Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
MSIMAMO wa Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wa kususia uchaguzi mkuu umezua mjadala mkali ndani ya chama, baada ya baadhi ya makada wake ambao pia ni watia nia wa Ubunge kujitokeza hadharani kuupinga, wakisema unaweka chama chao katika hatari kisiasa.
Wanachama hao, wakiongozwa na Jonh Mrema, Catherine Ruge, Julius Mwita, Susan Kiwanga, Grace Sindato Kiwelu, Daniel Naftari Ngogo, Henry Kilewo na Francis Kishabi, wamesema kuwa kuzuia uchaguzi mkuu ni hatari kwa mustakabali wa chama na kinachohitajika ni kushiriki ili kuleta mabadiliko ndani ya mfumo wa uchaguzi.
“Sisi tunaunga mkono juhudi za kutaka mabadiliko, ila lazima tujue kuwa si kazi rahisi kuzuia uchaguzi mkuu tukiwa nje ya mfumo wa uchaguzi wenyewe kama anavyojaribu kusema Lissu. Njia pekee ya kuleta mabadiliko ni kushiriki na kuhakikisha tunaingiza wagombea katika uchaguzi,” ilisema taarifa yao, iliyosainiwa na wanachama 55 waliotia nia ya kuwania nafasi ya ubunge kupitia Chadema.
Kwa mujibu wa makada hao, tamko la Lissu la “No Reforms, No Elections” halina tija kwa chama, na badala yake linaweza kuwa na athari mbaya kwa mustakabali wa Chadema.
Hata hivyo, katika kujibu wakosoaji wake, Lissu amesema kuwa msimamo wa chama ni wazi, na unalenga kuhakikisha Tanzania inapata uchaguzi huru na wa haki kabla ya kushiriki katika mchakato wa uchaguzi.
“Wanaosema kuwa kususia uchaguzi hakutasaidia wanapaswa kuelewa kuwa hatuwezi kuingia kwenye uchaguzi usio wa haki na unaoendelea kuwabeba walioko madarakani. Historia imetufundisha kuwa bila mageuzi ya mfumo wa uchaguzi, upinzani hauna nafasi ya kushinda. Hili si suala la utashi binafsi, bali ni msimamo wa chama kwa maslahi ya taifa,” alisema Lissu.
Wachambuzi wa siasa wameeleza kuwa mgawanyiko huu ndani ya Chadema unaweza kuwa na athari kubwa kwa uimara wa chama kuelekea uchaguzi mkuu.
Kwa sasa, bado haijafahamika kama uongozi wa juu wa Chadema utaandaa kikao cha ndani ili kutafuta mwafaka kati ya pande mbili au kama msimamo wa kususia uchaguzi utaendelea kuwa thabiti bila mabadiliko.