Majeraha janga jipya England

LONDON, ENGLAND. Hali ya majeraha kwa timu za Ligi Kuu England imeendelea kuwa mbaya siku hadi siku huku chama cha wachezaji wa soka la kulipwa kikidai idadi kubwa ya mechi ni janga linalosababisha hali hiyo.

Takwimu zinaonyesha wachezaji muhimu wa timu mbalimbali tangu kuanza kwa msimu huu wamekosa mechi 232 kutokana na majeraha ya aina mbalimbali.

Ndani ya wiki hii, timu ya taifa ya England itakayocheza dhidi ya Ugiriki na Ireland itakuwa inawakosa wachezaji wake wanane ambao ni majeruhi.

England itakuwa inawakosa mastaa wake Declan Rice, Bukayo Saka, Phil Foden na Jack Grealish ambao imethibitishwa kwamba wana majeraha na wengine ambao wana hatihati ni pamoja na Cole Palmer, Levi Colwill, Trent Alexander-Arnold na Aaron Ramsdale ambao walitolewa nje katika michezo yao ya mwisho ya ligi baada ya kushindwa kuendelea.

Mastaa wengine ambao hawatokuwepo ni John Stones, Harry Maguire, Kobbie Mainoo, Luke Shaw na Eberechi Eze.

Ripoti inaeleza hali inaweza kuwa mbaya zaidi mwakani kwa sababu baada ya mapumziko ya kupisha kalenda ya FIFA, timu za EPL zitakuwa na mechi 12 kucheza ndani ya wiki saba ikiwa ni mjumuisho wa michuano ya Ulaya, robo fainali za Carabao na Ligi Kuu England.

Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola, msimu huu mapema alimpoteza Rodri ambaye atakuwa nje kwa msimu mzima, sawa pia na Oscar Bobb ambaye majeraha yamesababisha asicheze tangu kuanza kwa msimu.

Kocha huyu ambaye amekiri matumaini ya kushinda ubingwa ni madogo kwa sababu ya majeraha kwa nyota wake pia ana wasiwasi wa kuwakosa Grealish, Kevin De Bruyne, Nathan Ake na Foden.

Vilevile hali inaweza kuwa mbaya zaidi mwakani kwani ligi itakapomalizika Guardiola na kikosi chake hawatapata muda mwingi wa kupumzika kwani mwakani watatakiwa kushiriki michuano ya Kombe la Dunia la Klabu ambalo pia litakuwa na mechi nyingi.

Msimu huu wachezaji wa Man City ambao ni majeruhi wamekosa jumla ya mechi 42 za Ligi Kuu England.

Kwa upande wa Manchester United hali ya majeraha nayo imeonekana kuwatesa sana na kocha aliyefukuzwa Erik Hag alikuwa akilalamika sana kuhusu majeraha akieleza ilikuwa sababu mojawapo ya timu yake kufanya vibaya.

Mastaa wa Man United kiujumla wakiwamo mabeki wake wa kushoto Luke Shaw na Tyrell Malacia, wamekosa mechi 57 hadi sasa.

Liverpool pia ni waathirika wakiwa wameikosa huduma ya kipa wao Alisson Becker  kwa mwezi mzima na Diogo Jota katika mechi kadhaa zilizopita na sasa iko hatarini kumkosa beki wao Alexander-Arnold kwa zaidi ya wiki nne kutokana na tatizo la misuli ya paja.

Arsenal ambayo imekuwa katika kiwango cha chini katika michezo ya hivi karibuni ikishindwa kupata ushindi kwenye mechi nne mfululizo, mara kadhaa imewakosa mastaa wake Saka, Riccardo Calafiori na Ben White pamoja na kapteni Martin Odegaard aliyerejea hivi karibuni.

Hali ya majeraha imezidi kuwa mbaya sana katika misimu mitatu iliyopita na ripoti zilizotolewa na taasisi ya Howden zinaonyesha kwamba msimu uliopita timu za Ligi Kuu England zililipa Pauni 266 milioni kama mshahara kwa wachezaji ambao hawakuwa na uwezo wa kucheza kutokana na majeraha na Man United ndio ilikuwa ikiongoza.

Rais wa PFA, Maheta Molango, alisema yote haya yanatokana na ratiba mbovu ambayo inahusisha mechi nyingi.

“Wachezaji wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu kuhusu athari za ratiba ya mechi nyingi, nafikiri sasa hata mashabiki watakuwa wanaona wenyewe wanapoangalia idadi ya wachezaji walioumia. Ni muhimu kuwa na namba na ushahidi juu ya madhara ya kucheza mechi nyingi ili tuweze kutoa hoja na kuhitaji muda wa kupumzika wa kutosha na idadi ya mechi. Inabidi pale wanapokuwa wanapanga ratiba wazingatie na kuwa na uelewa wa mipaka ya kimwili ya wachezaji,” alisema Malongo na kuongeza;

“Daima tunasema kwamba hili sio suala la faida kwa mchezaji pekee, ni suala la soka kiujumla. Mashabiki wanalipa ili kuwaona wachezaji bora wakishindana, lakini hilo haliwezi kutokea ikiwa wanakuwa majeruhi kila wakati.”