Mwanza. Wanachama na viongozi 20 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Viktoria wamekamatwa na Polisi wakiwa njiani kwenda kuonana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda.
Makada hao akiwemo Katibu wa Chadema Kanda ya Viktoria, Zakaria Obadi na wenzake wamekamatwa leo Jumatano, Februari 26, 2025 nje ya ofisi za mkuu wa mkoa na kuwekwa mahabusu kwa dakika kadhaa kisha kuachiwa kwa dhamana.
Habari za kuaminika zinaeleza kuwa makada na viongozi hao walikuwa kwenye harakati za kumuona Mtanda ili kufahamu hatima ya Katibu wa Baraza la Vijana wa chama hicho (Bavicha) Mkoa wa Mwanza, Amani Manengelo aliyetoweka tangu Februari 14, 2025 akiwa wilayani Misungwi.

Baadhi ya wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiwa wameongozana na askari kwenda kituo kikuu cha Polisi jijini Mwanza kabla hawajaachiwa. Picha na Damian Masyenene
Akizungumzia kukamatwa kwa makada hao, Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema, Salma Kasanzu amesema wanachama hao walikuwa sehemu ya ujumbe wa ufuatiliaji alipo Manengelo na walikwenda kumuona Mtanda, lakini wakakamatwa kabla ya kumuona bila kuelezwa sababu.
“Tulikuja leo hapa na tulikuwa na miadi na mkuu wa mkoa ili kupata mrejesho wa kinachoendelea kuhusu mahali alipo mwenzetu, lakini tumefika hapa wenzetu wamekamatwa na Polisi mpaka sasa hivi wako ndani,” amesema Salma
Salma, ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Wanawake Chadema Mkoa wa Mwanza (Bawacha), amesema wakati tukio hilo linatokea Mtanda alikuwa anawasubiri kikaoni.
“Tunasubiri wenzetu watoke huko ndani twende kwenye kikao, tukifika huko tutajua tutafanya nini kwa sababu huu ni uonevu. Polisi wanatakiwa kufuata utaratibu kwani, hawa viongozi wamekuja kwenye kikao sasa kwa nini wakamatwe,” amesema Salma.

Baadhi ya wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiwa wameongozana na askari kwenda kituo kikuu cha Polisi jijini Mwanza kabla hawajaachiwa. Picha na Damian Masyenene
Mmoja wa wanachama waliofika kuwatoa wenzao waliokamatwa, Audax Kweyamba amesema; “Watu ambao wanahitaji kujua mwenzao yuko wapi, lakini mnawatisha na kuwakamata ni jambo ambalo linatisha na linasikitisha.
“Tumeamua kuja kwa mkuu wa mkoa kwa sababu kila wakati tunaambiwa uchunguzi unaendelea, lengo letu ni kwenda kufahamu huu uchunguzi umefika wapi tunahitaji kuendelea kutia shinikizo.”
Hata hivyo, takribani saa moja baada ya makada hao kukamatwa na kuwekwa ndani, waliachiwa na kwenda ofisini kwa Mtanda kuendelea na kikao. Jitihada za kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Wilbroad Mutafungwa kuzungumzia kukamatwa kwa makada hao zinaendelea.
Endelea kufuatilia Mwananchi