Majeruhi Arsenal wampa kigugumizi Arteta

LONDON, ENGLAND: Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amezidi kupata pigo kwa orodha ya wachezaji wenye majeraha kuongezeka huku mechi ya robo fainali ya mkondo wa kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid ikizidi kukaribia.

Mastaa wake katika eneo la ulinzi ikiwemo Gabriel Magalhaes na Jurrien Timber waliongezeka katika orodha ya majeruhi baada ya kuumia katika mechi dhidi ya Fulham, Jumanne ya wiki hii.

Gabriel, anayecheza kama beki wa kati, aliondoka uwanjani akiwa na maumivu ya misuli ya paja kabla ya Timber kupata tatizo la goti na kushindwa kuendelea.

Ben White naye hakuwepo kwenye kikosi cha mechi hiyo na kuna shaka kubwa kama atashiriki kwenye mechi ya Ulaya kutokana na majeraha ya goti kama ilivyo kwa Riccardo Calafiori.

Arteta amekiri kwamba anahisi wasiwasi kuhusu Gabriel. “Najiwazia, kwa sababu yeye hafurahii kamwe kutoka uwanjani na alilazimika,” alisema kocha huyo mwenye umri wa miaka 43. 

Mtihani mkubwa kwa Arteta ni namna atakavyopanga kikosi chake kuziba nafasi za mastaa ambao huenda wasiwepo katika mchezo wao muhimu dhidi ya Madrid.

Kabla ya mchezo huo dhidi ya Madrid, Arsenal bado watahitaji kujichunga kumaliza mechi yao dhidi ya Everton bila majeraha kwa wachezaji ukiwa ndio mchezo wa mwisho kabla ya kuwavaa vijana hao wa Carlo Ancelotti katika dimba la Emirates.

Kocha huyu anaweza kufukia mashimo ya wachezaji ambao wamepatwa na majeraha kwa kusuka kikosi chake kwa njia hii.

Kwanza kama kawaida eneo la langoni ni kipa David Raya, kisha Thomas Partey anaweza kucheza kama beki wa kulia badala ya Timber na White, hili ni eneo ambalo kiungo huyu ameshawahi kucheza.

Katika eneo la beki wa kati ambapo Gabriel ameumia kuna uwezekano akamtumia Jakub Kiwior acheze pacha na William Saliba. 

Uwepo wa Partey kwenye eneo la ulinzi unaweza kumfanya Mikel Merino kurudi katikati ya uwanja kucheza kama kiungo katikati ya Declan Rice na Martin Odegaard.

Mbadala mwingine wa kuziba la eneo la kati ingekuwa ni kwa Kieran Tierney kuingia kwenye kikosi akaenda kucheza eneo la beki wa kushoto kisha Myles Lewis-Skelly apanda kucheza katikati ya uwanja. 

Ikiwa Arteta atachagua kumrudisha Merino kwenye eneo la kiungo ambalo ni asili yake, Leandro Trossard anaweza kuingizwa kikosini kisha akacheza kama mshambuliaji wa kati, pembeni akisaidiwa na Bukayo Saka pamoja na Gabriel Martinelli.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *