Maji ya kunywa yalivyomponza Diarra kufungwa bao la mbali

Baadhi ya mashabiki wakiwemo wa Yanga jana walimpa Selemani Bwenzi fedha baada ya kufunga bao safi wakati timu yake ya KenGold ikilala kwenye Uwanja wa KMC Complex, huku akisema kipa huyo alikuwa akiomba maji.

Kiungo huyo alifanya maajabu baada ya kufunga kwa shuti kali kutoka katikati ya uwanja  kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara ambao Yanga ilishinda mabao 6-1.

Hili ndiyo bao ambalo hadi sasa limefungwa kwa umbali mrefu zaidi lakini likiwa bao la tano anafungwa kipa wa Yanga Djigui Diarra kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu.

Baada ya bao hilo, Bwenzi amesema aliyatumia vyema makosa aliyokuwa anayafanya kipa huyo wa Yanga na yeye kila siku amekuwa ni mtu wa kujaribu.

“Hii ni moja ya jambo ambalo nimekuwa nikijifunza mazoezini. Diarra ni kipa mzuri lakini kama walivyo wazuri wengine wanachangamoto zao, ndiyo nilichokifanya niliangalia madhaifu yake nikayatumia unajua pale alikuwa mbele sana, ni goli zuri lakini makosa yake ndiyo yamechangia.

“Mimi kama mchezaji nilipokuwa naagalia niliona kama vile alikuwa anaomba maji, hivyo alishaondoka langoni kwake ndiyo maana nikaamua kujaribu na kweli nimefanikiwa kufunga,” alisema Bwenzi ambaye baada ya mechi baadhi ya mashabiki walionekana kumpongeza wakiwemo waliovaa jezi za Yanga.

Tayari mashabiki wameanza kugawanyika kutokana na ubora wa bao hilo baadhi wakiamini kuwa linaweza kuwa bora kwa msimu huu, huku wengine wakiamini kutokuwa makini  kwa Diarra kumechangia kwa sehemu kubwa staa huyo kufunga bao hilo ambalo ni la 12 kwa KenGod msimu huu ikiwa inashika nafasi ya mwisho kwenye msimamo na pointi sita.

Yanga ambayo hadi sasa imeruhusu mabao saba kwenye Ligi Kuu Bara ikiwa inashika nafasi ya pili kwa timu iliyofungwa mabao machache baada ya Simba ambayo imefungwa matano, imekuwa na kasi nzuri ya kufunga mabao ambapo hadi sasa ndiyo inaongoza kwa kupachika mengi ikiwa imeshafunga mabao 42 ikifuatiwa na Simba iliyofunga 34 na leo inacheza dhidi ya Fountain Gate kwenye Uwanja wa Kwaraa Manyara.