Majaliwa ataka viongozi wa dini kukemea mmomonyoko wa maadili

Arusha. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa dini nchini kuendelea kukemea vitendo vinavyochangia mmomonyoko wa maadili, kama vile matumizi ya dawa za kulevya.

Majaliwa amesema hayo leo, Februari 26, 2025, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Maridhiano Kitaifa (Maridhiano Day) yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).

Akizungumza kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, amesisitiza kuwa, ingawa Serikali ina sheria na vyombo vya dola, mchango wa viongozi wa dini ni muhimu katika kuhamasisha jamii kuhusu maadili mema na kupambana na matumizi ya dawa za kulevya.

Majaliwa amesema changamoto zinazokumba taifa ni pamoja na mabadiliko ya teknolojia na ushawishi wa tabia za Magharibi, ambazo zinachangia mmomonyoko wa maadili.

Ametoa mfano wa matumizi ya dawa za kulevya kama vile bangi na kusema kuwa Serikali inaendelea na jitihada za kupambana na uingizaji wa dawa hizo kupitia vituo vya usafiri na njia zisizo rasmi.

“Mfano hapa Arusha kuna ile inaitwa ‘cha Arusha’ (bangi), haikubaliki. Tunataka kupunguza na kuondoa matumizi ya dawa za kulevya. Tumezuia dawa kuingizwa kupitia vituo vya mabasi, ndege, meli na njia za panya. Tunaendelea na kampeni, hivyo endeleeni kuwa walinzi.

“Hivi karibuni kumekuwa na wimbi, na tumelidhibiti. Mdhibiti amesema hakuna ushoga. Atakuja nani? Atatokea wapi?” amehoji Majaliwa.

Amesisitiza kwamba viongozi wa dini wana nafasi ya kutoa maelekezo na miongozo kwa jamii, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.

Kuhusu amani, Majaliwa amewasihi viongozi wa dini waendelee kushirikiana na Serikali ili kutoa sauti ya amani na mshikamano, hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Sheikh Alhad Mussa Salum, amesisitiza umuhimu wa kuondoa chuki katika jamii na kusema kuwa jumuiya hiyo itakuwa mstari wa mbele kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani.

Amewataka viongozi wenzake wa dini kuwa mfano wa kuheshimu na kuunga mkono utawala wa sheria na amani, akisema kuwa ni jukumu lao kulinda maadili ya jamii.

Sheikh Salum pia amekumbusha kwamba chuki kati ya watu husababisha machafuko, hivyo ni muhimu kuishi kwa kuheshimiana na kupendana.

Katibu Mkuu wa JMAT, Dk Israel Ole Maasa, amesema jumuiya hiyo imekuwa ikifanya kazi katika kusuluhisha migogoro, kutoa elimu kuhusu amani na kusaidia jamii katika maeneo mbalimbali.

Ameweka wazi kuwa JMAT itashirikiana na Serikali katika kuhakikisha amani inadumishwa, hasa wakati wa uchaguzi.

Mlezi wa JMAT, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, amesisitiza kuwa viongozi wa dini ni nguzo muhimu katika kuhakikisha amani inatawala nchini.

Amesema viongozi wa dini wanapokuwa na msimamo thabiti wa kuhubiri amani, upendo na mshikamano, jamii inafaidika.

Pinda ameomba Serikali iendelee kuwawezesha viongozi wa dini ili wafanye kazi yao kwa ufanisi na kuhakikisha amani inadumishwa.

Spika wa Bunge mstaafu, Anne Makinda, ametoa rai kwa wanasiasa kuheshimu uongozi uliopo na kuepuka tamaa ya madaraka, ambayo inaweza kuleta machafuko nchini.

Amesema wakati wa uchaguzi, ni muhimu kwa wanasiasa kuheshimu mchakato wa kidemokrasia na kuhakikisha amani haivunjiki.

Kiongozi mkuu wa jamii ya kifugaji, Laigwanan Ole Kisongo, ameiomba Serikali kusaidia umoja wa jamii hiyo ili uweze kujitegemea na kusaidia wananchi katika masuala ya kisheria na haki za kijamii.

Amewataka viongozi wa JMAT kuhakikisha haki inatolewa kwa wananchi na kutoa wito wa kupata rasilimali na fedha ili watekeleze majukumu yao kwa uhuru na ufanisi.