Majibu ya mifumo ya anga ya Iran ndiyo sababu ya kusikika sauti za miripuko pembeni mwa Tehran

Duru za kiusalama za Iran zimetangaza kuwa, sauti kubwa za miripuko zilizosikika alfajiri ya leo Jumamosi hapa Tehran zimetokana na majibu ya mifumo ya ulinzi wa anga ya Iran kupiga silaha zilizorushwa dhidi ya baadhi ya maeneo ya pembeni mwa Tehran.

Shirika la habari la IRNA limezinukuu duru za kiusalama za Iran zikisema leo alfajiri kwamba milio ya miripuko iliyosikika alfajiri ya leo hapa Tehran imetokana na radiamali na majibu ya mifumo ya ulinzi wa anga ya Iran ambayo imefanikiwa kuyalinda vizuri maeneo yaliyolengwa na mashambulizi ya adui. 

Shirika hilo limesema kuwa hakukuwa na taarifa zozote za kupigwa sehemu yoyote wala kuhitajika misaada ya afya kama ambavyo hadi wakati tunaandaa habari hii, viwanja vya ndege vya Mehrabad na Imam Khomeini vya hapa Tehran vilikuwa vinaendelea kufanya kazi zao kama kawaida. 

Shirika la habari la Tasnim limeripoti leo asubuhi kwamba hali katika viwanja vya ndege vya kimataifa vya Imam Khomeini na Mehrabad vinaendelea kufanya kazi kama kawaida na hakuna kitu chochote kisicho cha kawaida kilichotokea kwenye viwanja hivyo.

Hali katika mji wa Tehran inaendelea kama kawaida. Ofisi zote ziko wazi, maskuli, vyuo vikuu, viwanja vya michezo na sehemu nyingine zote zinaendelea kama kawaida na shughuli zao za kila siku.

Shirika hilo limetangaza pia kuwa, hakuna kombora lolote lililopiga sehemu fulani au madhara yaliyotokea kwenye vituo vya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH hapa Tehran na kwamba picha zote zinazoenezwa kwenye mitandao ya kijamii ni za matukio ya zamani.

Hata vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni wa Israel vimekiri uwezo mkubwa wa Iran wa kujilinda na mashambulizi ya anga.

Duru za kuaminika zimeliambia shirika la habari la Tasnim kwamba kama ilivyotangaza huko nyuma, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kujibu uvamizi wowote ule wa Israel dhidi yake. 

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Iran ina haki ya kujibu uvamizi wowote na hapana shaka hata chembe kwamba Israel itapata jibu la ujuba wake wowote ule.