, huku wengine wakidaiwa kutumia nafasi zao kujipitisha kuongeza ushawishi wa kukubalika kwa wajumbe na jamii.

Mbali ya waliobwagwa kwenye kura ya maoni katika uchaguzi uliopita, pia anatajwa kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambaye ni mbunge wa viti maalumu.

Mbunge huyo anajipitisha akidai ana baraka zote za viongozi wa juu wa CCM, ambao hata hivyo mara kadhaa wamesikika wakikemea vitendo vya walionza kusaka udiwani na ubunge mapema.

Ni kutokana na mvutano uliopo, baadhi ya wanaojipitisha wanatajwa kufikia hatua ya kuchafuana kwenye mitandao ya kijamii.

Mwananchi ilipomtafuta Profesa Ndakidemi kuzungumzia yanayoendelea jimboni amesema kwa sasa hawezi kusema chochote.

Hata hivyo, mwaka 2024, Mwananchi liliripoti kuhusu baadhi ya madiwani wa kata ndani ya jimbo hilo, kudaiwa kumpinga wazi-wazi Profesa Ndakidemi, kauli zao zilihusishwa na vita vya ubunge 2025.

Mbunge huyo wakati huo alikaririwa akisema anafahamu kinachoendelea jimboni na kwamba,  viongozi wa CCM wa kitaifa, mkoa na wilaya walishatoa maelekezo na kuonya watu kuacha kampeni kabla ya muda kwa kuwa hatua hiyo inakivuruga chama na kuwachanganya wananchi.

Profesa Ndakidemi alisema ni vyema wenye nia ya kutafuta ubunge wakawaacha waliopo madarakani watimize majukumu yao ya kuwatumikia wananchi na wakati ukifika nafasi itatolewa kila mwenye nia akachukue fomu.

Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Mercy Mollel alipotafutwa kuzungumzia vuguvugu hilo la uchaguzi, amesema hana taarifa kama kuna mtifuano wa kusaka ubunge katika majimbo ya mkoa huo.

“Sina taarifa yoyote kama kuna migogoro na mtifuano majimboni kwa sababu hakuna taarifa iliyoripotiwa labda niulizie nikisikia ndipo nizungumze.

“Kuhusu makundi ya WhatsApp, mimi sifanyii kazi vitu vya makundi (magroup ya WhatsApp) lakini nitamuuliza Katibu wa Wilaya ya Moshi Vijijini ili kujua kama kuna kinachoendelea. Ninachotaka kukuambia sina taarifa hizo, sijasikia na hakuna mtu aliyeleta malalamiko kwangu,” amesema.

Hali ilivyo

Jimbo la Moshi Vijijini lenye kata 16 kwa sasa kumeibuka mtifuano kati ya baadhi ya makada wanaotafuta ubunge, huku wakidaiwa kuwarubuni madiwani.

Madiwani jimboni humo ambao wote ni kutokana na CCM, wapo wanaodaiwa kujitokeza hadharani kumpinga Profesa Ndakidemi na kutamka wazi hawawezi kufanya naye kazi.

Kwa mujibu wa wana-CCM, kuna mpasuko unaoweza kukigharimu chama hicho katika uchaguzi mkuu wa 2025.

Katika moja ya kikao cha halmashauri kuu ya CCM wilayani humo kilichofanyika mwaka 2024, Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya hiyo, Sirili Mushi alifichua uwepo wa baadhi ya madiwani aliodai wamenunuliwa na wameanza kupita mtaani kumnadi mgombea wao.

Ingawa katika kikao hicho mwenyekiti hakumtaja mbunge anayepingwa na kukejeliwa, lakini taarifa zilidai vita kubwa ipo katika jimbo la Moshi Vijijini licha ya kwamba wilaya hiyo kichama inalo pia jimbo la Vunjo.

Mwenyekiti huyo alisema kumeibuka makundi ya wanaosaka ubunge, ambao wanawarubuni baadhi ya madiwani ili kuwaunga mkono na kumkataa mbunge aliyepo, lakini tayari chama kimepata video ya mmoja wa madiwani hao.

Kwa mujibu wa Mushi, katika video hiyo anasikika diwani huyo akisema hawezi kufanya kazi na mbunge na kwamba, CCM imeanza kuchukua hatua kwani hawatakubali watu wachache wakisababishie mpasuko.

Alisema hali hiyo inaweza kukigharimu chama hicho katika uchaguzi, akisisitiza wanachofanya ni nje ya maadili ya chama.

Makada wafunguka

Wakizungumza baadhi ya makada wa CCM, wamedai mtifuano kwa sasa ni mkali na chama kinapaswa kuchukua hatua stahiki kwa wanaokiuka taratibu na kanuni za CCM.

Ansi Mmasi, amesema kinachoendelea mitaani na kwenye mitandao ya kijamii si sahihi na kwamba, wote ambao wameanza kampeni mapema wanapaswa kuitwa kuhojiwa na kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

“Siyo sahihi kwa kinachoendelea cha baadhi ya makada kuanza kuchafuana kwani wakati bado haujafika. Wakati wa kampeni haujafika, Bunge bado halijavunjwa na baraza la madiwani halijavunjwa,” amesema Mmasi amabye ni kada wa chama hicho.

“Kwa mujibu wa chama chetu kujipitisha ni ulafi wa madaraka na watu kama hao wanatakiwa wachukuliwe hatua za kinidhamu. Taratibu za kuwachukulia hatua zipo, kwani kamati ya maadili ipo kuanzia ngazi za tawi, kata, wilaya na mkoa,” amesema na kuongeza:

“Wale ambao wameanza kuchafuana ndani ya chama chetu wachukuliwe hatua za kinidhamu. Kamati za maadili kuanzia matawi, kata na wilaya wasimame kwenye nafasi zao.”

Mmasi ambaye ni mwanasiasa wa siku nyingi, amesema hatua zisipochukuliwa hali hiyo inaweza kuathiri chama hicho kutokana na kusababisha mpasuko na makundi.

“Hiki kinaweza kikaathiri chama kuelekea uchaguzi wa Oktoba, kwani hili limeanza kuleta mpasuko hivyo nishauri kamati za nidhamu zichukue hatua. Wabunge na madiwani bado hawajamaliza muda wao, waachwe wakishamaliza kipenga kikipulizwa kila mmoja aingie uwanjani,” amesema.

Kada mwingine, Deogratius Mushi ametahadharisha kuwa, malumbano yanayoendelea yanaweza kusababisha yakajirudia yale-yale ya mwaka 2015 ambao Chadema ilitumia udhaifu uliokuwapo na kuchukua jimbo hilo.

Amesema kwa historia ya jimbo hilo, lenye kanda nne za Kibosho, Uru, Old Moshi na Tambarare, watu wamekuwa wakimchagua mtu kutokana na uwezo wake, hivyo viongozi wanapaswa kuchukua hatua.

Amewaonya wanaokiuka taratibu na kueneza siasa za chuki na makundi.

“Jimbo la Moshi Vijijini linaweza kuchukuliwa tena na upinzani kama mwaka 2015 ambao malumbano haya-haya yalikuwepo kati ya Chami (Dk Cyril Chami) na Mwenyekiti wa Halmashauri aliyekuwapo,  Chadema walichokifanya waliongeza kuni kwenye jiko ili moto uwake zaidi, matokeo yake Dk Chami alipoteza na madiwani wake wakapoteza wote wa CCM, kwa sababu hakukuwa na watu wa kuwaonya Dk Chami na mwenzake,” amesema na kuongeza:

“Kila mmoja alianza kuwa mwamba wakaanza kutishiana ikafika mahali mmoja wao akasusia uchaguzi mwaka 2015 na ikatokea bahati mbaya akapata udiwani yeye pekee na madiwani wote wakakosa.”

Mushi amesema: “Bahati mbaya madiwani wanaomuunga mkono mmoja wa makada ambaye ameanza kujipitisha na kutajwa kuwa na nguvu,  asilimia 90  kwa mtu mwenye akili anayefuatilia mambo ya siasa hawakutokana na uwezo wao, asilimia kubwa ya madiwani hao walichukuliwa kwa sababu CCM ina nguvu hawakupita katika ule mfumo wa ‘competation’ ya kawaida, siyo madiwani wenye nguvu kwenye maeneo yao.”

“Sasa hivi hawa madiwani wanaomuunga mkono kada huyo ambao wameapa kutofanya kazi na mbunge hawana uwezo wa kujipigania wao wenyewe kwenye kata zao. Kitakachotokea sasa kwa sababu Chadema wanatufuatilia kwa karibu wataendelea kutafuta wagombea wazuri kwenye kata wakishapata wagombea wazuri watakuja kumtafuta mgombea mwingine ili hiyo ‘timing yao’ watasubiri ni nani wanayemtaka,” amesema.

Amesema huwezi kuwa mgombea unayepita bila kugawa pesa, kwa hiyo watu wameshagawa pesa, sukari, kwa hiyo wagombea wanaotaka jimbo ambao wanajipitisha asilimia kubwa wanapita wakigawa pesa.

Mushi amesema pamoja na kugawa pesa kumetokea kambi mbili, moja ya Kibosho na nyingine Uru.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *