Maji safi saa 24 bado kitendawili, wananchi wapaza sauti

 Dar es Salaam.  Wakati kiwango cha upatikanaji maji kikitakiwa kuwa saa 24 kwa siku, ripoti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) inaonyesha kuwa, ni mamlaka za maji nane pekee kati ya 82 ndiyo zimeweza kusimamia kiwango hicho.

Mbali na hizo, mamlaka sita za maji nchini za Rombo (Kilimanjaro), Kondoa (Dodoma), Liwale (Lindi), Kibaya (Manyara), Songe (Tanga) na Ruangwa (Lindi) nazo zimetoa maji kwa wastani wa saa tano pekee kwa siku katika mwaka 2023/24, ikiwa ni pungufu wa saa 19 ili kufikisha muda unaotakiwa.

Ripoti ya Taarifa ya Utendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa Mwaka wa Fedha 2023/24  iliyotolewa Machi 19, 2025 na Ewura inaonyesha kuwa, mbali na halmashauri hizo nane, nyingine zilikuwa zikiwapatia wananchi maji kwa vipindi tofauti jambo lililosababisha malalamiko kwa wananchi.

Hili linaonekana wakati ambao wastani wa upatikanaji wa maji nchini ni saa 14 kati ya 24 zinazohitajika, huku sababu mbalimbali zikitajwa kuchangia hali hiyo ikiwamo upotevu wa maji kabla ya kufika kwa wananchi.

Eneo kama Rombo ambalo wananchi wanapata maji kwa saa chache, pia linatajwa kushika namba moja kati ya sehemu zinazoongoza kwa maji yake mengi kupotea kabla hayajafika kwa wananchi.

Wakizungumza na Mwananchi leo Jumanne Machi 26, 2025 baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Rombo wamesema bado changamoto ya upatikanaji wa maji ni kubwa kutokana na baadhi ya maeneo kuwa na mgawo wa maji.

Mmoja wa wananchi wa wilaya hiyo, Josephine Tesha amesema licha ya Serikali kufanya jitihada za kuondoa changamoto ya maji wilayani humo, bado wanapata maji kwa mgawo na imekuwa ni changamoto.

Anna Kawau, mkazi wa Kijiji cha Nayeme wilayani humo, amesema kwa jitihada zinazofanywa na Serikali hivi sasa wana matumaini makubwa ya upatikanaji wa maji katika maeneo yao.

“Tulikuwa na changamoto kubwa ya maji na tulikuwa tukifuata maji umbali mrefu, lakini sasa hivi angalau tunapata maji licha ya kwamba tunayapata kwa mgawo lakini tuna afadhali,” amesema mkazi huyo.

Amate Kavishe amesema kwa miaka ya nyuma changamoto ya maji ilikuwa ni kubwa kuliko sasa.

Mkazi huyo wa Usseri amesema wakati mwingine watu walikuwa wakiamka saa nane za usiku kwenda kuweka foleni ya maji jambo ambalo limepungua na kuishukuru Serikali kwa jitihada inayofanya ya kuhakikisha wananchi wanapata maji ya kutosha.

Mbali na Rombo maeneo mengine yenye upotevu mkubwa wa maji ni Handeni (Tanga) asilimia 69, Mugango Kiabakari (Mara) asilimia 68, Ifakara (Morogoro) asilimia 56 na Kilindoni (Pwani) asilimia 55.

Maeneo yana upotevu wa maji kwa asilimia chache ni Maganzo (Shinyanga) asilimia 4, Nzega (Tabora) asilimia 6, Kashwasa (Shinyanga) asilimia 11, Biharamulo (Kagera) asilimia 12 na Monduli (Arusha) asilimia 13.

Kwa wastani kiwango cha upotevu maji katika mwaka wa fedha 2023/24 kilikuwa asilimia 36.8 sawa na Sh114.12 bilioni.

Kiwango cha upotevu wa maji ni juu ya kiwango cha huduma kinachokubalika cha asilimia 20.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo kiwango cha upotevu maji kilichokuwapo katika kipindi husika ni pungufu ikilinganishwa na asilimia 37.2 katika mwaka wa fedha 2022/23

Malalamiko ya kukosa maji

Lakini, si maeneo yaliyo na upotevu mkubwa wa maji pekee ndiyo kuna malalamiko hayo bali hadi sehemu kama Dar es Salaam kuna malalamiko ya kukosekana kwa huduma ya maji ya uhakika.

Mama Herieth mkazi wa Salasala jijini Dar es Salaam alipozungumza na Mwananchi jana amesema ni takribani mwezi mmoja sasa hawapati huduma ya maji.

“Mimi nafuga kuku, mahitaji yangu ya maji ni makubwa nalazimika kununua maji kwa watu wanaotembeza, nanunua lita 10,000 kwa siku kwa Sh130,000, tunaomba Serikali itatue kero hii tunaumia,”amesema.

Hali kama hiyo inaelezwa pia na Alwiya James mkazi wa Sinza E (Ubungo)  akisema siku zote wanakabiliwa na kero ya maji na wakilalamika zaidi hupata kidogo kwa saa chache.

“Dumu moja la maji tunanunua Sh500, kwa wiki natumia maji ya Sh30,000 hadi Sh35,000  tofauti na maji ya Dawasa ambayo kwa mwezi nilikuwa nalipia Sh65,000 kwa mwezi,” amesema.

Eva Sambo, mkazi wa Kinyerezi Mbuyuni (Ilala) amesema ni miaka mitatu sasa hawajawahi kushuhudia maji ya bomba licha ya kwamba wana miundombinu yote ya maji.

“Sio kwamba hatuna mabomba ya maji hapana, yapo lakini hakuna maji kabisa eneo walonaita kwa Smart tunanunua lita 1,000 (sawa na ndoo 50 zenye ujazo wa lita 20) kwa Sh30, 000 hii ni kero ya muda mrefu na hakuna utatuzi,”amesema.

Mkazi wa Goba, aliyejitambulisha kwa jina moja la Lastanza, naye alikiri uwepo wa shida ya maji akisema walikuwa wanapata maji mara tatu kwa wiki (Ijumaa, Jumamosi na Jumapili) lakini sasa hawapati hata mgao.

 “Wiki iliyopita tulipata maji Ijumaa tangu hapo hatujapata tena, tunanunua maji ya chumvi lita 1,000 kwa Sh15,000 lakini maji ya Dawasa yakitoka kwa mwezi bili ni Sh12,000 kama maji tumetumia kwa wingi,”amesema Lastanza.

Kwa upande wa eneo la Kimara King’ongo, Kata ya Saranga wilayani Ubungo upatikanaji wa maji umeendelea kuwa changamoto kwa takribani mwaka mmoja sasa.

Mkazi wa eneo hilo, Amina Shabani amesema awali angalau yalikuwa yakitoka walau mara moja au mara mbili kwa wiki (Jumanne na Alhamisi), lakini sasa yanaweza kupita miezi miwili hadi mitatu bila ya kupata maji hata siku moja.

“Hata yakitoka hiyo mara moja moja ni nyakati za usiku wa manane ambao watu wanakuwa wamelala, hivyo kusababisha wakazi wa eneo hilo kushindwa kupata huduma hiyo muhimu kwa ustawi wa afya ya binadamu.

 “Dumu la maji ya bomba tunanunua kwa kati ya Sh500 hadi Sh700, kwa yale ya chumvi hugharimu Sh300 hadi Sh400, hii inatuumiza sana kutokana na kuongezeka kwa gharama za maisha,” amesema.

Kwa upande wa Tabata (Ilala), Petro Shaban amesema maji ni changamoto na hununua kati ya Sh400 hadi Sh500 huduma ambayo huongeza gharama za maisha.

Vipi kuhusu ripoti?

Hata hivyo, wakati hayo yakisemwa, ongezeko la watu ni moja ya sababu iliyotajwa katika Ripoti ya Taarifa ya Utendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 kuwa haiendani  na kiwango cha maji kinachozalishwa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, uzalishaji maji ulifikia lita milioni 685 mwaka 2023/24 kutoka lita milioni 593 mwaka uliotangulia, lakini kiwango cha maji kilichozalishwa kilikuwa ni asilimia 45 pekee ya mahitaji ya maji katika maeneo yanayohudumiwa na mamlaka hizo.

 Ukilinganisha na miaka ya nyuma, uwiano wa uzalishaji dhidi ya mahitaji ya maji uliopo sasa umepungua kutoka asilimia 47 katika mwaka wa fedha 2022/23 na asilimia 48 katika Mwaka wa Fedha 2021/22.

Ongezeko la watu pia ni moja ya sababu iliyotajwa katika ripoti hii ambayo haiendani na kiwango cha maji kinachozalishwa.

Uzalishaji maji ulifikia lita milioni 685 mwaka 2023/24 kutoka lita milioni 593 mwaka uliotangulia lakini kiwango cha maji kilichozalishwa kilikuwa ni asilimia 45 pekee ya mahitaji ya maji katika maeneo yanayohudumiwa na mamlaka hizo.

 Ukilinganisha na miaka ya nyuma, uwiano wa uzalishaji dhidi ya mahitaji ya maji uliopo sasa, umepungua kutoka asilimia 47 katika mwaka wa fedha 2022/23 na asilimia 48 mwaka wa fedha 2021/22.

Katika kukabiliana na changamoto ya upotevu wa maji, Ewura iliandaa miongozo mbalimbali ukiwamo Mwongozo wa Kupunguza Upotevu wa Maji wa Mwaka 2021 ambao unazitaka mamlaka za maji kuhakikisha upotevu wa maji hauzidi asilimia 20 ya maji yanayozalishwa.

Pia, upo mwongozo wa kuchagua, kufunga, kupima na kufanyia matengenezo dira za maji kwa mamlaka za maji mwaka 2021, unaozitaka mamlaka za maji kuwa na sera ya dira za maji na kanzidata.

“lli kuhakikisha kunakuwa na udhibiti wa upotevu wa maji na kufikia lengo la kupunguza upotevu huu, uchambuzi umefanyika katika viashiria mbalimbali na mamlaka za maji na usafi wa mazingira zinatakiwa kuandaa na kutekeleza mikakati ya kupunguza upotevu wa maji,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Mwongozo wa Ewura wa Kupunguza Upotevu wa Maji wa Mwaka 2021 unasisitiza pia juu ya kuandaa mizania ya kupima viwango vya upotevu wa maji kwa mujibu wa mwongozo wa Jumuiya ya Kimataifa ya Majl (IWA) ili kujua maeneo ya upotevu wa maji kwenye mamlaka hizo.

Kwa Mwaka wa Fedha 2023/24, mamlaka za maji 25 kati ya 82 zilikuwa na mikakati iliyoidhinishwa ya kupunguza upotevu wa maji ikilinganishwa na mamlaka za maji 17 katika Mwaka wa Fedha 2022/23.

Mamlaka hizo ni Gairo, Iringa, Dodoma, Dawasa, Utete, Makonde, Bariadi, Biharamulo, Bukoba, Bunda, Busega, Maswa, Musoma, Ngara, Babati, Tanga, Arusha, Moshi, Igunga, Kahama, Nzega, Shinyanga, Kashwasa, Karatu na Orkesumet.

Aidha, mamlaka zote za maji 82 ziliandaa mizania ya kupima viwango vya upotevu wa maji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *