Makada CCM na kitanzi cha rushwa, lugha chafu kuelekea uchaguzi 2025

Dar es Salaam. Siku sita za ziara ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi mkoani Mara, zimetosha kwa chama hicho kuonyesha msimamo wake kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu, ikiwamo kujitenga na kauli hatari dhidi ya upinzani.

Hayo yote yamejidhihirisha kupitia hotuba na salamu za Dk Nchimbi alizozitoa kwa nyakati tofauti, akiwa kwenye wilaya mbalimbali za Mkoa wa Mara alikofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/25, kuanzia Aprili 22 hadi 26, mwaka huu.

Katika ziara hiyo, mtendaji mkuu huyo wa CCM, alipiga marufuku kwa chama hicho kutumia wimbo wenye maudhui yanayosababisha chuki dhidi ya upinzani, huku akikitaka chama hicho kuwa mfano wa lugha zinazoleta mshikamano wa taifa.

Sambamba na hilo, Dk Nchimbi, ambaye ndiye mgombea mwenza mteule wa Rais Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi wa mwaka huu, alitoa maelekezo kwa wizara na mawaziri mbalimbali ndani ya ziara hiyo, yakiwemo yale yanayopaswa kutekelezwa kabla Bunge halijavunjwa.

Hoja na maelekezo hayo ya mtendaji mkuu huyo wa CCM, yanatazamwa na wataalamu wa siasa kuwa, msingi wake ni hulka na uzoefu alionao kiongozi huyo ndani ya chama hicho.

Kuhusu karipio dhidi ya kauli za chuki kutoka CCM kwenda upinzani, Mwanazuoni wa Historia, Philemon Mtoi, anasema, “mtazamo wake (Dk Nchimbi) unaweza usipendwe na wahafidhina, lakini kwangu mimi ni mtazamo mzuri katika kujenga taifa la watu wamoja na wanaopendana.”

Kauli chafu dhidi ya upinzani

Alipokuwa Shirati wilayani Rorya akizungumza na wananchi, Dk Nchimbi alionyesha kukerwa na nyimbo na kauli mbaya kutoka ndani ya chama hicho dhidi ya upinzani, akisema CCM inapaswa kuwa mfano wa lugha zinazowaunganisha Watanzania.

Kwa sababu chama hicho ndicho kilicholiasisi Taifa, alisema wanachama wake hawapaswi kuwa chanzo cha uchochezi, vurugu na namna yoyote itakayochochea umwagaji damu nchini.

Aliijenga hoja hiyo akirejea sehemu ya wimbo unaosikika katika kipande cha video kilichosambaa mtandaoni kikionyesha wafuasi wa CCM wakiimba wimbo fulani dhidi ya vyama vya upinzani.

Maneno ndani ya wimbo huo yanasikika, “Upinzani ukifa… mimi siwezi kulia… nitawatupa mtoni, wawe chakula cha mamba.”

Baada ya Dk Nchimbi kuwasikilizisha kipande hicho cha video wananchi wa Shirati mkoani Mara aliko kwa ziara yake ya kikazi, hapo hapo alipiga marufuku kisitumike popote dhidi ya vyama vya upinzani.

Katika msisitizo wake kuhusu hilo, Mtendaji Mkuu huyo wa CCM, anasema chama hicho kiwe cha mfano na kwamba wimbo wa namna hiyo, una maneno yanayojenga chuki katika taifa.

“Hayajengi upendo miongoni mwa Watanzania, lazima zitafutwe nyimbo zinazohamasisha upendo bila kusababisha chuki kwa wengine. Wimbo wa namna hii, mimi kama Katibu Mkuu wa CCM napiga marufuku kutumikia dhidi ya upinzani,” alisema.

Akizungumzia hilo, Mwanazuoni wa Historia, Philemon Mtoi alisema kila hoja ya mwanasiasa huyo msingi wake ni hulka na uzoefu wake ndani ya CCM.

Alimtaja Dk Nchimbi kuwa jabali la siasa ndani ya CCM, kuwa amekulia na kulelewa ndani ya chama hicho tawala.

Philemon alisema mwanasiasa huyo siyo mhafidhina, bali ni mtu aliyejijenga katika itikadi za uliberali na hata alipo sasa kumetokana na mapito aliyopitia akiwa ndani ya CCM.

“Ni kiongozi mwenye misimamo isiyotikisika. Ni mtu anayesoma alama za nyakati anayetamani kuona siasa za hoja pasipo kuumizana,” anasema.

Mwanazuoni huyo anasema tangu Dk Nchimbi alipokuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, amekuwa akihamasisha umoja na mshikamano wa kitaifa na aliyetamani kuona tofauti za vyama haziwatenganishi Watanzania.

“Mtazamo wake unaweza usipendwe na wahafidhina na chama, lakini kwangu mimi ni mtazamo mzuri sana katika kujenga taifa la watu wamoja na wanaopendana,” anaeleza.

Hata hivyo, anasema iwapo hoja zake zingekuja na msukumo wa nguvu kuanzia kwenye vikao vya juu vya CCM, kungeshuhudiwa mabadiliko na utengamano wa kisiasa wa hali ya juu nchini. “Kwa siasa za nchi nyingi za Afrika, hasa zile zenye vyama vikongwe vya ukombozi, chama hupenda kuwa na nguvu dhidi ya Serikali na msingi huo umejengwa katika dhana kwamba mkataba, au ilani imeandaliwa na chama na lazima wafuatilie utekelezaji wake.

“Japokuwa kwa Tanzania hatujawahi kuona chama kikimwajibisha mwenyekiti wa chama taifa pale anapokosea,” anasema Philemon.

Kwa upande wa Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Conrad Masabo, anasema ni matamanio yake kuona kauli hiyo inaendana na uwajibishaji wa wanaofanya makosa hayo.

Anasema iwapo watawajibishwa, itaonekana dhahiri kuwa CCM imedhamiria kukomesha kauli na nyimbo mbaya.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kabobe, anasema ni hatua nzuri kwa Dk Nchimbi kukemea wimbo wenye maneno mabaya dhidi ya upinzani.

Hata hivyo, analeza matamanio yake ni kuona mtendaji mkuu huyo wa CCM haishii kwenye kutamka, bali anakwenda mbali zaidi hadi kuwachukulia hatua wahusika.

“Nilitamani aende mbali zaidi kwa wahusika kuchukuliwa hatua, maana kauli kama hizo za kufurahia wenzao wakipatwa majanga, hasa kifo siyo utamaduni wetu.

“Ukisikiliza huo wimbo utagundua kuwa kuna baadhi ya viongozi wa chama walikuwepo ila hawakujali hata kukemea,” anasema.

Anasema ingekuwa bora zaidi iwapo viongozi hao wangechukuliwa hatua hata za kinidhamu kwa kushindwa kuliona hilo na kulikemea.

Anasema Dk Nchimbi ni mmoja, hawezi kuwapo maeneo yote nchini, hivyo ni busara viongozi waliokuwapo wakati wimbo unaimbwa wangechukua hatua hata kabla ya Katibu Mkuu hajafanya hivyo.

“Kukaa kimya kwa viongozi hao kwangu binafsi naona ni kushindwa kuwajibika kwa kukemea maovu. Ikumbukwe kauli kama hizi ziliwahi kutolewa na kiongozi mmojawapo wa UVCCM kule Kagera akijigamba kutaka kupoteza watu ambao kwa maoni yake aliona wanatofautiana na Serikali. Huu sio utawala wa sheria na haukubaliki ndani na nje ya CCM,” anasema.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Kata ya Msigani Dar es Salaam, Reinhad Chikando anasema kauli ya Dk Nchimbi ni muhimu na inalenga kudhihirisha kuwa chama hicho ni kiongozi wa vingine.

“Kwa sababu CCM ni chama kiongozi, kilizaliwa na vingine vikafuata, hakiwezi kujitenga na wajibu wa kuelimisha wengine namna ya kufanya siasa,” anasema.

Wagombea watambuane

Akiwa Nyamongo, wilayani Tarime, Dk Nchimbi aliwataka wabunge wenye nia ya kugombea tena wawatambue watakaoshindana nao katika mchakato wa ndani wa chama hicho na wakiri hadharani kushirikiana iwapo yeyote atapitishwa.

Alisema kitendo hicho, kitathibitisha uhalisia kuwa, uchaguzi si ugomvi, bali ni suala la Watanzania wanamtaka nani awaongoze kwa wakati huo na pengine baadaye wakamchagua mwingine.

Dk Nchimbi alieleza tamanio lake hilo, baada ya Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara kumtaja hadharani mshindani wake, Nikolaus Chichake na kukiri kuwa hata ikitokea amepitishwa na chama hicho, atamshika mkono na kumtembeza katika kata zote za jimbo hilo.

“Leo kwa mara ya kwanza Waitara kawafundisha wana CCM Tanzania nzima. Uchaguzi siyo ugomvi, ni suala la Watanzania wanamtaka nani sasa hivi, wewe pengine watakuona baadaye,” alisema.

Kuhusu hilo, Chikando alisema itasaidia kuvunja vinyongo baada ya mchakato wa kura za maoni ambao aghalabu huisha kwa manung’uniko.

“Mtu akimtaja hadharani mshindani wake na akaahidi kumuunga mkono iwapo atapitishwa, inapunguza vita ya kiuchaguzi, kwa sababu kushindana kimyakimya kunazaa chuki na uadui,” alieleza.

Jukumu kwa wajumbe

Dk Nchimbi pia, aliwataka wajumbe watakaopiga kura za maoni, wachague wagombea kwa kuwasikiliza wananchi wanamtaka nani apitishwe ili wampigie kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa baadaye mwaka huu.

Sababu ya kauli yake hiyo ni kile alichoeleza, ni kiu ya chama hicho katika uchaguzi wa mwaka huu, kupata wagombea watakaokubalika na wananchi na sio wanaopitishwa kwa nguvu ya fedha zao, huku akiwasisitiza wajumbe wafanikishe hilo.

Alisema chama hicho kinatambua kuwepo kwa wabunge wake waliopitishwa na kushinda uchaguzi, lakini wamehudumu kwa miaka mitano bila kurudi majimboni walipo wananchi waliowachagua.

“Kulikuwa na watu ndani ya miaka mitano hawafanyi kazi wanaishia kuhesabu kwamba wajumbe wangapi awape fedha wampitishe, sasa hivi tumewaongezea wajumbe, kama kuwapa fedha, kwa sasa utawapa wangapi,” alisema.

Hata hivyo, Dk Nchimbi alisema pamoja maoni ya mjumbe binafsi, siku ya kura za maoni, wananchi wasiogope kuwaambia wanataka nani akapigiwe kura ili apitishwe kwa sababu ndiye hitaji lao.

“Waambieni bila woga kwamba tuleteeni mtu fulani tutampa kura zote,” alisema.

Kuhusu hilo, Philemon anasema hiyo ndio hoja ya msingi ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan na amekuwa akizungumza wakati wote.

“Rais Samia anaonyesha hataki kupata wabunge wasiokuwa na msaada kwake, anataka kupata wabunge wenye uwezo wa kumsaidia katika shughuli za Serikali,” anasema.

Kwa mtazamo wa mwanazuoni huyo, katika uchaguzi wa mwaka huu huenda wakashuhudiwa wabunge wengi wa CCM ni wale wenye elimu nzuri na watii kwa Serikali.

“Dunia imebadilika na wao wameamua kuja na mchakato ambao utawapa wanachotaka,” anasema.

Kuhusu hilo, Dk Masabo anasema pamoja na mabadiliko ya kikanuni yaliyofanywa na chama hicho, muhimu kutengeneze utaratibu wa kuimarisha mamlaka itakayochuja wagombea. “Hiyo mamlaka inapaswa kuwa na wajumbe wanaokubalika na kuaminika kutoka miongoni mwa wana CCM. Hawa ndio wanaweza kuleta wagombea watakaomudu ushindani,” anasema.

Kwa upande wa Dk Kabobe, anasema kunaweza kuwa na mengi katika hilo, lakini muhimu linaloweza kukinufaisha chama ni kuhakikisha kinapitisha wagombea wanaochagulika.

“Kuchagulika kuna maana pana, ikiwemo wagombea wanaokubalika kwa wapigakura, wagombea wawajibikaji, wasio walarushwa na wenye kubeba dhamana ya chama na wanapiga kura,” anasema Dk Kabobe.

Dinwa, Wasira watia neno

Mapema wiki hii, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohammed Said Mohammed (Dimwa) kwa nyakati tofauti ameonya wanachama na makada wa chama hicho  kutojihusisha na vitendo vya rushwa wakati wa mchakato wa kuelekea uchaguzi Mkuu.

Dk Dimwa amesema chama kimeandaa mkakati kamambe kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi (Zaeca).

Alikuwa akizungumza na Kamati za Siasa za siasa Mkoa wa Mjini Kichama ikiwa ni muendelezo wa ziara ya kukagua uhai wa chama na kuelezea mabadiliko na namna ya kupata wagombea na kura za maoni.

Alisema chama kimeanza kuweka watu wa ZAECA na watu wa maadili katika kila jimbo kwa lengo la kuzuia rushwa.

Hivyo aliwaonya wanachama ambao wana nia ya kugombea nafasi mbali mbali kujiepusha na vitendo hivyo na kwani hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

“Mimi nina nisimamo thabiti, Mungu amenijaalia nina chukia sana rushwa, rushwa katika uchaguzi ni mbaya sana hivyo mtu wala asije mbele yangu kunipa rushwa,”alisema

Alisema atawashughulikia viongozi wote wasio  waadilifu na wenye nia ya kula rushwa kwa lengo la kuwakandamiza watu wengine.

“Tukiwa chama kinachoongoza nchi, lazima tupigane na rushwa kwenye chaguzi zetu lengo ni moja tu la kuwapata viongozi makini watakao chagulia kwa haki bila ya upendeleo,” alisema Dimwa.

Naye Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira aliwahi kuwakemea wabunge wa viti maalumu akiwataka waache kuwahonga wanawake kwa kuwagawia majiko ya gesi na vitenge ili wapate uongozi.

Alisisitiza kwamba chama hicho kimedhamiria kujenga maadili katika kupata viongozi watakaokwenda kuwatumikia wananchi.

Wasira aliyasema hayo Machi 27, 2025 wakati akizungumza kwenye mkutano wa ndani na wanachama wa chama hicho Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga katika ziara yake ya kukagua utekelezaji wa ilani ya chama hicho.

Alisema anajua wabunge hao wanachaguliwa na watu wachache lakini lazima wajue rushwa ni adui wa haki na akasisitiza kwamba wanataka wananchi wawe na mamlaka na Bunge. “Akina mama wa viti maalumu muache kugawa mitungi ya gesi na vitenge, mitungi yenyewe mnawapa akina mama gesi, ikiisha inageuzwa kuwa ‘furniture’, wanakalia, maana hata hela ya kununulia gesi hawana, haya ndiyo mambo yanayoitwa maadili?

Alisema CCM inataka viongozi ambao wakienda bungeni, wawe wametumwa na wananchi na wakayaseme yale waliyowatuma.

Alisema rushwa inapofusha wajumbe, chama kinataka kamati za siasa kuleta wagombea wenye sifa na wasibabaike kuwawajibika makada wenye kutaka kugawa fedha ili wachaguliwe kuwa viongozi.

“Tumesema katika ahadi yetu tutasema ukweli daima, rushwa ni adui ya haki na mkono unanyoosha juu, sitapokea wala kutoa, ukishusha tu unapokea ahadi yako inakomea hewani maana yake unaachana na Mungu unapokea rushwa,” alisema Wasira.

Mawaziri kitanzini

Katika ziara hiyo, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alijikuta akipokea maelekezo matatu kwa nyakati tofauti.

Alielekezwa na Dk Nchimbi kuhakikisha anatoa fedha kabla Bunge halijavunjwa kumlipa mkandarasi anayetengeneza jenereta katika Hospitali ya Rufaa ya Mwalimu Julius Nyerere ili akamilishe kazi haraka.

Pia, Waziri huyo alielekezwa ndani ya siku 14 kuhakikisha anatoa fedha kukamilisha malipo ya fidia kwa wananchi waliopisha eneo la ushoroba wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti katika Wilaya ya Bunda.

Maelekezo kama hayo, aliyatoa pia kuhusu kutolewa kwa fedha za kukamilisha malipo ya mkandarasi wa Uwanja wa Ndege Musoma ili ukamilike haraka kama ilivyopangwa.

Dk Nchimbi pia, alimwelekeza Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi kushirikiana na Mkoa wa Mara kuona namna watakavyoharakisha tathmini kwa ajili ya wananchi waliopisha eneo hilo la ushoroba.

Kwa upande wa Wizara ya Maji, alielekeza itoe kipaumbele kwa kufanikisha kukamilika kwa mradi wa maji Rorya-Tarime.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *