
Same. Majeruhi 46 kati ya 75 wa ajali mbili tofauti ikiwemo iliyoua wanakwaya sita wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mmeni Chome, Dayosisi ya Pare, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro wameruhusiwa baada ya afya zao kuimarika.
Ajali ya kwanza iliyoua wanakwaya sita na kusababisha majeruhi 23. Ilitokea Machi 30, 2025 eneo la Barabara ya Bangalala, wilayani humo wakati wakitokea Chome kuelekea Vudee kwa ajili ya shughuli ya uinjilishaji ambapo gari walilokuwa wakisafiria aina ya coaster lilikosa mwelekeo na kupinduka katika milima ya Pare.
Waliofariki katika ajali hiyo ni, Namsifu Chedi Mbula(79), Mbazi Ahadi Mjema(14), Paulo Kadio Mchome(40), Christina Nzinyangwa Kirumbi(60), Agness Elikunda Mchome (59) na Niwaeli Ombeni Ngeruya(74).
Sambamba na ajali hiyo pia, kulitokea ajali nyingine eneo la Njoro wilayani humo, ambapo basi la Kampuni ya Osaka lililokuwa likitokea Moshi kwenda Dar es salaam lilipata ajali na kusababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhi 53 ambao walilazwa Hospitali ya Wilaya ya Same na wengine kupelekwa Hospitali ya KCMC.
Machi 30, mwaka huu Mkuu wa Wilaya hiyo, Kasilda Mgeni aliliambia Gazeti hili kuwa, chanzo cha ajali hiyo ni gari walilokuwa wakisafiria wanakwaya hao kupata hitilafu wakati likipanda mlima hivyo kupinduka katika milima hiyo, huku akitoa tahadhari kwa madereva wanaotumia barabara kuu ya Same, kuhakikisha wanaendesha kwa tahadhari kutokana na upepo mkali uliopo eneo hilo.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Same, Dk Alex Alexandra amesema hali za majeruhi 16 waliolazwa hospitalini hapo na 13 waliopewa rufaa kwenda Hospitali ya KCMC wanaendelea na matibabu.
“Mpaka sasa majeruhi 46 wameruhusiwa kurejea nyumbani baada ya afya zao kuimarika, ambapo kati yao wanawake ni 11 na wanaume ni 35, lakini majeruhi wengine 13 tumewapa rufaa Hospitali ya KCMC kwa uchunguzi zaidi,” amesema Dk Alexandra
Dk Alexandra amesema mpaka sasa hakuna idadi ya vifo vilivyoongezeka kutokana na ajali hizo mbili, huku akieleza kuwa hali za majeruhi waliopo hospitalini hapo wanaendelea vizuri na matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kanisa hilo jana, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu ataongoza mamia ya waombolezaji katika ibada maalumu ya kuaga miili ya wanakwaya hao katika Kanisa Kuu la KKKT Dayosisi ya Pare(cathedral).