Majaliwa awataka wanawake kuchangamkia fursa za mikopo TCB

Nachingwea. Serikali imewataka wanawake kuchangamkia fursa za mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri zote nchini ili kujiendeleza kiuchumi.

Pia wametakiwa kuitumia Benki ya Taifa ya Biashara (TCB), ambayo ni miongoni mwa taasisi za fedha zilizopewa jukumu la kuratibu mikopo hiyo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema hayo leo Alhamisi Machi 6, 2025 kwenye kongamano la maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani (IWD), Kanda ya Kusini, lililofanyika kwenye viwanja vya Maegesho, wilayani Nachingwea, mkoani Lindi. Kongamano hilo lilijadili mada kadhaa kuhusu mustakabali wa wanawake.

Majaliwa amesema benki ya TCB imejipanga vizuri kuwawezesha kupata mikopo kwa riba nafuu, hivyo kila wilaya mkoani Lindi na maeneo mengine nchini inapaswa kuchangamkia fursa hiyo.

“Amua leo hutokwama, unataka mkopo utapata, fanya uamuzi wako leo. Nimeleeza hayo muone namna TCB ilivyokuja mbele yenu kutangaza fursa na kuwafungulia milango. Kuna bidhaa nyingi wamezieleza hapa kwenu, hizi zitawasaidia kuanzisha biashara,” amesema.

Kwa mujibu wa Majaliwa, taasisi za fedha zinazoratibu mchakato wa makundi ya wanawake, vijana na wenye ulemavu kunufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani ya halmashauri, zitayarahisisha makundi hayo kupata mikopo kwa haraka.

Serikali imeanza kutekeleza utaratibu mpya unaoziwezesha benki na taasisi za fedha nchini kusimamia utoaji wa mikopo kwa makundi hayo ili kuhakikisha walengwa waliokusudiwa wananufaika.

Awali, Serikali ilisimamisha utaoji mikopo hiyo kutokana na walionufaika kutoirejesha kwa wakati na wengine kutorejesha, hivyo kuathiri utekelezaji wa mkakati huo unaolenga kuwainua wanawake, vijana na wenye ulemavu kiuchumi na kuchochea maendeleo ya Taifa.

Baadhi ya watendaji wasio waaminifu na wanasiasa walidaiwa kupenyeza vikundi hewa kwa ajili ya kunufaika na mikopo hiyo, ikashauriwa kubadilishwa utaratibu wa utoaji kuhakikisha tija inapatikana.

Mkurugenzi Mtendaji wa TCB, Adam Mihayo amesema katika sekta ya uwezeshaji, taasisi hiyo imejipanga vema kuimarisha eneo la rasilimali watu ili kutoa huduma bora ya mikopo kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu.

Mihayo amesema TCB imekuwa mstari wa mbele kusimamia usawa wa kijinsia, ndiyo sababu Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu iliwapa heshima ya uenyekiti wa kamati ya kimataifa ya kuwaleta wanawake kwenye jukwaa la uwezeshaji.

“Tuko tayari kuwahudumia kupitia bidhaa zetu kwenye matawi yetu kote nchini. Tuna bidhaa ambazo ni maalumu kwa wanawake kwa kuwa tuna jukumu la kuhakikisha tunaendeleza ustawi na uwezeshaji wa wanawake nchini,” amesema.

Amesema benki hiyo imeboresha akaunti ya Tabasamu ambayo ni mahususi kwa wanawake.

Akaunti ya Tabasamu ilizinduliwa Machi 28, 2019 na Rais Samia Suluhu Hassan wakati huo akiwa Makamu wa Rais.

Amesema baada ya kufanyika maboresho makubwa yanayolenga kumuinua mwanamke wa Kitanzania wa sasa na wa baadaye, akaunti hiyo itazinduliwa upya.