Majanga Arsenal, Gabriel, Timber wakiumia

Wasiwasi umetanda ndani ya Arsenal wiki moja kabla ya kuivaa Real Madrid katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya wachezaji wake wawili tegemeo wa safu ya ulinzi, Gabriel Magalhaes na Jurrien Timber kupata majeraha kwenye mchezo wa Ligi Kuu England (EPL) jana, Jumanne, Aprili Mosi, katika Uwanja wa Emirates dhidi ya Fulham.

Katika mchezo huo, Arsenal iliibuka na ushindi wa mabao 2-1, ikifunga kupitia kwa Mikel Merino na Bukayo Saka huku la Fulham likifungwa na Rodrigo Muniz.

Gabriel alifanyiwa mabadiliko mapema katika dakika ya 16 ya mchezo kumpisha Jakub Kiwior baada ya kupata maumivu yalioonyesha kuwa ya nyama za paja na katika dakika ya 77, Jurrien Timber alilazimika kumpisha Leandro Trossard baada ya kupata majeraha yaliyoonekana kuwa ya goti.

Jumamosi wiki hii, Arsenal itakuwa ugenini dhidi ya Everton katika mechi ya EPL lakini wasiwasi mkubwa ni wachezaji hao kukosekana katika mechi ya mkondo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid, Aprili 08, 2025.

Meneja wa Arsenal, Mikel Arteta amesema kuwa hana uhakika kama wachezaji hao wataivaa Real Madrid au la na majibu ya mwisho yatapatikana baada ya nyota hao wawili kufanyiwa vipimo kujua ukubwa wa majeraha yao.

“Hatujui ukubwa wake (jeraha) na Timber pia. Alikuwa anapata shida tangu mwanzoni mwa mchezo. Aliweza kujitahidi kuendelea na kwa pointi fulani akashindwa kwa hiyo hiyo ndio hasara yake,” alisema Arteta.

Magalhaes amekuwa mtu muhimu wa Arsenal katika safu yao ya ulinzi tangu alipojiunga nayo mwaka 2020 akitokea Lille ya Ufaransa ambapo katika kipindi hico hadi sasa, Arsenal imekuwa na uhakika wa asilimia 63.5 za ushindi katika mechi 159 alizoichezea na pindi alipokosekana katika mechi 22, Arsenal imekuwa na asilimia 40.9 tu za ushindi.

Arsenal imekuwa na mkosi wa majeraha ya mara kwa mara kwa wachezaji wake msimu huu na ikiwa itawakosa Timber na Gabriel, timu hiyo itakuwa kwenye wakati mgumu dhidi ya Real Madrid.

Majeraha ya wawili hao yanatokea katika kipindi ambacho Arsenal inawakosa mabeki wengine watatu ambao ni Ben White, Takehiro Tomiyasu na Riccardo Calafiori ambao wote wanauguza majeraha ya goti.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *