Majogoro kutimkia Orlando Pirates

KIUNGO wa Chippa United, Mtanzania Baraka Majogoro inaelezwa hayupo kwenye kikosi hicho kwa wiki ya tatu sasa, huku taarifa zikieleza yupo kwenye hatua za mwisho kujiunga na Orlando Pirates ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini.

Huu ulikuwa msimu wa pili kwa kiungo huyo fundi kuichezea Chippa United ambayo msimu wake wa kwanza alicheza mechi 16 na msimu huu akikiwasha kwenye michezo minane.

Majogoro ndiye Mtanzania pekee aliyesalia kwenye ligi hiyo baada ya Gadiel Michael aliyekuwa anacheza naye timu moja kutimkia Singida Black Stars na Abdi Banda aliyekuwa anakipiga Baroka kusajiliwa Dodoma Jiji.

Chanzo kimoja kililiambia Mwanaspoti nyota huyo ambaye awali tetesi zilisambaa mitandaoni ameondolewa kwenye kikosi hicho atajiunga na timu hiyo bure bila ya ada ya uhamisho kama dili hilo litafanikiwa.

“Mawasiliano kati ya Majogoro na uongozi wa Orlando yamekuwa na matumaini na mazungumzo yalikwenda vizuri Jumanne iliyopita, ninachojua atajiunga bure kwa sababu Chippa imemvunjia mkataba,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Nafikiri uamuzi wa mwisho upo mikononi mwa Baraka, kwani Riveiro tayari ameidhinisha usajili wake na anatamani kuwa na kiungo huyo ambaye ana nidhamu kubwa ya ukabaji uwanjani.”

Tulipomtafuta kiungo huyo wa zamani wa KMC juu ya ishu hiyo hakupatikana na wala hakujibu ujumbe wa ‘Whatsapp’ aliotumiwa.

Mara ya mwisho Majogoro kucheza ni Desemba 29 akitumika dakika 56 dhidi ya Kaizer Chiefs timu hiyo ilipochapwa bao 1-0 na tangu hapo hakuwa sehemu ya mchezo huo.