Makada 55 Chadema wajilipua na waraka kupinga kuzuia uchaguzi

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinaonekana kukumbwa na mgawanyiko kuhusu msimamo wake wa No Reforms, No Election.

Wakati kampeni hiyo ikiendelea katika Kanda ya Kusini baada ya kuhitimishwa Kanda ya Nyasa, baadhi ya makada na viongozi wa chama hicho wanatofautiana nayo, licha ya kwamba uamuzi huo ulifikiwa na vikao vya juu na kuridhiwa rasmi.

Katikati ya sakata hilo, taarifa zinadai baadhi ya makada wameanza kuchukuliwa hatua, na Katibu wa sekretarieti, Julius Mwita ameondolewa kwenye wadhifa huo kutokana na kudaiwa kwenda kinyume.

 Mbali na hilo, kwa sasa ndani ya chama hicho kuna fukuto baada ya kundi la watia nia wanaotaka kugombea nafasi za ubunge kupitia Chadema, maarufu kama G55, kupinga uamuzi wa kutoshiriki uchaguzi.

Hata hivyo, kwa upande mwingine wanaonekana kuunga mkono hatua ya chama hicho kupigania mageuzi kwenye mifumo ya uchaguzi, lakini  hawakubaliani na mpango wa kususia (kuzuia) uchaguzi.

Watia nia hao ambao ndani yake wapo waliowahi kuwa wabunge, madiwani na viongozi kwa nyakati tofauti ndani ya Chadema, wanataka chama hicho kishiriki kwenye uchaguzi na kuweka wagombea kwenye nafasi zote.

Tayari watia nia hao wamewasilisha waraka kwa Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kueleza msimamo wao kupinga no election (hakuna uchaguzi) huku wakitoa sababu tisa za kutetea uamuzi huo.

Kwa siku kadhaa sasa kumekuwa na ujumbe z

Unaotembea kwenye makundi sogozi ya WhatsApp pamoja na mitandao ya kijamii, kuwa wana mtandao wa  G55 wenye msimamo wao huo.

Miongoni mwa sababu za wana mtandao wa G55 wanaamini kwamba, mkakati wa Chadema kuzuia uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 hauwezi kufanikiwa kwa kuwa ni takwa la kikatiba.

Katiba ya Jmahuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 65 inaelekeza Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani ufanyike kila baada ya miaka mitano. Ibara hiyo ya 65 (1) inasema bila ya kuathri masharti mengneyo ya Katiba hii, maisha ya kila Bunge yatakuwa ni muda wa miaka mitano.

Kutokana na hilo, wana mtandao hao wanaamini kuwa uamuzi wa Chadema kutoshiriki uchaguzi huo utawafanya makada wake wenye ndoto za kuwa wabunge na madiwani kuikosa fursa hiyo.

Pia, uamuzi huo utaiweka Chadema nje ya siasa za ushindani kuwa wawakilishi wake watakosa sauti ndani ya vyombo vya maamuzi, hivyo kuendesha harakati nje ya mfumo sahihi ambazo hazitakuwa na tija kwa ustawi wa Tanzania.

Na badala yake kupitia waraka huo ulitiwa saini na wana mtandao hao, wamependekeza mbinu za kulinda kura na njia mbalimbali za kuzuia hujuma zinazofanywa kwenye vituo vya kupigia kura zidhibitiwe kwa nguvu zote.

Hata hivyo, wakati makada hao wa Chadema wakija na mpango huo, tayari viongozi wakuu wa chama hicho wameketi na watiania wote wa ubunge na udiwani na kusisitiza utekelezaji wa kampeni ya Bila mageuzi, hakuna uchaguzi uko pale pale.

Pia, wamewapa makada hao majukumu ya kutafuta saini milioni 15 za Watanzania nchi nzima kama sehemu ya mkakati wa kupinga kufanyika kwa uchaguzi mkuu hapo baadaye mwezi Oktoba, 2025.

Katika kikao hicho kilichofanyika Alhamisi Aprili 3, 2025 kwenye ofisi za makao makuu ya chama hicho, Mikocheni jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu alisema kwa kutorishiki uchaguzi huo, chama hicho hakitakufa.

Lissu alisema kwa mwanachama wa Chadema anayetaka ubunge kwa umakini, basi aungane na chama hicho katika safari ya mabadiliko, akisisitiza kama kuna mtu anafirikia kuwa mbunge Oktoba au Novemba, 2025, asahau hilo katika mazingira ya sasa.

Naibu Katibu Mkuu Chadema- Bara, Aman Golugwa ameliambia Mwananchi leo Ijumaa Aprili 5, 2025 kuwa tayari wameona waraka wa G55 wenye kichwa cha habari ‘Ushauri kwa chama’ uliowasilishwa katika Ofisi ya Katibu Mkuu, akisema hauna mambo magumu yote yanajibika.

Katika waraka huo wenye saini za wana mtandao hao wakiwemo viongozi wa mikoa, pamoja na kuunga mkono hoja ya mageuzi ya kisheria hasa za uchaguzi, wamesema ni vema chama hicho kishiriki uchaguzi huo.

Mbali na hilo, Mwananchi linafahamu kuwa wana mtanadao wa G55 ni sehemu tu, kwani wapo makada wengine wanaotaka Chadema ishiriki uchaguzi, lakini hawataki kuwa mstari wa mbele kwa sasa.

“Ni rahisi kwa wagombea kuhamasisha na kuongeza wananchi kuzuia uchaguzi katika vituo mahsusi vya uchaguzi, katika kata au majimbo yanayoelekea kufanyiwa hujuma kuliko kuzuia uchaguzi huku tukiwa nje ya uchaguzi wenyewe,” wamesema kupitia waraka huo.

Hoja nyingine ni kile walichoeleza kuwa, dhana ya “No Reforms, No Elections”, ilianza Januari mwaka 2020 na haikulenga kuzuia uchaguzi, bali ililenga kuhamasisha uungwaji mkono wa kudai mageuzi.

Kupitia waraka huo, wamesema kwa muda mfupi uliosalia, hawaoni mafanikio ya kuzuia uchaguzi kwa kuwa michakato kadhaa imeshapita na sasa umefikia mgawanyo wa majimbo.

Wameandika waraka huo, wakirejea Ibara ya 4 ya Katiba ya chama hicho inayosema madhumuni ya kushika dola, hivyo kushika dola ni sharti la msingi la kikatiba.

Pia, wamesema katiba hiyo hiyo Ibara ya 5.2.2 inaeleza kuchaguliwa na kuwakilisha chama ni moja ya masharti ya kikatiba, hivyo kwenda kinyume ni kuipinga katiba ya chama.

Sababu nyingine, wamesema hakuna chama kingine kinachounga mkono ajenda hiyo na kwamba, vipo ambavyo vinaendelea kujiandaa huku vikishinikiza mageuzi.

“Ukiondoa chama chetu, mpaka sasa hakuna chama kingine cha siasa kinachounga mkono mpango wa kuzuia uchaguzi ikiwa mageuezi hayatapatikana bali vinandelea kujipanga kusimamisha wagombea.

“Kinyume chake, kuna chama kimoja tu cha upinzani ambacho kinapigania mageuzi lakini huku kikiendelea kujipanga kushiriki uchaguzi. Vyama vingine vimeendelea kutangaza nia zao za kushiriki uchaguzi,” wamesema.

Hoja ni nyingine ya G55 ni kwamba viongozi wa dini na madhehebu yenye waumini wengi hapa nchini, tayari wamehimiza na wanaendelea kuelimisha na kuhamasisha waumini wao kwenda kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura kwa ajili ya kushiriki uchaguzi.

“Hali hii inaashiria kuwa ni ama chama chetu kimechelewa au tayari kimekwama kupata uungwaji mkono wa wadau muhimu katika mpango wa kuepuka uchaguzi usio na mageuzi,” wamesema.

Kwa mujibu wa G55, katika uchunguzi na uchambuzi wao unaony9esha wadau wengi wa demokrasia wanaunga mkono madai ya mageuzi, lakini hawaungi mkono mpango wa .

“Hali hiyo kwao inatafsiriwa kuwa ni karibu sawa na kufanya uasi au kuvunja katiba na sheria zilizopo licha ya ubaya wake. Kwa maneno mengine, msisitizo wa kuzuia uchaguzi unaathiri au kupunguza kasi ya uungwaji mkono katika madai ya msingi ya mageuzi,” umeeleza waraka huo.

Athari za kutoshiri uchaguzi

Katika waraka huo, G55 imeanisha athari zitakazoweza kujitokeza endapo Chadema haitashiriki uchaguzi ikiwemo kuondokewa au kupoteza viongozi na wanachama wenye nia ya kuwania urais, ubunge, udiwani pamoja na nafasi za ubunge wa maalumu.

“Chama kitapoteza mvuto kwa umma, kitadhalilishwa kwa propaganda na hata kudhohofika, hadi sasa chama kiko vipande viwili vinavyosigana kuhusu jambo hili. Ikitokea tukashindwa kushiriki uchaguzi, mpasuko huu utakuwa na athari nyingi na mbaya zaidi,” imesema sehemu ya waraka huo.

Kutokana na hilo, G55 wameshauri Chadema kuingia katika uchaguzi, wakati huohuo kikiendelea kuongeza kasi na nguvu ya kudai mabadiliko ya chaguzi huru na zenye kuaminika.

“Kwa kuzingatia msingi wote huo, sisi tuliokuwa wagombea ubunge 2020 na watiania wa ubunge 2025, tunakishauri chama chetu kiruhusu kuanza mara moja kwa maandalizi ya chini kwa chini ya kujipanga kushiriki uchaguzi,” wamesema.

Ulichosema uongozi

Katika majibu yake kuhusu waraka huo, Golugwa amesema hakuna jambo lisilojibika katika waraka wa G55, ndio maana Chadema iliwaita watia nia wote kuwaeleza kuhusu kampeni yake hiyo na majibu ya hoja ya waraka huo yalitolewa.

“Hakukuwa na hoja ngumu, cha kusema kuwa waraka ni ngumu… mambo yote yalijibika na tulitoa fursa kwa watia nia wote. Hata ambaye hakuelewa no reforms, no election alielimishwa, kwa sababu tupo katika awamu ya kutoa elimu, watu wote hawawezi kuelewa kwa haraka.

“Tuna siku 47 za kuelimisha ili kuwa na watu wanaounga mkono kitu wanachokielewa, hatutaki ‘misukule’ wanaounga mkono kitu wasichokielewa.

“Kitu ambacho tutakuwa wakali ni kupinga misimamo iliyopitishwa na chama ndio dhana tunayoiona kwenye hili kundi la G55,” amesema Golugwa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *