Majina ajira mpya serikalini haya hapa, walimu ‘kibao’

Dar es Salaam. Sekretarieti ya ajira imetangaza majina 122 kuingia katika ajira mpya serikalini jana Februari Mosi 2025.

Kwa mujibu wa tangazo hilo lililochapishwa katika tovuti ya sektretarieti ya ajira, 95 ni walimu wa kada mbalimbali, ambayo ni sawa na asilimia 77.8 ya walioitwa kazini.

Walimu hao wamepangiwa katika halmashauri tatu kama ifuatavyo; Halmashauri ya Manispaa Temeke, Halmashauri ya Mji Kibaha na Halmashauri ya Manispaa Kinondoni.

Upande wa kada zao, walimu hao wapya walioajiriwa ni kama ifuatavyo: Mwalimu daraja la III B fizikia (14), mwalimu daraja la III B – hisabati (27), mwalimu daraja la III B  biashara (4), mwalimu daraja la III C fizikia (8), mwalimu daraja la III C hisabati (28).

Kada nyingine ni: Mwalimu daraja la III C sanaa (2) na mwalimu daraja la III C biashara (12).

Taarifa hiyo imeeleza kuwa: “Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma anapenda kuwataarifu waombaji kazi wa nafasi mbalimbali waliofanya usaili kati ya Agosti 14, 2024 na Januari 17, 2025 kuwa matokeo ya waombaji kazi waliofaulu usaili huo ni kama yalivyoorodheshwa katika tangazo hili.

“Orodha ya majina haya pia inajumuisha baadhi ya wasailiwa waliokuwa kwenye kanzidata kwa kada mbalimbali ambao wamepangiwa vituo vya kazi baada ya nafasi kupatikana.”

Tangazo hilo limeeleza kuwa waombaji waliofaulu usaili wanatakiwa kuchukua barua za kupangiwa kituo cha kazi Ofisi za Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma zilizopo Chuo Kikuu Dodoma (UDOM) kwenye majengo ya Dk Asha Rose Migiro, masjala ya wazi ndani ya siku saba kutoka tarehe ya tangazo hilo, baada ya hapo barua ambazo hazitachukuliwa na wahusika zitatumwa kupitia anuani zao za posta.