Nachingwea. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kukuza usawa wa kijinsia na kwamba hakuna mwanamke atakayebaguliwa katika uongozi na ajira.
Majaliwa amebainisha hayo leo Alhamisi Machi 6, 2025 huko Nachingwea mkoani Lindi kwenye kongamano la wanawake wa kanda ya kusini kuelekea kilele cha Siku ya Kimataifa ya Wanawake Machi 8, 2025.
Amesema Serikali imesaini mikataba ya kumlinda mwanamke ambapo ni azimio la mwaka 1977 ya nchi wanachama ya Umoja wa Mataifa.
“Chimbuko la siku ya mwanamke duniani lilitokana na wanawake wafanyakazi wa sekta ya viwanda Marekani kupinga vitendo vya kutopewa huduma za kijamii katika maeneo yao ya kazi. Vilevile kulikuwa na unyanyasaji wa ajira kwenye maeneo yao, walipinga mshahara mdogo huku wakifanya kazi sawa na wengine,” amesema Majaliwa.
Kutokana na hayo, amesema Serikali baada ya kusaini mikataba ya kumlinda mwanamke watahakikisha wanawake katika sehemu za kazi hakuna kubaguliwa.
“Niwahakikishie wanawake wote nchini hakuna mwanamke atakayebaguliwa katika ajira au uongozi,” amesema.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB), Adam Mihayo amesema kwa sasa benki yao imekuwa ikitoa mikopo kwa wanawake wa zaidi ya Sh300 bilioni.
“Benki yetu imetoa mikopo kwa wanawake zaidi ya Sh300 bilioni na pia tumekuja na mabadiliko ya fursa kwa kanda ya kusini kwa kuangalia biashara kwa wanawake na kuwapa mikopo,” amesema Mihayo.

Naye Stella Andrea kutoka Taasisi ya Utafiti (Tari _Naliendele) amesema taasisi yao imetoa mchango mkubwa kwa wanawake kwa kuwapa mbegu bora za korosho, ufuta ili kuongeza mnyororo wa thamani.
Mkazi wa Nachingwea, Sofia Jumbe amesema kongamano hilo litasaidia kuleta chachu katika maendeleo kwa kupata elimu mbalimbali ikiwemo jinsi ya kupanda mbegu bora hasa kwenye zao la korosho, ambalo ni zao la mkakati kwa kanda ya kusini.
“Tari wametupa elimu bora ambayo itatusaidia wanawake tunaolima korosho kupata mavuno mengi na kuongeza thamani katika mazao hayo,” amesema Jumbe.
Kongamano hilo kanda ya kusini limejumuisha wanawake kutoka Lindi, Mtwara na Ruvuma.